Ifahamu anemia, madhara yake na namna ya kuitibu

WaMtaalam wa maabara wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Gration Rwegasisa (kulia) akimtoa damu Arafa Said alipokuwa akitumia kifaa maalum cha kupimia ugonjwa wa Selimundu wakati wa uzinduzi wa kifaa kipya cha kupimia ugonjwa huo, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Maktaba

Anemia ni ugonjwa unaosababishwa na kiwango hafifu cha seli nyekundu za damu kwenye damu. Ugonjwa huu ukidumu kwa muda mrefu na kuwa mkubwa mwilini, unaweza kusababisha matatizo ya moyo na ya ogani zingine na muathirika anaweza kufariki dunia kama hata pata matibabu sahihi.

Sababu za mtu kuugua anemia

Wataalamu wa afya wanasema maradhi hayo husababishwa na matatizo makuu matatu ambayo ni upungufu wa damu, uzalishwaji hafifu wa seli nyekundu za damu na uharibifu wa seli nyekundu za damu kwenye damu.

Sababu hizi mara nyingi huchangiwa na matatizo mbalimbali ya kiafya. Tofauti na sababu hizi, matatizo mengine yanayoweza kusababisha anemia ni ya kupata hedhi inayopitiliza, ujauzito, vidonda vya tumbo, saratani ya utumbo mpana, matatizo ya kurithi, ulaji wa vyakula visivyo na madini ya chuma na vitamini B12 na maradhi yanayohusiana na damu ikiwamo seli mundu.

Tiba yake

Daktari atakufanyia vipimo vya anemia kwa kutumia vipimo vya damu. Tiba itategemea na aina ya anemia uliyonayo. Pamoja na sabau hizo kuu, baadhi ya wagonjwa wa anemia hupata pia ugonjwa huu kutokana na;

Upungufu wa damu ambao huchangia ugonjwa wa anemia kwa kiwango kikubwa. Upungufu huo unaweza kuwa ni wa muda mfupi au muda mrefu kulingana na chanzo chake.

Kupata hedhi ya kupitiliza au kuvuja kwa damu kwenye njia ya mmeng’enyo wa chakula au njia ya mkojo, kunaweza kusababisha upungufu wa damu.

Mgonjwa pia anaweza kupata upungufu wa damu baada ya kufanyiwa upasuaji, na hata saratani zinasababisha upungufu wa damu.

Kama kiasi kikubwa cha damu kikipotea, mwili pia unaweza kupoteza kiasi kikubwa cha seli nyekundu za damu na kusababisha anemia.

Uzalishwaji hafifu wa seli nyekundu za damu.

Matatizo yoyote ya kiafya ya kurithi na hata yale yanayopatikana baada ya kuzaliwa, yanaweza kusababisha uzalishaji hafifu wa seli nyekundu za damu na hivyo kusababisha anemia.

Matatizo haya ni pamoja na ya aina ya vyakula, matatizo ya viwango vya vichocheo mwilini (abnormal hormone level), baadhi ya maradhi sugu yanayodumu kwa muda mrefu ndani ya mwili na ujauzito pia.

Vyakula

Aina ya mlo wenye ukosefu wa madini ya chuma na vitamini B12, unaweza kuuzuia mwili ketengeneza seli nyekundu za damu kwa kiasi kinachohitajika.

Mwili unahitaji kiasi fulani cha vitamini C ili kuzalisha seli nyekundu za damu. Lakini matatizo yanayoweza kutokea kwenye mfumo wa utoaji wa takamwili, yanaweza kusababisha mwili kushindwa kuzalisha seli nyekundu za kutosha.

Maradhi mengine

Maradhi ya muda mrefu kama ya figo na saratani, mara nyingi huwa kikwazo kwa mwili kuzalisha seli nyekundu za damu, tiba za saratani za mionzi nazo huathiri urojo unaopatikana ndani ya mifupa (bone marrow) na zinaweza kuharibu uwezo wa damu kusafirisha oxygen kwenda sehemu za mwili.

Uboho unapoathiriwa kwa namna yoyote ile, hauwezi tena kuzalisha seli nyekundu za damu kwa kazi yoyote ile ili kuzirudisha zilizoharibika au zilizokufa.

Watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi au ugonjwa wa Ukimwi, wanaweza kuugua anemia kutokana na maambukizi mengine au dawa wanazotumia kupunguza makali ya VVU.

Mjamzito

Madaktari wanasema mjazito anakua hatarini sana kupata anemia kwa sababu katika kipindi hicho anakua na uhitaji mkubwa wa madini ya chuma kuliko kipindi cha kawaida.

Katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya ujauzito, ile sehemu ya damu ambayo ni majimaji yanayobaki kwenye damu baada ya damu kuganda (plasma) kwa mwanamke, huongezeka kwa kasi kuliko seli nyekundu za damu.

Hivyo kutokana na kuongezeka huko, inafanya damu iwe hafifu na hivyo kusababisha anemia. Wajawazito wanashauriwa kufuatilia ushauri wa kiafya mara kwa mara na kuendelea kutumia dawa zinazosaidia uzalishwaji wa madini ya chuma kwa kipindi chote cha ujauzito.

Watoto wanaozaliwa wapo hatarini zaidi.

Baadhi ya watoto wanaozaliwa bila kuwa na uwezo wa kuzalisha seli nyekundu za damu katika miili yao. Hali hii kitaalamu inaitwa ‘aplastic anemia’.

Watoto wachanga hata wale wa umri wa kawaida ambao hugundulika na aplastic anemia, kwa kawaida huwa wanahitaji kuchangiwa damu mara kwa mara ili kuongeza kiasi cha seli nyekundu za damu kwenye damu zao.

Baadhi ya sababu kama matumizi ya baadhi ya dawa walizotumia mama zao wakiwa wajawazito, sumu na baadhi ya maradhi ya kuambukiza yanaweza kusababisha anemia.

Dalili za anemia

Kwa kawaida, dalili za maradhi haya ni pamoja na mtu kujisikia uchovu. Uchovu huo ni ule wa viungo na mwili mzima pamoja na wa kiakili. Ukiwa na ugonjwa huu utakua unapata shida kufanya shughuli ambazo zinahitaji nguvu ya kawaida.

Dalili nyingine zinaweza kuwa kupata shida wakati wa kupumua, maumivu ya kichwa na pia wakati mwingine kupatwa na baridi sehemu za viganya na nyayo, mabadiliko madogo yanayotokea kwenye ngozi hasa rangi na maumivu ya kifua.

Dalili hizi zinatokea kwa sababu moyo unalazimika kutumia nguvu ya ziada ili kusukuma damu yenye hewa safi ya oksijeni kwenda sehemu zingine za mwili.

Pia, kuna mazingira hatarishi ambayo yanachangia mtu kuugua ugonjwa huu na hasa ukizingatia ukweli kwamba anemia huwapata watu wa rika zote, rangi zote na jinsia zote.

Hata hivyo, wanawake ambao wamefikisha umri wa kuzaa, wapo hatarini kuugua ugonjwa huo kutokana na kiasi cha damu wanachopoteza wakati wa mizunguko yao ya hedhi.

Hivyo, wanashauriwa kula vyakula vyenye madini ya chuma kwa wingi wakati wa hedhi ili kurudisha kiasi cha damu kinachopotea wakati huo.

Mazingira mengine hatarishi ni kama ya upotevu wa damu nyingi wakati wa kufanyiwa upasuaji, homa ya kukauka sehemu za maungio (rheumatoid athritis), Ukimwi, maradhi ya moyo na ‘thalassemia’.

Thalassemia ni aina ya ugonjwa wa damu unaozuia uzalishwaji wa seli nyekundu za damu kadri zinavyohitajika mwilini na uhafifu wa chembe chembe za kwenye damu zinazosaidia kusafirisha hewa ya oksijeni (hemoglobin).