Namna rahisi ya kuondoa kiribatumbo

Muktasari:

  • Kiribatumbo ni matokeo ya ulaji holela wa vyakula na kutoushughulisha mwili na mazoezi au kazi zinazoutembeza mwili

Kiribatumbo ni kiashiria kimojawapo cha uzito uliozidi au unene na ndiyo maana wataalamu wa afya hupima mzunguko wake kama moja ya njia ya kutathimini tatizo la unene.

Kiribatumbo ni matokeo ya ulaji holela wa vyakula na kutoushughulisha mwili na mazoezi au kazi zinazoutembeza mwili. Nitaeleza namna rahisi ya kuondoa kiribatumbo kama ifuatavyo.

Kufanya mazoezi mepesi na udhibiti wa ulaji holela wa vyakula hasa vinavyonenepesha ambavyo ni pamoja na vyakula vyenye mafuta mengi, sukari na wanga nyingi.

Ulaji wa vyakula visivyokobolewa mfano mikate ya ata ambayo unapoila humfanya mtu kujisikia ameshiba, lakini pia uwepo mashudu ambayo huwa hayana wanga yapo kuongeza ujazo tu.

Hivyo husaidia kumpunguzia wanga ambao unachangia kunenepa na kupata kitambi. Vile vile ulaji wa vyakula vya nyuzi nyuzi kama mboga mboga hasa zile mbichi.

Pale unapoitazama sahani yako yenye mduara wa nyuzi 360  ya mlo mkuu iwe na  chakula robo wanga, robo protini na nusu iwe mboga mboga na matunda.

Utahitaji kuwa na mwenendo na mtindo bora wa kimaisha kwa kutenga muda mwingi wa mazoezi mepesi ambayo yanahitaji dakika 150 kwa wiki, yaani sawa na dakika 30 kwa siku katika siku tano za wiki.

Kwa wenye viribatumbo ambao ni wanywaji pombe ambao tayari wana viribatumbo ni muhimu kuacha au wakishindwa wapunguze kiasi cha pombe waanze kunywa angalau kuwa mnywaji wa mwishoni mwa wiki na si kila siku.

Kwa upande wa mazoezi, si kila zoezi lina matokeo makubwa katika kudhibiti kiribatumbo. Yapo mazoezi ambayo huitaji kwenda vituo vya mazoezi yanaoonyesha kuwa na matokeo makubwa katika kudhibiti tatizo hili.

Mazoezi mepesi yanasaidia kuufanya mwili kushughulisha viungo vingi, hivyo kuchoma mafuta yaliyorundikana ikiwamo katika eneo la kitambi.

Lakini inashauriwa ili kuweza kuchoma mafuta ya ziada ni pale utakapofanya mazoezi mepesi kwa muda wa dakika 30 na kuendelea.

Ni muhimu kabla ya mazoezi yoyote, mwili uandaliwe kwa mazoezi ya viungo kwanza, ili kuuweka utayari wa viungo kufanya mazoezi kwa ufanisi.

Zoezi la kukimbia kidogo kidogo ni zuri na linawafaa vijana zaidi.

Watu wazima pengine kukimbia ni changamoto wanaweza kufanya zoezi la kutembea, lakini kwa mtindo wa kutupa mikono kama vile watembeavyo askari.

Mtindo huo husaidia kushughulisha maeneo mengi ya mwili ikiwamo misuli ya eneo la tumboni.

Kuruka kamba ni moja ya zoezi rahisi lenye matokeo makubwa katika kukabiliana na kiribatumbo. Tafiti zinaonyesha zoezi hili likifanywa kwa ufanisi linasaidia kupunguza tatizo hili kwa haraka.

Zoezi lingine ni kuogelea, pale unapofanya zoezi hili linahusisha utendaji wa misuli mingi ikiwamo ile ya tumboni.

Ili kukabiliana na tatizo hili kwa umaridadi zaidi inahitaji pia kufanya mazoezi yanayolenga moja kwa moja kuishughulisha misuli ya tumboni ambayo utayafanya ukiwa umetulia.

Ili kuleta matokeo chanya zaidi, mazoezi mepesi yanaweza kuchanganywa na mazoezi ya viungo ambayo yanalenga kuishughulisha misuli ya tumboni.

Pia tumia mbinu ya kutumia muda mwingi na mara kwa mara kukaza misuli yako ya tumbo hata unapokuwa katika kazi zako za kila siku inasaidia kuishughulisha misuli ya tumbo.

Unaweza kutumia dakika 30 hadi 60 kufanya mazoezi mepesi na dakika 10 mazoezi ya moja kwa moja ya tumboni. Baada ya mazoezi yoyote muhimu pia kutumia dakika tano za mazoezi ya kuupoza mwili.

Pakua video mbalimbali au apps zinazoonyesha aina hiyo ya mazoezi ya kuondoa kiribatumbo. Fika katika huduma za afya kwa ushauri na jenga tamaduni ya kuchunguza afya angalau miezi sita mara moja.