Prime
Maajabu ya tende, faida zake kufungulia Swaum
Tende ina faida gani mwilini?
Mwasora anasema hata tende iliyokaushwa vizuri ina ubora wa hali ya juu kilishe na pia ina kalori nyingi kuliko tende mbichi. Kalori iliyopo katika tende ni ile ya aina ya nishati lishe au wanga.
"Vilevile sukari nyingi kwenye tende, inatokana na virutubisho vya aina ya glukosi, fructose na sucrose ambayo huweza kuyeyushwa kwa urahisi mwilini," anasema Mwasora.
Faida nyingine tende ina madini na vitamini kwa wingi ambao husaidia kuulinda mwili dhidi ya maradhi.
Madini hayo ni pamoja na potasiamu, magnesiamu, shaba, manganase na madini ya chuma.
Madini mengine yanayopatikana kwa wingi kwenye tende ni pamoja na potasiamu ambayo husaidia kujenga na kuimarisha misuli ya moyo, pamoja na kudhibiti shinikizo la damu.
Pia tende zinaweza kuliwa kama chakula chenye sukari ya asili na kuwa mbadala wa sukari. Kalsiamu iliyoko kwenye tende ni muhimu kwenye mifupa na meno.
Anasema faida nyingine ya tende husaidia katika kupunguza tatizo la kuganda kwa damu, huku madini ya shaba ni muhimu katika uzalishaji wa seli nyekundu za damu. Vile vile magnesiam ni muhimu katika ukuaji na kuimarisha mifupa.
Anafafanua kuwa tende ni chanzo kizuri cha madini chuma mwilini na uwepo wa vitamin C kwenye tende husaidia ufyonzwaji wa madini chuma kwa wingi mwilini, ndiyo maana katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani tende kavu hutumika kama chakula cha mwanzo baada ya funga kwani, madini chuma hufyonzwa kwa urahisi kwenye tumbo tupu.
Pia madini chuma ni muhimu katika kusaidia kusafirishwa kwa hewa ya oksijeni mwilini.
Tafiti zinaonesha kuwa kuna vitamini nyingi kwenye tende, ikiwa ni pamoja na vitamini A, vitamini C (asidi ascorbic) na vitamini B (kwa mfano vitamini B1 (thiamine), vitamini B2 (riboflavin) na vitamini B3 (Niacin au asidi ya Nikotini). Vitamini B6 nayo inapatikana kwenye tende.
Mtaalamu wa lishe huyo anasema makapimlo au nyuzinyuzi (fibres) katika tende huwa haviwezi kuyeyushwa kwa urahisi mwilini, hivyo basi humfanya mtu kukaa muda mrefu pasipo kusikia njaa. Ndiyo maana katika kipindi hiki cha mfungo inashauriwa kutumia vyakula vyenye makapimlo au nyuzinyuzi kwa wingi ili kumfanya mtu asisikie njaa mapema.
"Makapimlo au nyuzinyuzi ni muhimu katika uyeyushwaji wa chakula na kusaidia katika umeng’enywaji na ufyonzwaji wa chakula tumboni, ikiwa ni pamoja na kuzuia mtu kupata choo kigumu,” anasema Mwasora na kuongeza;
"Mtu anapokuwa amefunga ana uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la kufunga choo. Hivyo basi, iwapo atatumia vyakula vyenye makapimlo au nyuzinyuzi huweza kuondoa hali hiyo" anasema.
Anabainisha kuwa makapimlo au nyuzinyuzi husaidia kuzuia hali ya kuvimbiwa na kuwa na uwezo pia wa kudhibiti sukari katika damu.
Makapimlo hayo pia huweza kupatikana kwa wingi kwenye matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa.
Anafafanua kuwa viondoa sumu vilivyoko katika tende vina uwezo wa kukinga seli za mwili zisiharibiwe na chembechembe haribifu ambazo huweza kusababisha saratani. Viini hivyo huungana na chembechembe hizo haribifu na kuzidhibiti ili zisisababishe madhara.
Kwenye tende kuna aina kadhaa za viondoa sumu ambavyo vinaweza kusaidia kuzuia au kupunguza magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama ya moyo, baadhi ya saratani, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu na ugonjwa wa sukari.
Anasema vitamin B6 iliyoko katika tende husaidia katika ufyonzwaji na utumikaji wa mafuta, kabohaidreti na protini mwilini.
Pia, husaidia katika utengenezwaji wa seli za kinga na kuweka sawa viwango vya madini ya sodiamu na fosforasi mwilini, husaidia kuimarisha mfumo wa fahamu na utengenezwaji wa seli nyekundu za damu.
Kwenye tende pia kuna protini ambayo inapatikana kwa kiwango kidogo, huboresha afya ya ubongo.
Tende zinaweza kusaidia kupunguza uvimbe kwenye ubongo ambayo ni muhimu kwa kuzuia ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
Faida nyingine ni kuboresha afya ya mifupa, madini ya fosforasi, potasiamu, kalsiamu na magnesiamu yana uwezo mkubwa wa kusaidia kuzuia matatizo ya mifupa kwa wenye ugonjwa wa mifupa.
Anabainisha kuwa kuna njia mbalimbali za kuongeza tende kwenye chakula. Njia mojawapo ni kulila kama lilivyo ili kupata utamu wa asili na hivyo wanashauriwa kula tende kwa kiasi.
Angalizo
Tende zina kiwango cha juu cha sukari, hivyo basi watu wenye ugonjwa wa kisukari na ambao wanajaribu kudhibiti sukari, wanapaswa kuzingatia kanuni za ulaji wa kila siku wa sukari wakati wa kula tende.
Ushahidi wa kitafiti unaonyesha kuwa wakati huu wa Ramadhani ni rahisi pia kudhibiti sukari kwa mgonjwa wa kisukari na pia ni salama kwa anayesumbuliwa na ugonjwa huu kufunga.
Ingawa tafiti nyingine zinaonyesha kuwa mgonjwa wa kisukari wa aina ya kwanza (type II diabetic), ambaye anatibiwa ugonjwa wa kisukari kwa kutumia sindano za insulini, pamoja na kurekebisha ulaji wake wa chakula, anakatazwa kufunga wakati huu wa Ramadhani.