Homa ya ini bado ni tishio, Serikali yasema...
Muktasari:
- Kauli hiyo imetolewa leo, Ijumaa, Aprili 10, 2026, Bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, wakati akieleza hali ya ugonjwa huo nchini na mikakati ya Serikali katika kudhibiti maambukizi.
Dodoma. Serikali imekiri kuwa ugonjwa wa homa ya ini bado ni changamoto ya afya ya umma nchini, licha ya kuwepo kwa chanjo na tiba, huku mikoa minne ikitajwa kuwa kinara kwa kiwango kikubwa cha maambukizi.
Kauli hiyo imetolewa leo, Ijumaa, Aprili 10, 2026, Bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati akieleza hali ya ugonjwa huo nchini na mikakati ya Serikali katika kudhibiti maambukizi.
Amesema licha ya chanjo kupatikana katika vituo vya afya nchini, bado mwitikio wa wananchi, hasa watu wazima, wa kujitokeza kupima na kupata chanjo ni mdogo, hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi.
“Tunawaasa Watanzania kwenda hospitalini kupima afya zao. Changamoto kubwa tuliyonayo kwa sasa ni mwitikio mdogo wa watu wazima kujitokeza kupata chanjo ya homa ya ini,” amesema Dk Samizi.
Ameeleza kuwa chanjo hiyo inapatikana bure katika vituo vya afya, ingawa kwa baadhi ya watu wanaolazimika kujilipia, huchangia Sh10,000 kwa kila sindano moja.
Dk Samizi alitoa ufafanuzi huo akijibu swali la Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza kutoa chanjo ya homa ya ini kwa Watanzania wote.
Akitoa takwimu za kitaifa, amesema utafiti unaonyesha asilimia 3.5 ya Watanzania wamebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, huku takwimu hizo zikihusisha wananchi waliokwenda kupima afya zao.
Hata hivyo, amesema baadhi ya mikoa ina kiwango kikubwa zaidi cha maambukizi, ambapo Katavi, Kigoma, Rukwa na Geita imebainika kuwa na wastani wa asilimia sita ya maambukizi ya homa ya ini.
Ameongeza kuwa kwa wajawazito, kiwango cha maambukizi kimefikia asilimia saba, hali inayoonyesha ukubwa wa tatizo hilo kiafya.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, chanjo ya homa ya ini pia ni sehemu ya ratiba ya chanjo kwa watoto wachanga, ambapo mtoto hupatiwa chanjo muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Amesema huduma hiyo hutolewa katika hospitali za ngazi zote, zikiwemo za Taifa, Kanda, Mikoa, Wilaya na Halmashauri, ili kuhakikisha watoto wanalindwa mapema dhidi ya maambukizi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Ikupa, amehoji kuhusu mkakati wa Serikali kuhakikisha wagonjwa wa afya ya akili wanapata dawa bure, hasa kwa kuwa wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za bima ya afya.
Akijibu hoja hiyo, Dk Samizi amesema Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayolenga kutoa msamaha wa gharama za matibabu kwa wananchi wasio na uwezo.
Ameeleza kuwa mpango huo unawahusu pia wagonjwa wa magonjwa sugu, yakiwemo saratani, Ukimwi, kisukari pamoja na matatizo ya afya ya akili.
Amesema kukamilika kwa utekelezaji wa mpango huo kutasaidia kuhakikisha wananchi wote wanaohitaji huduma za matibabu wanazipata bila kukumbana na vikwazo vya kifedha.