Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitindo hii ya maisha chachu ya afya ya ubongo, mwili

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa ubongo wa binadamu una uwezo wa kujifunza na kubadilika katika hatua zote za maisha. 

Dar es Salaam. Wazo kwamba uwezo wa akili hupungua kadri mtu anavyozeeka limekuwa likikubalika kwa muda mrefu katika jamii. 

Watu wengi huchukulia kusahau mambo madogo kama sehemu ya kawaida ya uzee. 

Hata hivyo, kazi za kitafiti za kisayansi zinaonyesha kuwa hali hiyo si lazima iwe hivyo, kwani kuna mambo ambayo mtu anaweza kufanya ili kulinda afya ya ubongo na kuendelea kuishi maisha yenye ubora hata katika umri mkubwa.

Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa ubongo wa binadamu una uwezo wa kujifunza na kubadilika katika hatua zote za maisha. 

Ingawa kasi ya kujifunza hupungua kadri umri unavyoongezeka, bado ubongo unaweza kuendelea kuunda miunganisho mipya. 

Kazi za kitafiti zinaonyesha pia kuwa kuna vipindi maalum katika maisha ambapo ubongo hupitia mabadiliko makubwa, jambo linaloonyesha kuwa maendeleo ya akili hayaishii utotoni pekee.

Moja ya njia muhimu za kulinda afya ya ubongo ni kujifunza mambo mapya mara kwa mara. 

Hii inaweza kuwa kujifunza lugha mpya, kuanza shughuli mpya kama bustani, au hata kushiriki katika kazi zinazohitaji kufikiri kwa kina. 

Shughuli hizi huchochea ubongo kufanya kazi zaidi na kusaidia kudumisha uwezo wa kufikiri. 

Aidha, utafiti umeonyesha kuwa kujifunza lugha mpya kunaweza kuchelewesha dalili za magonjwa ya kupoteza kumbukumbu kwa muda mrefu zaidi.


Zingatia lishe

Lishe bora pia ina nafasi kubwa katika kuboresha afya ya mwili na ubongo. Wataalamu wanashauri kula vyakula vyenye rangi mbalimbali, hasa matunda na mboga, ili kupata virutubisho muhimu.

 Hata kuongeza kiasi kidogo cha matunda au mboga katika mlo wa kila siku, kunaweza kuleta mabadiliko chanya katika afya. Vilevile, ulaji wa vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi husaidia kuboresha utendaji wa ubongo kwa muda mfupi.

Kwa upande mwingine, ni muhimu kuepuka ulaji wa mafuta yasiyo na afya, hasa yale yanayotokana na vyakula vilivyosindikwa.

 Mafuta hayo yanaweza kusababisha matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo na yale yanayoathiri ubongo. 

Badala yake, wataalamu wanashauri kutumia mafuta yenye afya kama yale yanayopatikana kwenye samaki na karanga.

 Pia, virutubisho kama 'choline' vinavyopatikana kwenye mayai vina mchango mkubwa katika kuboresha kumbukumbu na afya ya ubongo.

Mazoezi ya mwili ni nguzo nyingine muhimu katika kulinda afya ya ubongo na mwili kwa ujumla. Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kuongeza mzunguko wa damu mwilini, jambo linalochangia ukuaji wa seli za ubongo na kuboresha hali ya hisia.

 Hata mazoezi madogo ya kila siku yanaweza kuwa na faida kubwa kwa muda mrefu.

Uhusiano wa kijamii nao una mchango mkubwa katika ustawi wa binadamu. Kukaa karibu na marafiki, familia na jamii husaidia kupunguza upweke na msongo wa mawazo. 

Tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye uhusiano mzuri ya kijamii wana uwezekano mkubwa wa kuishi maisha marefu na yenye afya bora ya akili.

Wataalamu wanasisitiza pia umuhimu wa kufanya mabadiliko madogo lakini endelevu katika maisha ya kila siku. Badala ya kubadilisha kila kitu kwa ghafla, ni vyema kuanza na hatua ndogo kama kuongeza muda wa mazoezi, kuboresha lishe au kujifunza jambo jipya. Hatua hizi ndogo, zikifanywa kwa uthabiti, zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa muda mrefu.

Kwa ujumla, kuishi maisha marefu yenye afya njema kunategemea uamuzi wa kila siku anaofanya mtu. 


Makala hii iliyoboreshwa imetafsiriwa kutoka mtandao wa BBC.