Magonjwa yasiyo ya kuambukiza sasa yanatishia uhai kuliko malaria, Ukimwi

Muktasari:

  • Kati ya vifo 10, saba vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, binadamu sasa anapaswa kuchukua hatua tano muhimu kuepuka janga hili ambalo sasa linaongezeka kwa kasi duniani kulingana na jinsi miaka inavyoongezeka.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni yale ambayo hayasambazwi kwa mtu mwingine kwa kuwa hayana vimelea vinavyohusiana na magonjwa hayo.  Hayo ni pamoja na magonjwa ya akili, moyo na mishipa ya damu, figo, saratani, kifua sugu, mapafu, pumu, kisukari na mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu.

Katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, ajali za barabarani na madhara yatokanayo na vilevi, yamewekwa kwenye orodha ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaoongoza kwa vifo duniani kwa sasa.

Utafiti mpya unasema kwa sasa asilimia 72.8 ya vifo duniani vinasababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na shinikizo la damu limekuwa kichocheo kikubwa. Utafiti huo uliofanywa na Nature mwaka 2007 umeripoti kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaua kwa kasi ikilinganishwa na yale ya kuambukiza. 

Utafiti unaonyesha kuwa ugonjwa wa moyo unaua kwa asilimia 30.2, saratani (15.7), kisukari (1.9), huku magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yakiua kwa asilimia 15.7 na ajali (9.3).

Hiyo ni kinyume na magonjwa yaliyo ya kuambukiza ambayo yanaua kwa wastani wa asilimia 30. Mfano Ukimwi kwa sasa unaua kwa asilimia 4.9, Kifua Kikuu – TB (2.4), malaria 1.5 na magonjwa mengine ya kuambukiza yakiua kwa asilimia 20.9.

Hali ikoje nchini Tanzania?

Kutokana na takwimu hizo za kidunia kwa hapa nchini katika utafiti uliofanywa mwaka 2012, unaonyesha kuwa asilimia 92.6 ya Watanzania ambao vipimo vyao vya shinikizo la damu vina walakini hawajaanza kutumia dawa, hali inayowafanya wawe katika hatari ya kupata magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Utafiti huo unatoa majibu ya ongezeko la wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza nchini yakiwamo kisukari, ugonjwa wa moyo, saratani na matatizo ya mapafu.

Kwa mujibu wa utafiti wa Tanzania Steps Survey uliofanyika nchini mwaka 2012, asilimia 26 pekee ya Watanzania ambao vipimo vyao vya shinikizo la damu vina walakini na tayari wameshaingia katika mfumo wa matibabu. Mwenyekiti wa Muungano wa Taasisi za Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA), Dk Tatizo Waane anasema utafiti huo ulilenga kuangalia ukubwa wa tatizo la magonjwa wasiyo ya kuambukiza nchini.

Anasema katika matokeo ya awali ya utafiti huo, yalionyesha watu wanaokabiliwa na tatizo la shinikizo la damu, imekuwa rahisi kwao kupata magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kama moyo, kisukari, saratani, mapafu na magonjwa mengineyo.

Hata hivyo, anasema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa na visababishi vitokanavyo na mtindo na maisha, ulaji wa vyakula ambavyo havijaandaliwa vizuri, utumiaji wa tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi.

“Kati ya watu wazima 5,680 wenye umri kati ya miaka 25-64 waliofanyiwa utafiti huu, asilimia 14.1 wanavuta sigara, asilimia tano pekee wanatumia matunda wakati wa mlo, asilimia 4.5 wanakula mboga za majani, 30 hawafanyi mazoezi, asilimia 26 wana uzito ulioongezeka, 8.7 wana uzito uliozidi na asilimia 30 wana tatizo la kuongezeka kwa lehemu kwenye damu,” anasema Dk Waane.

Akielezea athari za magonjwa yasiyoambukiza duniani Makamu Mwenyekiti wa TANCDA, Profesa Andrew Swai anasema, zaidi ya vifo 56 milioni vinavyotokea duniani kila mwaka husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza ukilinganisha na vifo milioni 38 vitokanavyo na magonjwa ya kuambukiza.

 

Nini kifanyike

Waane anasema Tanzania bado kuna mengi yanayotakiwa kufanyika ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza na athari zake.

Anasema Tanzania inatakiwa kupunguza kwa asilimia 25 magonjwa yasiyoambukiza kufikia mwaka 2018 kwa mujibu wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mwaka 2011 na mkutano wa pili mwaka 2014.

“Mpaka sasa bado hatujafika popote zaidi magonjwa yasiyoambukiza hayapewi kipaumbele na badala yake fedha kwa ajili ya kutibia magonjwa; zote zinakwenda kwenye magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi, malaria na TB, hali inayosababisha ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema Profesa Swai.

Mmoja wa wagonjwa wanaoishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza Ramadhani Mongi anasema, “Serikali inatakiwa kuweka sera na sheria za kuaangalia watu ambao tayari wameshaathirika na magonjwa haya na kuweka mikakati ya kulinda wale ambao bado hawajakumbwa na magonjwa haya, lakini pia kudhibiti matangazo na biashara chochezi za magonjwa haya.”

Anatoa mfano waganga wa dawa asili na mitishamba ambao wanajipambanua kama wenye dawa mbadala, wamekuwa wakiwadanganya watu wengi wana dawa za kutibu maradhi sugu jambo ambalo siyo kweli. Tatizo la magonjwa yasiyo ya kuambukiza linakua kwa kasi katika nchi zinazoendelea. Inakisiwa kuwa mwaka 2020 magonjwa haya yatasababisha asilimia 73 ya vifo vyote duniani na asilimia 60 ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.

 

Mambo ya kuzingatia

Moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa haya ni mabadiliko ya taratibu za kimaisha zinazohusisha matendo yanayoweza kusababisha ugonjwa.

Mojawapo ni kutofanya mazoezi, kukaa darasani, ofisini au kuangalia runinga kwa muda mrefu na kutoshiriki michezo.

Pia, ulaji usiofaa. Kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa, kula mafuta na chumvi zaidi ya mahitaji ya mwili. Sababu zingine ni kutokula mbogamboga na matunda kwa kiasi cha kutosha na kula nafaka zilizokobolewa.

Sababu nyingine zilizotajwa ni pamoja na matumizi ya pombe kupita kiasi, uvutaji wa tumbaku matumizi ya dawa za kulevya na msongo wa mawazo.

Mambo matano muhimu ya kuzingatia yanatajwa kuwa ni kuzingatia kanuni za ulaji, kufanya mazoezi au kazi zinazotoa jasho angalau kwa nusu saa kwa siku, kuepuka ulevi kupita kiasi, kudhibiti msongo wa mawazo na kupima afya mara kwa mara hasa kuchunguza uzito na dalili za magonjwa kama ya kisukari, shinikizo la damu, lehemu ili kuyadhibiti katika hatua za awali.

 

Dalili za magonjwa hayo

Kwa watu wazima, zifuatazo zinaweza kuwa dalili za mojawapo ya magonjwa hayo. Kupungua uzito na kuchoka bila sababu, kichwa kuuma mara kwa mara, kushikwa na kizunguzungu mara kwa mara, macho kutoona vizuri, kuona giza au kushindwa kusoma maandishi, meno kushikwa ganzi, kung’oka na au kutokwa na damu mara kwa mara kwenye fizi, miguu na mikono kuwa na maumivu kama ya kuwaka moto, maumivu ya kifua, kupumua kwa shida au kukosa pumzi unapotembea umbali mdogo au kujishughulisha na shughuli kidogo.

Kukosa pumzi usiku wakati umelala, moyo kwenda mbio, kubadilika tabia ya choo kama vile kufunga choo kusiko kwa kawaida, kukojoa mara kwa mara au mkojo kuchelewa kutoka, kutokwa damu sehemu yoyote kama vile puani, kwenye makohozi, kwenye choo kikubwa, kwenye mkojo na kadhalika.

Kwa upande wa mwanamke ni pale anapotoka damu nje ya mzunguko wa kawaida wa hedhi, wakati wa tendo la ndoa au baada ya kufunga hedhi; kutokwa na majimaji au ute ukeni, kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa na kuibuka kwa vidonda mwilini.

Dalili nyingine ni kujisikia mpweke, mwoga, wasiwasi na hofu bila sababu yoyote, kuwa na hasira za mara kwa mara, kushindwa kutimiza wajibu, unywaji wa pombe kupita kiasi, kuvuta sigara kwa wingi na kuona vitu ambavyo watu wengine hawavioni.

 

Wiki ijayo usikose mwendelezo wa tafiti zilizobaini kuwa karibu binadamu wote wanaugua magonjwa matano.

Maoni au maswali tuma [email protected] au 0713247889