Kwanini maziwa ya mama pekee muhimu kwa mtoto?

Muktasari:

Elimu ya umuhimu wa maziwa ya mama katika makuzi ya mtoto kuanzia siku ya kwanza hadi anapofikisha miezi sita, imekuwa ikitolewa na wataalamu wa fya.

Elimu ya umuhimu wa maziwa ya mama katika makuzi ya mtoto kuanzia siku ya kwanza hadi anapofikisha miezi sita, imekuwa ikitolewa na wataalamu wa fya.

Maziwa hayo ndiyo chakula cha mtoto kilicho salama, kisafi, kinajoto halisi, kinavirutubisho kamili na kinga zote za mwili.

Kwa kawaida maziwa ya mama hutengenezwa kipindi cha ujauzito, anapojifungua huanza kutoka kidogo na kuongezeka kadri siku zinavyozidi kwenda na mtoto anavyonyonya yakiwa na virutubisho kama sukari ya lactose, protini, mafuta, vitamini na madini huku maji yakiwa ni sehemu kubwa yananayokidhi kiu ya mtoto kwa miezi sita ya mwanzo.

Daktari wa wanawake katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza Dk Boniface Messanga anasema kuna hatua tatu za utokaji wa maziwa ya mama na zote zina umuhimu

Maziwa ya mwanzo ( Colostrum)

Daktari huyo anasema maziwa ya mwanza hutoka siku ya kwanza anapojifungua hadi siku ya nne yakiwa mazito na yenye rangi ya njano.

Anasema maziwa hayo ni rahisi kwa mtoto kumeng’enya, yana kingamwili nyingi , yana chembechembe nyeupe za damu nyingi, yana viini vinavyomkinga mtoto na maradh na vya ukuaji ambavyo husaidia utumbo wa mtoto mchanga kukua baada ya kuzaliwa.

Pia, anasema yana vitamini nyingi (hasa vitamini A) na protini.

Anasema maziwa hayo pia husaidia kusafisha tumbo la mtoto kwa kutoa choo cha kwanza cha rangi ya kijani (meconium) na kumkinga na tatizo la manjano.

Maziwa ya mpito (Transitional breast milk)

Dk Messanga anasema maziwa haya huanza kutoka siku ya nne baada ya yale ya mwanzo kutoka, hubadilika na hutoka kwa wingi.

“Yanapoanza kutoka yanakuwa mengi na yana protini, sukari, maji na virutubishi vingine kwa wingi,”anasema.

Hata hivyo, kauli ya Dk Messanga haitofautiani na ya Ofisa Lishe wa Mkoa wa Mwanza, Sophia Lugome anayesema kuwa kutokana na maziwa hayo kuwa na zaidi ya asilimia 80 ya maji, wanashauri wanawake wanaonyonyesha kutowapa watoto wachanga chakula chochote au maji mpaka watakapofikisha miezi sita.

“Ndiyo maana tunasema chini ya miezi sita mtoto asipewe hata maji ni maziwa ya mama pekee,” anasema Lugome.

Maziwa yaliyokomaa (mature breast milk)

Mhudumu wa afya ngazi ya jamii wa Kituo Isegeng’he katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza Timotheo John anasema maziwa hayo huanza kutoka baada ya wiki mbili za mama kuanza kunyonyesha. Anasema huwa maziwa mepesi (foremilk) na maji mengi, vitamini na protini.

John anasema baadaye hutoka maziwa mazito baada ya mtoto kuendelea kunyonya na huwa na kiwango kikubwa cha mafuta hivyo kumfanya mtoto kushiba na kukua vizuri.

Hata hivyo, Lugome ambaye ni ofisa lishe anasema virutubisho vilivyomo kwenye hatua zote za unyonyeshaji vinasaidia ukuaji wa mtoto kwa kuwa na afya bora, kukua vizuri na kuwa na akili.

Mtindo wa maisha huathiri unyonyeshaji

Licha ya wataalamu wa afya kusisitiza umuhimu wa kunyonyesha mtoto miezi sita ya mwanzo, bado kuna wanawake huogopa kunyonyesha wakihofia kupoteza mvuto wa maumbo yao.

Wanawake wengi hasa wa mjini wanaamini kunyonyesha kuna haribu maumbile yao ikiwamo matiti kulala na miili yao kuwa mikubwa (kunenepa) kupitiliza.

Mkazi wa Mwanza, Sarah Donard anasema baadhi ya wanawake wanaojifungua huacha kunyonyesha watoto wao kwa makusudi wakiogopa kunenepa na matiti yao kulala.

Anasema ili kulinda maumbile yao ulazimika kuwapa watoto maziwa ya ng’ombe, mbuzi au ya kopo kitu kinachohatarisha ukuaji wa mtoto. “Ni vizuri elimu ya faida ya maziwa ya mama kwa mtoto izidi kutolewa ili mama anayejifungua ajue hatari wanayoweza kuisababisha kwa watoto endapo wataacha kuwanyonyesha maziwa yao kwa makusudi,” anasema Sarah.

Imani potofu

Kitabu cha mafunzo ya lishe kwa ajili ya watoa huduma wa vituo vinavyotoa huduma za afya kilichoandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Lishe (Nutrition International) na Shirika la World Vision kinataja baadhi ya imani potofu zinazoaminika katika jamii.

Imani hizo ni maziwa ya mama kutotosha katika siku tatu za mwanzo baada ya kujifungua, hayafai kumpa mtoto hivyo inafaa kumpa mtoto asali, maji yenye sukari au maziwa mbadala katika kipindi hicho kitu ambacho si cha kweli. Imani zingine ni wakati mtoto anaponyonyeshwa anahitaji maji ya nyongeza hasa hali ya hewa inapokuwa ya joto, kama mama ana matiti madogo atatengeneza kiasi kidogo cha maziwa.

Pia, kama amejifungua kwa njia ya upasuaji hatakiwi kumnyonyesha mtoto na nyingine ni mtoto anayeharisha asinyonyeshwe maziwa ya mama vitu ambavyo sio kweli.

Kutokana na imani hizo, Grace Jonathan Mkazi wa Butimba jijini Mwanza anashauri wahudumu wa afya watoe elimu ya kutosha juu ya imani hizo kipindi chote cha mahudhurio ya kliniki wakati mama anapokuwa mjamzito na baada ya kujifungua.

Hata hivyo, Dk Messanga anasema mtoto anaweza kupata utapiamlo au ukuaji duni endapo atapatiwa vyakula mbadala badala ya maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo.

Anasema, mtoto anaweza kupata magonjwa ikiwamo maambukizi kwenye masikio, magonjwa ya ngozi, magonjwa ya mfumo wa njia ya chakula, kuhara, magonjwa ya njia ya mfumo wa hewa pamoja na kuathiri mahusiano ya mama na mtoto.

Madhara mengine mtoto anayoweza kupata ni kifo cha ghafla.

Dk Massenga anasema madhara mengine mama anaweza kupata ujauzito ndani ya muda mfupi baada ya kujifungua, kuchelewa kukatika kwa damu baada ya kujifungua, uwezekano wa kupata saratani ya mfuko wa mayai, saratani ya matiti, kuathiri upendo na ukaribu kati ya mama na mtoto.

Ushauri wa wataalamu

Bertha Yohana ambaye ni Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana anasema wanawake wanaojifungua wanyonyeshe watoto wao bila kuwapa kitu chochote hadi watakapofikisha miezi sita kwa ukuaji bora na salama ili kumuepusha na madhara anayoweza kupata mtoto au mama mwenyewe.

“Mtoto anapozaliwa anyonye maziwa ya mama pekee bila kupewa kitu chochote tangu kuzaliwa hadi miezi sita halafu anaanze kupewa chakula cha nyongeza,”anasema Bertha kauli inayoungwa mkono na Dk Messanga kuwa huwa wanatoa elimu ya unyonyeshaji kwa wazazi baada ya kujifungua.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (Unicef) linasema mwaka 2018 watoto wanne kati ya 10 ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo.

Shirika hilo linasema endapo kiwango cha unyonyeshaji kitaongezeka kitazuia vifo vya watoto chini ya miaka mitano 823,000 kila mwaka na vifo 20,000 vya kina mama vitokanavyo na saratani ya matiti kwa kila mwaka.