Mwongozo ulaji sahihi kwa wanaofunga

Dar es Salaam. Wakati Waislamu wameanza kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni muhimu wakazingatia mpangilio sahihi wa makundi ya vyakula wakati wa kufungua (kufuturu), ili waendelee kuimarisha afya zao.

 Mara nyingi vyakula vinavyoliwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi hiki ni vya aina ya mizizi kama mihogo, magimbi na viazi vitamu ambavyo vyote vipo katika kundi mola la vyakula, jambo ambalo halishauriwi kiafya.

Fatma Mwasora, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC anasema mfungaji anapaswa kupata mlo wenye mchanganyiko wa virutubishi vyote muhimu, ikiwa ni pamoja na uwiano sahihi na sawa kulingana na mahitaji ya mwili.

Anasema mtu anapokula mlo kamili kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili, hupata virutubisho vyote muhimu.

“Futari na daku ni muhimu iwe ni milo kamili, hasa kwa mfungaji kwa sababu husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini,” anasema.

Mwasoro anasema si sahihi kula kundi moja la vyakula vya nafaka na mizizi, kwani itachangia mlaji kupata virutubishi ambavyo ni vya aina moja.

“Vyakula hivi mara nyingi hutupatia virutubishi vya aina ya nishati lishe au wanga ambayo huongeza nguvu na joto mwilini. Hali hii huweza kuwasababishia ukosefu wa baadhi ya virutubishi vingine kutoka katika aina nyingine ya makundi ya vyakula,” anasema.

Athari nyingine inayoweza kujitokeza iwapo vyakula vya asili ya nyama na jamii ya mikunde havitajumuishwa katika milo ya futari na daku ya kila siku, huweza kusababisha upungufu wa virutubishi vya protini katika mwili ambavyo husaidia kujenga mwili na kuimarisha kinga ya mwili.

Mfano wa vyakula hivyo ni aina zote za nyama, samaki, wadudu wanaoliwa kama senene, vyakula jamii ya kunde kama maharage, choroko na vinginevyo.

Akizungumzia jinsi ya kuondoa hali ya uchovu mwilini ama kuhisi kizunguzungu kwa mfungaji, Ofisa lishe huyo anasema inaweza kuondolewa kwa mhusika kula vyakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote matano ya vyakula.

“Ulaji wa vyakula vya aina ya nyama na jamii ya mikunde ni muhimu ili kupata protini ya kutosha ambayo husaidia kujenga mwili na kuimarisha kinga ya mwili. Pia ulaji wa mbogamboga na matunda kwa wingi husaidia kupata vitamini na madini ambayo huimarisha kinga ya mwili na kuongeza damu,” anabainisha.

Mtaalamu huyo wa lishe anasema endapo vyakula hivyo havitajumuishwa kwenye milo ya futari na daku ya kila siku huweza kusababisha upungufu wa kinga ya mwili na kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa, mfano maambukizi katika mfumo wa upumuaji au Uviko-19.


Tahadhari matumizi ya sukari, mafuta mengi

Mwasora anaonya matumizi makubwa ya vyakula vya mafuta mengi na sukari akisema ni hatari kwa afya.

“Vyakula vya mafuta na sukari vikiliwa kwa wingi katika milo ya kila siku vinaweza kusababisa uzito mkubwa au viribatumbo.

“Uchaguzi wa vyakula usiozingatia mpangilio sahihi katika milo ya familia huweza kusababisha uzito mkubwa ama viribatumbo na pia kusababisha magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu, kisukari, pumu na baadhi ya saratani endapo vitatumika mara kwa mara na kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Mwasora anashauri jamii pia kuepuka matumizi ya chumvi nyingi kwenye chakula, kutumia kidogo.

Anasema tafiti mbalimbali zinaonyesha kufunga mwezi mzima kuna faida kubwa kiafya, hata kwa mtu anayezingatia ulaji sahihi wa vyakula pamoja na kula kwa kiasi.

Anasema kufunga husaidia watu wenye magonjwa ya moyo na wale wenye uzito mkubwa na viribatumbo kupungua uzito kwa haraka.

Hivyo, anaonya ulaji wa kupita kiasi katika kipindi hiki, ili faida za kufunga zionekane kwa mhusika.


Anza na vyakula hivi

Walbert Mgeni, Ofisa Mtafiti Mafunzo na Elimu ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) anasema vyakula vinavyofaa kwa mtu aliyefunga ni kuanza kula vyakula vyenye majimaji kama supu kwa sababu husaidia kufanya umeng’enyaji mzuri.

“Huyu mtu ameshinda na njaa siku nzima, hivyo ili kuamsha vimeng’enyo vinavyosagwa na chakula ni vizuri akaanza na vyakula laini, supu kwa sababu inarudisha maji mwilini, pia husaidia vimeng’enyo vilivyokaa muda mrefu bila kufanya kazi, kuanza kufanya kazi,” anasema Mgeni.

Anasema pia ulaji tende kama kianzio ni vizuri kwa kuwa inasaidia kwa kuwa mfungaji ameshinda njaa na nishati au nguvu imepungua, hivyo tende husaidia apate nishati kwa wingi.