Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wagonjwa wa moyo kupata majibu ndani ya dakika tano JKCI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 15, 2026 kuhusu Wiki ya Uhamasishaji wa Huduma za maabara baada ya uzinduzi wa maabara hiyo inayotumia roboti na teknolojia ya AI  kurahisha upatikanaji wa majibu. Picha na Said Powa

Muktasari:

  • Maabara hiyo inayotumia akili unde katika uchunguzi wa sampuli imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Afrika Mashariki kwa hospitali zinazomilikiwa na Serikali kutumia teknolojia hiyo katika uchunguzi wa sampuli za wagonjwa.

Dar es Salaam. Ile hali ya kutumia dakika 30 kusubiri majibu ya vipimo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inabaki historia, baada ya taasisi hiyo kusimika mtambo wa Akili Unde (AI) utakaotoa majibu ndani ya dakika tatu.

Kwa mujibu wa JKCI, mtambo huo wa AI una uwezo wa kuchakata sampuli 4,000 za wagonjwa kwa saa na kutoa majibu ndani ya dakika tatu hadi nane, bila kuhitaji uingiliaji wa binadamu.

Tayari, taasisi hiyo imeanza kuwajengea uwezo wataalamu wake wa maabara kutumia teknolojia ya akili unde (AI) katika utoaji wa huduma.

Akizungumza leo, Juni 15, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Juni 15 hadi 17, 2026.

Amesema maabara hiyo inayotumia akili unde katika uchunguzi wa sampuli imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Afrika Mashariki kwa hospitali zinazomilikiwa na Serikali kutumia teknolojia hiyo katika uchunguzi wa sampuli za wagonjwa.

Akizungumzia uwekezaji huo, amesema mitambo hiyo yenye thamani ya Sh9 bilioni ina uwezo wa kubaini magonjwa katika hatua za awali kabisa, akitolea mfano malaria ambao unaweza kubainika kabla ya mgonjwa kuanza kuonyesha dalili.

Baadhi ya wataalam wa maabara wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wakitumia roboti kuchakata taarifa za uchunguzi. Picha na Said Powa

Amesema taasisi hiyo imeanza kutoa mafunzo kwa wataalamu wa maabara kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili unde katika uchakataji wa sampuli za wagonjwa.

"Sasa mgonjwa ambaye alikuwa akisubiri majibu kwa zaidi ya nusu saa hatalazimika kufanya hivyo tena. Atapata majibu ndani ya dakika tatu hadi nane," amesema Dk Kisenge.

Amesema hatua hiyo itasaidia wagonjwa wanaoweza kupata madhara kutokana na kuchelewa kwa majibu ya vipimo, akieleza kuwa kwa baadhi ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo, muda wa kupata majibu ni muhimu katika kuokoa maisha yao.

Kwa mujibu wa Dk Kisenge, kuwepo kwa maabara hiyo pia utasaidia kupunguza gharama zinazotokana na muda mrefu wa kusubiri majibu ya vipimo.

Amesema maabara hiyo imekuwa kivutio kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku taasisi mbalimbali zikianza kuwasiliana na JKCI kwa ajili ya ushirikiano katika tafiti za kisayansi.

"Lipo shirika limetuomba tushirikiane kufanya utafiti, na utafiti huo unaweza kuiingizia nchi dola za Marekani milioni tano. Fedha hizi zinakuja kutokana na uwekezaji tulioufanya," amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kampuni ya Roche Afrika Mashariki (iliyohusika katika usimikaji wa maabara hiyo), Taofik Oloruko-Oba, ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

Amesema maabara hiyo itachangia kuongeza ufanisi wa huduma za matibabu na kupunguza haja ya kusafirisha sampuli za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi wa kina.

Naye, Mkuu wa Maabara wa JKCI, Thadei Kavishe, amesema ushiriki wa binadamu katika uendeshaji wa mfumo huo ni mdogo kwa kuwa sehemu kubwa ya kazi inafanywa na teknolojia.

"Uandaaji wa sampuli, uchakataji wake na utoaji wa majibu vinafanyika kwa kiwango kikubwa bila uingiliaji wa binadamu.”

"Tayari tumealika wakuu wa maabara kutoka sehemu mbalimbali nchini kuja kujadili maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwani sasa sisi ndiyo tuna teknolojia hii," amesema Kavishe.