Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinga mpya ya VVU ya sindano kuanza kutumika Januari 2027

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Lenacapavir ni dawa ya kisasa inayotolewa kwa njia ya sindano mara mbili kwa mwaka, tofauti na dawa za kila siku zinazotumika sasa katika kinga dhidi ya VVU (PrEP) na dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV).

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema sindano ya kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), Lenacapavir, inatarajiwa kuanza kupatikana nchini kuanzia Januari 2027, hatua inayotajwa kuwa mapinduzi katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Baadhi ya wananch wamepokea taarifa za ujio wa dawa hiyo  kwa matumaini, huku wakieleza matarajio yao juu ya upatikanaji na gharama zake.

Lenacapavir ni dawa ya kisasa inayotolewa kwa njia ya sindano mara mbili kwa mwaka, tofauti na dawa za kila siku zinazotumika sasa katika kinga dhidi ya VVU (PrEP) na dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV).

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 3, 2026, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, amesema maandalizi ya awali yanaendelea, huku wadau mbalimbali wa afya wakishirikiana kuhakikisha upatikanaji wa dawa hiyo unakuwa wa uhakika na wenye manufaa kwa Watanzania.

“Utekelezaji wake utaanza mwakani, Januari 2027. Kwa sasa wadau mbalimbali, hususan watekelezaji wanaofadhiliwa na Global Fund, wako kwenye vikao vya maandalizi ili kuhakikisha mfumo mzima wa upatikanaji na usambazaji unakuwa imara,” amesema Msasi.

Mkazi wa Dar es Salaam, Amina Juma (32), amesema dawa hiyo inaweza kuwa mkombozi kwa watu wanaopata changamoto ya kutumia dawa kila siku, lakini akasisitiza umuhimu wa kuifanya ipatikane kwa gharama nafuu.

“Kwa kweli hii ni habari njema, hasa kwa sisi ambao ratiba zetu ni ngumu. Lakini kama bei itabaki kuwa kubwa, itakuwa ni ndoto kwa watu wengi. Serikali iangalie namna ya kutusaidia wananchi wa kawaida,” amesema Amina.

Naye Othman Iddi (41), mkazi wa Morogoro, amesema elimu kwa umma inahitajika ili kuondoa hofu na unyanyapaa unaoweza kuambatana na matumizi ya dawa hiyo.

“Watu wengi bado wanaogopa hata kwenda kupima VVU, sasa hii sindano mpya inaweza kusaidia, lakini lazima kwanza watu waelimishwe vizuri. Bila elimu, hata dawa nzuri kiasi gani haitasaidia kufikia walengwa,” amesema.

Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni, Msasi alisema Lenacapavir itatumika zaidi kwa watu waliopata changamoto ya usugu wa dawa nyingine za ARV.

Sambamba na hao, ni wale wanaoshindwa kufuata ratiba ya matumizi ya dawa za kila siku. Aidha, dawa hiyo pia itatumika kama kinga kwa watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU.

Alisema tofauti na dawa nyingi za sasa zinazohitaji matumizi ya kila siku, Lenacapavir hutolewa kwa njia ya sindano mara mbili kwa mwaka, hali inayotarajiwa kuongeza ufuasi wa matibabu na kupunguza changamoto ya wagonjwa kusahau au kuchoka kutumia dawa.

“Ni mageuzi makubwa. Tunazungumzia mtu anayepata sindano moja na inamlinda au kumtibu kwa miezi sita. Hii inabadilisha kabisa mtazamo wa matibabu ya VVU,” alisema Msasi.

Dawa hiyo ya sindano inayozuia maambukizi ya VVU, yenye uwezo wa kutumika kama mbadala wa ARV kwa wenye maambukizi ya VVU, ilionesha ufanisi mkubwa katika tafiti za awali, ikiwemo jaribio lililofanyika nchini Uganda mwaka 2025.

Wataalamu wa afya wanaeleza ujio wake utaongeza utii wa matumizi ya kinga, hasa kwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi.

Kwa mujibu wa wataalamu, changamoto kubwa katika matumizi ya PrEP ya kila siku imekuwa ni ufuasi mdogo wa watumiaji, jambo linalopunguza ufanisi wake.

Hata hivyo, Lenacapavir inatarajiwa kupunguza changamoto hiyo kwa kuwa mtumiaji atahitaji kupata sindano hiyo mara mbili kwa mwaka, hivyo kuongeza uwezekano wa kufuata maelekezo ya kitaalamu.

Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (APHFTA), Dk Egina Makwabe, alisema ujio wa dawa ya Lenacapavir ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, lakini akasisitiza haja ya kupunguza gharama, ili iwafikie Watanzania wengi.

Pamoja na ubora wake, dawa hiyo bado ina changamoto ya gharama kubwa inayokadiriwa kufikia kati ya Sh40 milioni hadi Sh50 milioni kwa miezi sita kwa mtumiaji mmoja, hali inayoweza kuifanya ishindwe kufikiwa na wananchi wengi.

Mbali na maandalizi ya ndani, jitihada za kimataifa pia zinaendelea kuharakisha upatikanaji wa dawa hiyo katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.

Mataifa tajiri yanayounda kundi la G8 yamekuwa yakisisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya duniani, hususan katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kama VVU.

Kupitia ushirikiano wa kimataifa, G8 imekuwa ikichangia rasilimali fedha na kiufundi kupitia mifuko ya kimataifa kama Global Fund, ambayo ina mchango mkubwa katika kugharamia programu za VVU, kifua kikuu na malaria katika nchi nyingi za Afrika.

Kwa Tanzania, mchango wa G8 unatarajiwa kuendelea kuwa chachu muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa Lenacapavir. Hii ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa fedha za kununua dawa, kuimarisha mifumo ya ugavi pamoja na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia hiyo mpya.

Serikali kwa upande wake ilisema itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha huduma za kinga na tiba ya VVU zinaimarika na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa katika maeneo yenye maambukizi makubwa.

Kwa sasa macho yote yanaelekezwa kwenye maandalizi yanayoendelea, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na ubunifu huo wa kisayansi.