Tamu, chungu wanawake wanaouza ‘busta’ barabarani

Muktasari:

  • Ili kujiingizia kipato, kinamama wamekuwa wakifanya kazi ya uchuuzi wa mihogo mibichi, karanga, tende, mchele na nazi maarufu busta

Dar es Salaam. Katikatika ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, wanaonekana wanawake wenye mabeseni vichwani wakizunguka huku na huko.

Hawa ni wajasiriamali, wachuuzi wa mihogo mibichi, karanga, tende, mchele na nazi maarufu busta.

Wachuuzi hawa wanatumia msongamano kwenye makutano ya barabara kuuza bidhaa zao, wateja wanaolengwa ni wanaume.

Inaaminika ulaji wa vitu hivyo ambavyo huchanganywa na kufungashwa pamoja unachangia kuongeza nguvu za kiume.

Hata hivyo, wataalamu wa lishe wanasema vyakula hivyo huongeza protini na nguvu mwilini.

Mtaalamu wa chakula na lishe Mkoa wa Katavi, Esta Sabato amesema vyakula hivyo vina mafuta, protini na wanga, hivyo huleta nguvu joto mwilini.

Amesema vyakula hivyo vimethibitika kitaalamu kuwa husaidia kuimarisha nguvu kutokana na madini yanayopatikana na hasa zinki.

“Kuna uvumi mwingi kuhusu faida za mihogo mibichi na nazi kavu (mbata) kwa wanaume. Wengi huhusisha na masuala ya tendo la ndoa, ukweli ni kwamba wanaozungumzia suala hilo wako sahihi ingawa wanaweza kuwa si wataalamu,” amesema.

“Atakayekula mchanganyiko wa vyakula hivyo hususani vikiwa vibichi anapata faida nyingi zaidi kwa kuwa na nguvu na vinakuwa havijafa,” amesema.

Amesema vyakula hivyo vina faida kwa mwanamke na mwanamume kwa kuwa huleta hamu, akieleza lishe nzuri husababisha homoni kufanyakazi vizuri.

Daktari katika Kituo cha Afya cha Tumaini, kilichopo Arusha, Samson Ndonde amesema mihogo mibichi na mbata (nazi)husaidia kuimarisha afya za walaji katika maeneo mengi ikiwamo via vya uzazi.

Amesema faida nyingine kiafya, hasa kwenye mbata ni kuepusha matatizo ya moyo yatokanayo na wingi wa lehemu kwa kuwa nazi aina hiyo huwa na kiwango kikubwa cha kiambata kiitwacho ‘lauric acid’ (jamii ya asidi mafuta).

“Kwa mfano, kalisiamu ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mifupa na meno kwa mwanadamu, hivyo mtu anayekula kwa wingi mihogo mibichi huimarisha meno na kuyafanya kuwa na nguvu,” amesema.


Kauli za wachuuzi  

Mariam Juma maarufu Mama Nuru, mkazi wa Buguruni ni miongoni mwa wanawake wengi wanaofanya biashara hiyo.

Amesema huu ni mwaka wake wa nne anafanya biashara ya bidhaa hizo. Anaeleza huamka saa 12 asubuhi kwenda sokoni kuchagua mihogo.

Amesema gharama za mihogo hutegemea wachuuzi sokoni, kuna wakati huuza mitatu kwa Sh2,000 au mmoja kwa Sh1,000  hivyo ukataji wa vipande hutegemea na bei ya manunuzi.

Mariam Juma akifanya biashara ya  mihogo na bidhaa nyingine katika Barabara ya Mandela, eneo la Buguruni Gana jijini Dar es Salaam.

Mchanganyiko wa bidhaa hizo hufungashwa kwa kipimo cha Sh200 na Sh500.

Mama Nuru amesema awali alikuwa akichanganya mihogo, karanga na mbata pekee, lakini watumiaji walitoa maoni wakimtaka aongeze karoti, mchele na tende.

“Maoni hayo niliyazingatia kwa sababu nahitaji kuuza zaidi, hivyo nachanganya kila kitu kwa pamoja,” amesema.

Amesema wateja wake wakuu ni madereva wa malori na daladala, huku wanaume wengine wachache hununua baadhi wanunuapo huona aibu.

Mama Nuru amesema imezoeleka ndani ya jamii kwamba wanunuzi ni wanaume, lakini wapo wanawake wanaonunua ingawa si wengi.


Changamoto

Amesema changamoto zilizopo ni wao kuonekana wanafanya biashara hiyo kwa ajili ya ‘kujiuza’ hivyo baadhi ya wateja huwauliza iwapo wapo tayari kutoka nao kimapenzi.

“Nakutana na wateja wa aina mbalimbali, mwingine anakuuliza unatuuzia huu mzigo au tunaondoka na wewe? Kuna wakati huwa nawajibu na mwingine nakaa kimya,” amesema.

Kupitia biashara hiyo anasema kuna faida lakini kinachohitajika ni ushapu na jitihada za kutafuta wateja.

Amesema wapo wanaotembea kidogo na kuchoka bila kujua kuwa mwendo mrefu unampatia wateja zaidi.

“Naweza kutembea umbali mrefu kutoka Buguruni hadi Tabata, inategemea foleni iliyopo. Siku nyingine natembea kutoka Buguruni hadi Vetenari, hiyo yote ni kuhakikisha nawafikia wateja kwa wingi,” amesema na kuongeza:

“Kwa kuwa natafuta wateja nakubaliana na kila ninaloambiwa sina la kuongeza wala kupunguza kwani najua ni changamoto za kazi.”

Changamoto nyingine amesema ni wateja kuikataa bidhaa hiyo wakieleza hawajui mazingira ya namna ilivyotengenezwa.

Si hivyo tu, amesema wapo wanaogongwa na pikipiki barabarani, huku waliosababisha ajali wakikimbia, hivyo hufanya kazi ya kuuguza majeraha wakati mwingine kwa muda mrefu hivyo kushindwa kujiingiia kipato.

“Mwezi uliopita kuna mwenzetu kagongwa na pikipiki dereva akakimbia, hatukupata msaada zaidi ya kumsaidia sisi na wafanyabiashara wengine bado hajurudi hadi barabarani,” amesema.

Anaeleza kuna wakati hukosa wateja, hivyo hurudi nyumbani pasipo kuwa na fedha. Amesema hilo hutokea kunapokuwa hakuna foleni barabarani.

Wateja wasio waaminifu amesema hukimbia na fedha baada ya magari kuruhusiwa kutembea.

“Huwezi kuacha beseni katikati ya barabara au pembezoni ili kukimbia kufuata fedha,” amesema.


Wasemavyo walaji

Hussein Mwinyi, dereva wa lori amesema hutumia bidhaa hiyo kuongeza protini mwilini, hupata hamasa ya kutafuna awapo katika safari ndefu.

“Napenda kutafuna, hivyo nisipokuwa na kitu mdomoni naona bora kutumia muhogo au karanga. Niliwahi kumsikia daktari akisimulia umuhimu wa karanga mbichi kuwa inaongeza protini na nguvu,” amesema Mwinyi.

Alfonce Selasini, dereva wa bodaboda amesema anapenda kununua kipande cha muhogo kuliko kifurushi (mchanganyiko) kwa kuwa hajui mazingira ya uandaaji wake.

“Bora nile muhogo kipande kuliko kifurushi ambacho sijaona alivyoandaa kwani nakuta ameweka kwenye kifuko akiwa amechanganya na karoti, sijui hata kama amesafisha lakini muhogo ananikatia naona,” amesema Selasini.

Amewata watu kuacha kukimbia na pesa za wajasiriamali kwa kuwa wanajitafutia riziki katika mazingira magumu.


Ukosefu wa nguvu

Imezoeleka katika jamii wanaume ndiyo hukosa nguvu ya kiume, lakini inaelezwa kwamba wanawake pia huathirika.

Mhadhiri wa Fiziolojia ya Homoni na Mazoezi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Fredrick Mashili amesema mabadiliko ya homoni wakati mwingine husababisha mwanamke kuwa mkavu, hivyo hawezi kufurahia tendo la ndoa.

“Sehemu kubwa ya wanawake imewekwa kwa ajili ya kufurahi hivyo kama ana tatizo hawezi kuonyesha kwani hashindwi kufanya tendo la ndoa tofauti na mwanamume,” amesema Dk Mashili.

Amesema ili kuwa katika hali ya kawaida anatakiwa kubadili mtindo wa maisha na endapo atakuwa na maradhi yasiyoambukiza sukari ikiwamo anatakiwa kuidhibiti ili kurudi katika hali yake ya kawaida.

Ulaji wa vyakula amesema unaweza kuchangia hali hiyo, hivyo inatakiwa kufuata ushauri wa lishe iliyokamili na kufanya mazoezi.

Dk Mashili amesema wanawake hupata hamu ya kufanya tendo la ndoa umri unavyozidi kusogea kutokana na mabadiliko ya homoni.

Mwanasaikolojia Ramadhani Massenga amesema msongo wa mawazo na kukosa muda mzuri wa kupumzika husababisha kutokuwa na hamu ya tendo la ndoa.

"Watu wengi wanazungumzia kuhusu homoni lakini ukifuatilia kwa undani watu hawana tatizo hilo ila wanakuwa hawapo sawa kiakili, kwani akili ya mtu inatakiwa kupeleka taarifa kamili pale anapofanyiwa kitendo hicho," amesema Massenga.

Amesema na matatizo hayo yamechangiwa kwa asilia kubwa kutokana na mtindo wa maisha wanayoishi ya kuhudumia familia na matokeo yake watu wanakuwa na mzigo mkubwa zaidi.

Amesema wapo ambao pia hushindwa kuyaacha matukio yaliyotokea maishani mwao, hivyo hujikuta akiyaweka moyoni na humuathiri.

"Tumeamua kutembea na vitu ambavyo vinatuvuruga kwenye kichwa unakuta bosi au wateja wamekukwaza basi hasira zinakwenda hadi nyumbani, hamu ya kufanya tendo la ndoa haiwezi kuwepo," amesema.