Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaabu ya makundi ya damu na tabia ya binadamu

Muktasari:

  • Kwa wananchi wa Japani haikushangaza kusema hivyo, kwa sababu hata ukiwa mgeni nchini humo lakini ukajipambanua kitabia, Mjapani atakuambia sababu ya wewe kuwa hivyo kunasababishwa na kundi lako la damu.

Wakati wa Waziri Mkuu wa Japani, Junichiro Koizumi akijiuzulu mwaka 2008, alisema moja ya sababu ya kushinikizwa kujiuzulu kulitokana na yeye kuwa na damu kundi B.

Kwa wananchi wa Japani haikushangaza kusema hivyo, kwa sababu hata ukiwa mgeni nchini humo lakini ukajipambanua kitabia, Mjapani atakuambia sababu ya wewe kuwa hivyo kunasababishwa na kundi lako la damu.

Kwanini huamini hivyo?

Wajapani siku zote huamini kuwa kiongozi bora ni yule aliye damu ya kundi 0, kwa madai kuwa mtu mwenye damu hiyo anakuwa na uwezo mkubwa katika kuongoza, wana msimamo, wanajali, wabunifu na wana bidii kusaka mafanikio.

Wana imani kuwa makundi ya damu yanauhusiano wa moja kwa moja na kujitokeza kwa tabia ya mtu ikiwamo tabia mbaya na nzuri, katika kupata mafanikio kiuchumi, kiutawala na kiuongozi.

Profesa Masahiko Nomi ni mtu maarufu nchini Japani kutokana na kuandika vitabu vinavyoelezea makundi ya damu na tabia zake. Kitabu chake cha mwaka 1970 kilipata umaarufu na kuaminiwa na wajapani.

Nadharia ya kuamini makundi ya damu na tabia ilianza lini?

Nadharia za tabia za wanadamu na makundi hayo ya damu hazikuanzia kwa Profesa Nomi, bali tangu enzi za mafilosofa wakiwamo Aristotle na Hippocrates ambao maandiko yao yaliwapa shauku watafiti wengine.

Wajapani wanaamini kuwa makundi hayo ya damu ndiyo pia yanatoa mustakabali wa mwanadamu kuwa na tabia njema na dhaifu.

Wanaamini kundi la damu ‘A’ wao huwa ni wasikivu, wenye bidii, mfano wa kuigwa, wakomaliaji wa mambo, wachambuzi, watu wakujitoa, waaminifu na wenye hisia kali.

Vile vile wakizungumza jambo huwa wanamaanisha, wanasubira, wawajibikaji, watu makini, waangalifu na wapole.

Udhaifu wao mkubwa ni kukosa utulivu, mchaguzi, bidii iliyopitiliza, mkaidi, wana wazimu, wakujikweza na kujiona.

Wenye kundi la damu ‘B’ tabia zao nzuri ni pamoja na kuwa wenye shauku, imara, wabunifu, wapenda wanyama, mrahisi kubadilika kuendana na hali, wachangamfu na wanajua urafiki.

Vile vile wana matumaini ya kuweza jambo, wanajisimamia, wanajitegemea na hawahitaji ushirika kufanya kitu na yeyote.

Udhaifu wao mkubwa ni pamoja na kutowajibika, wasahaulifu, wabinafsi, wavivu, hawana subira, vikigeugeu, mtu wa kivyake vyake, huwa wakatili na wenye hasira kali.

Tabia ya watu wenye kundi la damu la AB

Kwa mujibu wa vitabu vya Wajapani watu wenye kundi la damu la AB wanatabia mchanganyiko na hawatabiriki, tabia zao nzuri na ni wabunifu, wanaakili, watulivu na hufanya mambo kwa vitendo.

Pia wana tabi ya ucheshi, wana mantiki na uwezo wa kukabili mambo na kubadilika kuendana na hali.

Udhaifu wao mkubwa wa kitabia ni pamoja na kuwa wakosoaji wasio na mipaka, wasiosamehe, hawatabiriki, wabishi sana, hawana uamuzi, sio wakali, hawana msimamo, hupinga hata vitu vidogo, hisia za kuyumba na siyo waamininifu.

Kwa upande wa kundi la damu O ambalo ndilo wajapani wanaliamini kuwa na tabia za kuvutia zinazowafanya kuwa na mafanikio katika uongozi na maendeleo. Watu hao huitwa ‘cheerleaders’ kwa lugha ya kitaalamu.

Pia huaminika kuwa ni mahodari na mashujaa katika mambo mazito na wana uwezo mkubwa wa kujieleza na kuhamasisha. Huwa na kiu kubwa ya kuwawezesha wengine, wanafikra pana na wanajali sana marafiki.

Tabia nzuri ni pamoja na kujiamini, wenye malengo, jasiri, wana misimamo, wadadisi, wana bidii, wapambanaji kimaisha, waangavu, wenye maono, wana uamuzi mgumu na waelewa.

Vile vile ni watu wakujitolea, wanakubalika kwa mazuri, washindani, shupavu na huwa waasilia.

Lakini wataalamu wanasema watu hawa wana udhaifu wao ambao ni pamoja na wa kitabia. Pia, hawatabiriki, wabinafsi, watulivu, wakali, wanahasira, wajeuri, wepesi kuvurugwa, wapuuziaji wa mambo, wababe na hawapendi kuingiliwa hata inapobidi.

Tabia hizi ndizo zinawafanya Wajapani kufikia mahali hulazimisha upimaji wa makundi ya damu kwa watoto wao, wanajeshi, viongozi, wageni wanaoajiriwa na wafanyabiashara.

Imani yao imesababisha hali ya kunyanyapaliwa kwa watu wenye makundi ya damu ambayo wanasemakana yana tabia hasi zisizofaa katika jamii yao.

Wanasayansi wanavyolizungumzia hilo

Jumuia ya wanasayansi wanapinga machapisho ya Kijapani ya nadharia ya makundi ya damu na tabia za wanadamu, wakieleza ni dhana ya ovyo na ni imani potofu.

Wanasema hivyo kwa madai kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha au majaribio yenye kuleta majibu chanya juu ya hilo.

Tafiti hizo za Wajapani pia zinaelezwa kukwama kwa upande wa takwimu kwani zimeshindwa kuleta matokeo chanya katika idadi ya makundi makubwa ya watu.

Kisayansi, utofauti wa makundi ya damu upo katika uwapo au kutokuwapo kwa aina fulani ya chembe za protini za antigeni na antibody.

Chembe hizo ndizo zinawezesha mifumo ya uanishaji wa makundi ya damu.

Kila mtu ana aina tofauti ya chembe hizo za protini na namna zilivyounganika.

Kundi la damu alilonalo binadamu inaelezwa kuwa hutegemeana na alichorithi kutoka kwa wazazi wake wote wawili.

Taarifa za aina ya chembe hubebwa katika chembe za urithi (vinasabaa).

Taaluma ya uhandisi wa chembe za urithi unaeleza chembe hizo ndizo zimebeba maelekezo ya vitu vinavyounda mwili.

Chembe hizo pia ndizo zinatoa maelekezo kwa mwili kutengeneza aina ya vitendea kazi vya mfumo wa kinga kuweza kukabiliana na maradhi.

Ndiyo maana zipo tafiti zilizofanyika na kuonyesha kuwa kuna baadhi ya makundi ya damu yana faida zake na hasara katika upambanaji na vimelea vya maradhi na kuyadhibiti.

Katika makundi hayo, wanasayansi wameanisha maradhi mbalimbali na makundi ya damu yakiwamo uwezo wa kinga ya mwili kukabiliana na maradhi.

Pia, yapo makundi yanayoonyesha hatari ya kuugua maradhi kama ya saratani.

Kwa kawaida, mama huchangia nusu na baba huchangia nusu ya malighafi za mtoto za kiurithi.

Kuna mifumo karibu 20 ya kijenetiki ambayo ndiyo inatoa mwelekeo wa uanishaji wa makundi ya damu mwilini.

Mfumo wa ‘ABO’ na ‘RH’ ndiyo unaotumika kuanisha kundi la damu alilonalo binadamu.

Mwanasayansi Karl Landsteiner ndiye alihusika na kugundua mfumo huu wa uanishaji wa makundi ya damu ABO (mwaka 1901) na RH (mwaka 1937) ambao ndiyo unatumika hadi sasa.

Ingawa katika makundi ya damu wapo ambao wana chembe za urithi katika nyuso za seli zao ambazo zinahusishwa katika kuchochea utengenezwaji wa vichochezi vinavyotiririshwa wakati wa shinikizo la kiakili au lakimwili, vichochezi hivyo huitwa stress hormons.

Wanasayansi wanakubaliana kuwa ni kweli kuna makundi ya damu yenye uwezo wakipekee katika kukabilina na maradhi, lakini bado wanapinga kukubaliana na Wajapani na nadharia yao.

Hivyo basi katika hili bado tafiti nyingi zinahitajika kufanyika maeneo mbalimbali duniani na katika tabaka tofauti katika makundi makubwa ili kusaka ukweli wa nadharia hiyo.