Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Atolewa uvimbe kwenye kizazi uliomtesa kwa miaka 10

Muktasari:

  • Uchunguzi wa jopo la madaktari waligundua mwanamke huyo alikuwa na uvimbe tumboni, ambao pia uliomsababishia kutofanya shughuli zake za kila siku za kujiingizia kipato.

Dar es Salaam. Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji, wamefanikiwa kutoa uvimbe wenye uzito wa gramu 800 kwenye kizazi cha mwanamke mwenye umri wa miaka 49 alioishi nao kwa miaka 10, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini.

Mwanamke huyo alifanyiwa upasuaji Septemba 17, 2024 na timu ya madaktari bingwa kupitia kampeni ya huduma za madaktari bingwa bobezi wa (Rais) Samia Suluhu Hassan.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Emmanuel Ngadaya kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kusini katika Halmashauri ya Nanyumbu, aliyeongoza jopo la madaktari hao amebainisha hilo mara baada ya kukamilika kwa upasuaji huo juzi.

Ngadaya ameeleza kuwa wakiwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo walipokea mgonjwa aliyekuwa na tatizo la uvimbe kwenye kizazi kwa zaidi ya miaka 10.

“Mara baada ya uchunguzi, tukagundua kuwa amekuwa na hali ya uvimbe tumboni uliomsababishia kutofanya shughuli zake za kila siku za kujiingizia kipato,” ameeleza.

Ameongeza kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya Mangaka iliyopo Halmashauri ya Nanyumbu ambapo madaktari bingwa wameweka kambi hiyo, waligundua kuwa uvimbe wake unahitaji kufanyiwa upasuaji.

Aidha amesema wanafanya utaratibu wa kuusafirisha uvimbe uliotolewa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa vipimo na uchunguzi zaidi.

Mgonjwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, baada ya upasuaji amemshukuru Rais Samia, kwa kujali wananchi wake na kuwasogezea huduma za kibingwa karibu kwani hakuwa na uwezo wa kusafiri na kulipia gharama za matibabu.

“Leo najisikia vizuri hata hamu ya kula nimepata, awali kabla ya upasuaji nilikuwa hata hamu ya kula sina namshukuru sana mama (Rais) Samia kwa hii kampeni yake ya huduma za madaktari bingwa bobezi ambayo imesaidia kuondolewa uvimbe ulionitesa kwa muda wote huo na kushindwa kufanya kazi za kuniingizia kipato,” amesema.

Kampeni hii ilianza septemba 16, 2024 ambapo itadumu kwa muda wa siku sita, huduma za kitabibu zitatolewa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mtwara.