Nafasi ya lishe bora katika kuzuia maradhi yasiyoambukiza

Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni dunia imeshuhudia kuwapo kwa kipindi cha mpito kuhusiana na ulaji. Chakula kimekuwa kikipitia katika mlolongo mrefu hali ambayo imefanya pia kalori zinazopatikana kwenye nyama, sukari na mafuta kuongezeka kwa kiwango kikubwa na kufanya virutubisho vinavyopatikana kupungua.

Madhara yake ni kwamba mabadiliko hayo yamesababisha kuwapo kwa ongezeko la maradhi yasiyoambukiza(NCDs).

Tafiti zinaonyesha kuwapo kwa uhusiano wa karibu kati ya chakula, virutubisho na lishe. Inaelezwa kuwa ni mambo yanayochangia kwa kiwango kikubwa maradhi yasiyoambukiza na hasa kukosekana kwa virutubisho. Hata hivyo, wataalamu wa lishe wanasema ulaji mzuri wa chakula kunaondoa uwezekano wa kuyapata maradhi hayo.

Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoendelea, imetumbukia kwenye hali hiyo ya kutozingatia ulaji bora na hivyo kuwafanya watu wake kuwa hatarini kupata unene wa kupindukia na vitambi, sababu inayowafanya wengi waugue maradhi yasiyoambukiza kama ya kisukari, moyo na saratani. Kulingana na Sensa ya Idadi ya Watu na Afya(TDSH) iliyofanywa 2015-2016, inaonyesha asilimia 9 ya watu wazima wanakabiliwa na kisukari huku asilimia 26 wakiwa na vitambi.

Kulingana na mtaalamu wa vyakula na lishe kutoka muungano wa masuala ya lishe(Panita), Deborah Esau, mfumo wa ulaji nchini ni changamoto kubwa na ndiyo inayochangia uwapo wa maradhi yasiyoambukiza. Anasema wananchi wengi bado wana dhana potofu wakiamini kuwa ulaji mzuri ni ile hali ya kula vyakula vingi visivyo na virutubisho (junkfood). “Kama hukudhibiti namna ya ulaji wako, uko hatarini kupata maradhi haya sugu. Watu wengi wanaoishi mijini wanatumbukia kwenye mtego huu wa ulaji ovyo usiozingatia afya. Lakini hali ni tofauti unavyokwenda maeneo ya vijijini ambako uwapo wa maradhi haya ni mdogo na sababu kubwa ni kwamba hawali kianasa – pengine kwa vile hawana vyakula vingi au kile chakula walichonacho wanakipika katika hali ya kawaida tu,” anasema Esau.

Maeneo mengi ya mijini ambako wengi wamekuwa na shida ya kukosa lishe bora ni kutokana na mazingira ya kazi zao zinazowafanya wakose muda wa kutosha kuandaa vyakula vyao. Hali hii imewafanya wakose virutubisho vidogovidogo tunavyovipata kutoka kwenye matunda na mboga za majani, anaeleza Esau. “Vyakula vinavyopikwa mitaani hatujui ni kiasi gani cha chumvi kimetumika au chumvi iliyotumika ni ile inayopendekezwa au aina ya mafuta yaliyotumika ni yale yanayofaa? lakini unaamua kula tu kwa sababu una njaa. Vyakula vingi havina kalori na muda unavyokwenda na mtu anakuwa hana mazoezi pamoja na mfumo wa kukaa sana kwenye viti, ni rahisi kujikuta akipata kitambi na hivyo kutumbukia katika hatari ya kuugua maradhi yasiyoambukiza,” anasema.

Ulaji wa vyakula sahihi

Esau anasema kuendelea kuwa na afya nzuri kunahitaji kujitoa na kumaanisha, ili kuboresha mfumo wa maisha, hatua ambayo ndiyo njia sahihi ya kujiepusha kukumbwa na maradhi yasiyoambukiza.

Anasema mtu anapaswa kuzingatia kutunza afya yake na kutambua kuwa kuharibu afya kunachangiwa pia na mfumo duni wa kimaisha.

“Jambo la kwanza, tunahitaji kubadilika katika mfumo wetu wa ulaji na kuanza kula vizuri ikiwamo kuondokana na tabia ya kupenda kula chakula cha aina moja kama wali, ugali na vyakula vya aina mbalimbali. Pia, tunapaswa kuangalia namna tunavyoandaa vyakula vyetu kwa kuhakikisha hatuvipiki sana, kuepuka kutumia mafuta mengi ya kula, sukari na chumvi pia. Kila kitu kitumike kwa kiasi,” anashauri Esau.

Anasema wale wanaofanya kazi na kujikuta wakila vyakula vingi vya kwenye vioski, wanaweza kuepukana na hali hii kwa kujiandalia vyakula vyao wenyewe vya mchana.

“Tunapaswa kujitahidi kadri tuwezavyo kubeba chakula kutoka nyumbani hasa kama pale mazingira ya ofisi zetu hayatuwezeshi kununua vyakula ambavyo vimeandaliwa vyema. Pia, lazima tujifunze kupata kifungua kinywa cha asubuhi kama vile cha kifalme na kula kiasi, lakini kwa afya kama vile wafungwa nyakati za jioni.” Esau anashauri watu wajenge tabia ya kutembea angalau kwa dakika 20 hasa kwa wale wanaofanya kazi, ni jambo jema linaloweza kusaidia kupunguza hatari ya kukumbwa na maradhi hayo.

“Haiwezekani ukawa umekaa siku nzima ofisini, mazoezi yanasaidia kuwa na mzunguko mzuri wa damu na kuufanya mwili kuwa imara na tunapaswa kujifunza kutumia kila kitu kwa kiasi ikiwamo pombe tunazokunywa,” anasema mtaalamu huyo.

Akitambua kuwa siyo kila sababu inaweza kufanana, kama vile mmoja anaweza kujikuta yuko hatarini kukumbwa na maradhi kama ya kisukari, wakati mwingine akiwa katika hatari ya kukumbwa na saratani au shinikizo la damu na mengineyo, mtaalamu huyo anasema tabia ya kupima afya mara kwa mara inaweza kuwa suluhisho litakalokufanya utambue mapema tatizo na hatimaye kuanza kulishughulikia.

Mkakati wa Taifa wa lishe unasemaje?

Serikali iliweka Mkakati wa Taifa wa Lishe (NNS) ambao uliainisha vipaumbele vyake kuanzia Julai 2011 hadi Juni 2016. Mkakati huo ulilenga kuhakikisha taifa na watu wake wanastawi vyema. Mkakati huo ulikwenda sambamba na kuchangia katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta), Mkakati wa Afrika wa Lishe (2005-2015) na sera na mikakati ya Serikali ya Tanzania. Lengo la mkakati huo ni kukuhakikisha Watanzania wote wanafikia kiwango cha kuwa na lishe bora ikiwa ni hitaji muhimu la kuwa na afya njema na taifa lenye uwezo wa kuzalisha.

Inaelezwa kuwa lengo hilo litafikiwa kupitia sera zilizopo, mikakati, programu na ushirikiano wa pamoja kwa kutoa matokeo halisi na kuchukua hatua muhimu ili kuboresha hali ya lishe.

Katika hatua nyingine, mwaka 2015 Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO), liliitisha mkutano wa jopo la wataalamu duniani kwa ajili ya kubuni sera ya lishe. Mkakati wa pamoja wa kukabiliana na kudhibiti maradhi yasiyoambukiza 2013-2020, ulikuja na mapendekezo ya kuangalia mazingira halisi ya nchi, kila taifa lifikirie kutumia mbinu za kiuchumi zitakavyodhibitika na linaweza kuweka kodi na ruzuku kusudi kuboresha hali ya lishe na kuweka marupurupu kwa mabadiliko ya tabia ambayo yatachangia kuleta afya njema na upunguzaji ulaji wa vyakula visivyozingatia afya bora.

Ilihitimishwa kuwa kunauhalisia na hoja za msingi kuwa kukiwekwa kodi mahsusi kwenye vinywaji vilivyoongezwa sukari, kutasaidia kwa sehemu kubwa kupunguza matumizi yake na hasa iwapo ongezeko hilo litahusu bei ya wauzaji wa rejareja kwa asilimia 20. Pia, kuna uthibitisho ulio hai kwamba ruzuku ikiwekwa katika bidhaa kama matunda na mbogo za majani kwa asilimia 10 hadi 30, hali ya ulaji wake itaongezeka.

Ulaji unaozingatia afya bora

Msingi wa ulaji mzuri pia unagusia maeneo mengine yanayohusu mfumo wa maisha unaoheshimu afya kama vile kufanya mazoezi, kudhibiti uzito, vitamini D na nyongeza ya vitamini nyingine na unywaji wa kiasi kwa wanywaji wa pombe. Hizo ndizo dhana kuu zinazotumiwa na wataalamu wa afya.

Mpango huo kwa lugha nyingine ni mwongozo wa kujua aina na kiwango cha chakula kinachopaswa kuliwa katika maisha ya kila siku ili kuwa katika afya njema. Msingi wake mkuu unahusisha sehemu tatu; ya kwanza vyakula vitokanavyo na jamii ya mimea ambazo ni mboga za majani na kunde zake, matunda na punje. Sehemu ya kati ni ile inajumuisha maziwa, mtindi, nyama isiyokuwa na mafuta, nyama ya kuku, samaki, mayai, mbegu.

Sehemu ya mwisho ambayo ni ya juu ni kiwango mafuta kwa vile yanahitajika kiasi kidogo kila siku ili kusaidia afya ya moyo na ubongo.