Kipi kilichojificha nyuma ya mbegu za maboga?
Baada ya mihogo mibichi, karanga mbichi na nazi kupata umaarufu wa kutosha jijini Dar es Salaam, sasa ni zamu ya mbegu za maboga.
Kinamama wanaouza vipande vya mihogo mibichi, karanga na nazi kwenye foleni za magari barabarani, pia wameongeza mbegu hizo katika bidhaa zao.
Hata hivyo, nilifanya utafiti mdogo wa kutembelea maduka ya nafaka nikajionea magunia ya mbegu za maboga yakipukutika kuliko mchele, maharagwe na unga.
Kwa nini mbegu za maboga zinauzwa kama karanga mbichi?
Mashime Mkude, mkazi wa Tabata Mawenzi, anayeuza nafaka anasema mbegu za maboga sasa ni sehemu ya bidhaa zinazouzwa kwa wingi.
“Ni zaidi ya mchele, maharagwe na karanga, kwa siku nauza gunia mbili au mbili na nusu. Zinanunuliwa sana kwa kweli,” anasema Mkude.
Pia, anasema wapo wanawake na wanaume ambao hununua nusu kilo hadi kilo kumi kwa ajili ya kuuza kidogo kidogo.
Mkude anataja sababu za kuuzwa kwa wingi mbegu za maboga kuwa ni lishe tu, lakini kwa anavyosikia kutoka kwa wanunuzi wake ni kuwa kuna uhusiano mkubwa wa nguvu za kiume na mbegu hizo.
“Nasikia kwa wale wanaotaka watoto wengi, basi wakila hizi kila siku, mke wake atapata mimba, wengine wanasema zinasaidia kuwapa hamu ya tendo la ndoa, sina uhakika lakini,” anasema Mkude.
Daktari Bingwa wa Mifumo ya Uzazi kwa wanaume Sydney Yongolo anasema ili kujua kama kweli mbegu za maboga zinasaidia katika nguvu za kiume unahitaji kujua kemikali zinazotengeneza karanga.
Anasema kwa mfano karanga ni kweli ina kemikali zinazosaidia kuchochea mwamko wa nguvu za kiume.
“Lakini mengine haya ni saikolojia tu, mtu akiambiwa hii ni ‘booster’ basi anakimbilia na huenda ikamsaidia kweli kwa sababu ipo kwenye hisia zake,” anasema Dk Yongolo.
Maboga yana mafuta ambayo huweza kuwa ni kichocheo cha nguvu za kiume.
“Mbegu mbegu nyingi za mimea, zina asidi ya linoleic (linoleic acid) asidi hii ndiyo inatengeneza arachidonic acid. Hizi ndizo zinatengeneza prostaglandins,” anasema Dk Yongolo.
Anasema prostaglandins zipo za aina nyingi, A, B, C, D na E, hivyo aina ya E ndiyo inayosaidia kunyanyua misuli ya uume na kuipa nguvu.
“Haya mafuta, yaani linoleic na arachidonic ni sawa na malighafi inayozalisha hizi homoni za prostaglandins. Hizi mbegu zina mafuta ya asili ambayo yanasaidia kuzalisha homoni muhimu kama prostaglandins. Kwa mfano karanga na korosho zina uhakika wa mafuta haya,” anasema Dk Yongolo.
Akitolea mfano anasema kuna tiba ya muda mrefu ya kumchoma mtu homoni za prostaglandis E1 kwa wanaume wenye matatizo ya nguvu za kiume.
“Unaweza kumchoma mgonjwa kwenye uume kwa sindano ya Prostaglandins E1 au kuweka kidonge chenye homoni hizo kwenye mirija ya uume,” unaeleza mtandao wa Afya wa WebMed.
Dk Yongolo anasema hata nazi zina mafuta yenye faida kwa nguvu za kiume lakini tatizo lake zina lehemu kwa wingi.
Jarida la Afya kwa Wanaume (Mens Journal) lililo chini ya American Media, limeeleza manufaa ya mbegu za maboga kwa wanaume.
Katika makala hiyo iliyochapishwa Desemba 2013, imeelezwa kuwa mbegu za maboga zina madini ya chuma kwa wingi hivyo kusaidia kuongeza hamu ya tendo la ndoa. Pia, mbegu hizo husaidia kuzalisha mbegu za kiume zenye afya na zenye nguvu.
“Madini ya chuma yanazalisha vichocheo aina ya ‘testosterone’ ambavyo ni vichocheo vikuu kwa wanaume,” limeeleza jarida hilo.
Jarida hilo limeeleza kwa kuwa mwili hauna mfumo wa utunzaji madini ya chuma hivyo ni vyema kula mara kwa mara mbegu hizo kwa ajili ya ubora wa mbegu za kiume.
Mfanyabiashara wa nafaka soko la Kariakoo, ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini anasema mbegu hizo zinauzwa kuliko hata mahindi ambayo ni chakula kikuu kwa Watanzania wengi.
Anasema amefanya biashara ya nafaka kwa zaidi ya miaka kumi lakini hakukuwa na wanunuzi wa mbegu za maboga lakini umaarufu wa mbegu hizo umeanza mwaka 2017/2018 na kadri siku zinavyokwenda ndivyo wateja wake wanavyoongezeka.
“Hapa nauza gunia tatu hadi nne kwa siku, wapo wanawake wanaokuja kununua pia na wao wanasema wametumwa na waume zao. Lakini wafanyabiashara wanaokwenda kuzifungasha pia ni wengi, hawa wananunua kilo tano hadi sita kwa mara moja,” anasema mfanyabiashara huyo.
Anasema mengi yanasemwa kuhusu matumizi ya mbegu hizo, lakini walio wengi wanadai zinaongeza ubora wa mbegu za kiume.
“Sijui ni kweli, lakini wanaume wanapenda kubwia tu, zikiwa mbichi hivi hivi wanasema zina protini ambayo inasaidia mambo fulani hivi,” anasema.
Mkazi wa Masasi, Mtwara Frederick Mitande anasema mbegu za maboga zinapata umaarufu kwa sababu tu zinatajwa kuongeza nguvu za kiume.
“Tatizo kubwa kwa sasa ni nguvu za kiume kutokana na mfumo wa maisha, sasa wanaume wanaposikia kuna chakula au dawa inasaidia kuongeza nguvu za kiume, inakuwa kimbilio la wanaume wote,” anasema Mitande.