Mtoto wa miaka mitatu afanyiwa upasuaji wa ubongo kwa saa 10, KCMC
Jopo la madaktari bingwa kutoka Marekani likishirikiana na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), wakifanya upasuaji kuondoa uvimbe kwenye ubongo wa mtoto aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Upasuaji huo ulifanywa kwa saa 10 chini ya jopo la madaktari bingwa na bobezi wa upasuaji kutoka Marekani kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka hospitali ya KCMC ambao waliondoa uvimbe mkubwa uliokuwa kwenye ubongo wa mtoto huyo.
Moshi. Jopo la madaktari bingwa kutoka Marekani, kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), wamefanikiwa kufanya upasuaji uliotumia saa 10 kuondoa uvimbe kwenye ubongo wa mtoto wa miaka mitatu, ambaye alikuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu.
Madaktari hao ambao wameweka kambi kwa siku tano katika hospitali hiyo, tayari wameshafanya upasuaji kwa wagonjwa saba kati ya 10 waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la uvimbe kwenye ubongo na mishipa ya fahamu.
Akizungumzia upasuaji huo uliodumu kwa saa 10, ambao umefanyika Juni 26, mwaka huu, daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo ambaye ni Rais wa Taasisi ya Barrow Neurological Institute Phoenix nchini Marekani, Profesa Michael Lawton amesema upasuaji huo ulihitaji umakini mkubwa kutokana na ukubwa wa uvimbe huo na sehemu uliokuwa kwenye ubongo.
"Tupo hapa KCMC kwa wiki moja na mpaka sasa tumefanya upasuaji wa ubongo kwa watu saba ambao wengi wao ni watoto, jana tumefanikiwa kuondoa uvimbe mkubwa uliokuwa kwenye ubongo wa mtoto wa miaka mitatu, ambaye kwa sasa anaendelea vizuri," amasema Profesa Lawton.
Katika upasuaji huo amesemal "Ni mara yangu ya kwanza kumfanyia mtu upasuaji kutumia saa 10 na ni kwa sababu uvimbe ulikuwa mkubwa sana na ulikuwa umeathiri sehemu kubwa ya ubongo wake," amesema Profesa Lawton.
Aidha, Profesa Lawton amesema teknolojia ya kisasa iliyotumika na uzoefu wa timu hiyo ya madaktari imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha upasuaji huo wa aina yake ambapo lengo ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hiyo kwa urahisi.
"Upasuaji huu si tu umeokoa maisha ya mtoto huyu, bali pia ni mfano wa mafanikio yanayopatikana kupitia ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya,"amesema Profesa Lawton.
Akizungumza daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, Hospitali ya KCMC, Dk Happiness Rabiel, amesema wiki hii wameandaa wagonjwa maalumu kwa ajili ya upasuaji ambao unahitaji taaluma ya hali ya juu zaidi ikiwemo upasuaji wa mtoto wa miaka mitatu ambaye upasuaji wake ulichukua muda mrefu.
"Kwa wiki hii kuna wagonjwa maalumu tuliwaanda ambao wapo 10 kwa ajili ya upasuaji ambao unahitaji taaluma ya hali ya juu zaidi kuliko operesheni ambazo tumekuwa tukifanya hapa KCMC, na jana tumefanya upasuaji mrefu sana ambao upasuaji mmoja ulichukua zaidi ya saa 9," amesema Dk Rabiel.
Amasema mpaka kufikia jana, wamefanikiwa kufanya upasuaji wa ubongo kwa wagonjwa Saba ambao kwa sasa afya zao zinaendelea vizuri.
Dk Rabiel amesema, toka kuanzishwa kwa huduma hiyo ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu hospitalini mwaka 2022, kila mwaka huwafanyia wagonjwa kati ya 400 hadi 600.
"Kambi hii maalumu ambayo ndio tumeanza kufanya nayo kwa mara ya kwanza toka mashirikiano haya yameanza na Taasisi hii ya Marekani hapa KCMC tumepanga kufanyia upasuaji wagonjwa 10 ndani ya siku tano, ambapo kwa siku moja tunafanya upasuaji wagonjwa wawili," amasema Dk Rabiel.
Pamoja na mambo mengine amesema, uvimbe kwenye ubongo unasababishwa na sababu mbalimbali huku dalilii kubwa zikiwa ni kupoteza uoni, kuumwa kichwa mfululizo kwa muda mrefu, degedege ambayo huanza ukubwani na nyingine kupooza upande mmoja wa mwili.
Naye, mtaalamu wa masuala ya upasuaji wa ubongo kutoka Taasisi ya Barrow Neurological Institute, Marekani, Dk Kerry Vaughan amesema suala la utoaji wa uvimbe kwenye ubongo siyo jambo jepesi linahitaji umakini mkubwa na kwamba wanajivunia kuondoa uvimbe kwenye ubongo wa mtoto wa miaka mitatu ambaye ameteseka nao kwa muda mrefu.
"Tunaishukuru hospitali ya KCMC na Watanzania kwa kuunga mkono kazi yetu kwa pamoja, tunafanya upasuaji kila siku, hii ni kazi ngumu kidogo lakini tunaifanya kwa ubora na kwa umakini mkubwa, tunashukuru Mungu mtoto wetu anaendelea vizuri sana," amesema Dk Vaughan.