Unajua faida ya mbegu za ubuyu?

Unapomung’unya ubuyu huwa unatafuna na mbegu zake? Au huwa hutafuni? Kama huwa hutafuni mbegu zake basi unakosa uhondo na faida inayopatikana katika tunda hilo.

Ubuyu ni tunda kama yalivyo matunda mengine, huimarisha kinga ya mwili na mifupa na hapa tunazungumzia ubuyu halisi (fresh) ambao haujachanganywa rangi, ladha wala kitu kingine.

Hata hivyo, wakati nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, zikiendelea na mapambano ya Uviko-19, jamii haina budi kula vyakula na matunda yenye uwezo wa kupandisha kinga ya mwili.

Ofisa Lishe wa Mkoa wa Dodoma, Heriet Nyange anasema moja ya faida kubwa iliyopo katika ubuyu halisi, una vitamini C nyingi zaidi kuliko matunda jamii ya machungwa na kizuri zaidi huongeza damu mwilini.

“Ubuyu una vitamini C nyingi, mara tano ya ile inayopatikana katika matunda jamii ya machungwa,” anasema Nyange.

Pia, anasema mbali na vitamini C, ubuyu una vitamini A, E, B2 pamoja madini ya chuma, calcium, magnesium, potasium, folic, zinki na protini.

“Tunda hili pia lina wanga, hivyo raha ya kula ubuyu utafune na mbegu zake na ule ubuyu ambao ni halisi, yaani haujawekwa rangi wala ladha,” anasema Nyange.

Anazitaja faida za ubuyu na mbegu zake mwilini kuwa husaidia kuimarisha kinga ya mwili, huimarisha afya ya mifupa, husaidia katika mfumo wa umeng’enyaji na huongeza damu mwilini.

Pia, huondoa tatizo la kukosa choo kutokana na kwamba ubuyu una nyuzi nyuzi ambazo husaidia kurekebisha matatizo ya umeng’enywaji wa chakula.

“Faida nyingine ni kwamba tunda hili huondoa sumu na mafuta mwili, hata majani ya ubuyu hutumika kama mboga kwa jamii ya Wagogo,” anasema Nyange.

“Wagogo huchuma majani ya ubuyu yale laini na kuyapika na hivyo kupata mboga aina ya mlenda.”

Kwa upande wa watoto wadogo wenye umri wa miezi sita na kuendelea, mtaalamu huyo wa lishe anashauri wachanganyiwe kidogo juisi ya ubuyu katika uji ili waweze kupata vitamini C na virutubisho vingi vitakavyomwezesha kuwa na afya nzuri.