Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Njia bora na salama ya utayarishaji wa chakula

Muktasari:

  • Chakula kisicho salama kina uwezo wa kusababisha magonjwa mbalimbali na hata vifo.
  • Hali hii huathiri jamii kiafya na kiuchumi hivyo kurudisha nyuma jitihada za maendeleo ya jamii.

Chakula ambacho si salama ni kile ambacho hakijachafuliwa na vimelea vya maradhi, kemikali au takataka nyingine kama mchanga, majani, wadudu na madini, kwa kiasi ambacho kinaweza kusababisha madhara kwa mlaji.

Chakula kisicho salama kina uwezo wa kusababisha magonjwa mbalimbali na hata vifo.

Hali hii huathiri jamii kiafya na kiuchumi hivyo kurudisha nyuma jitihada za maendeleo ya jamii.

Uchafuzi wa chakula husababishwa na vimelea vya maradhi kutoka katika mazingira, wanyama, wadudu au binadamu.

Aidha, uchafuzi wa vyakula unaweza kusababishwa na sumu asili, mayai ya vimelea vya maradhi au mabaki ya viuatilifu pamoja na mabaki ya dawa zinazotumika kutibu mifugo.

Madhara yatokanayo na matumizi ya chakula kilichochafuliwa na vimelea vya maradhi, hujionyesha kwa mtu kupitia dalili kama kuumwa tumbo, kuhara, kuhara damu, kichefuchefu na kutapika.

Uchafuzi wa chakula husababishwa na kutozingatiwa kwa kanuni bora za utayarishaji wa chakula salama majumbani, hotelini, katika migahawa na kwenye maeneo mengine.

Ili kufanikisha utayarishaji wa chakula salama na hivyo kuepuka madhara yatokanayo na kula chakula kisicho salama, Shirika la Afya Duniani (WHO), limeainisha mambo matano muhimu ya kuzingatiwa.

Usafi ni tabia binafsi wakati wa kutayarisha chakula

Hali ya usafi ni tabia binafsi ya mwaandaaji wa chakula inahusisha mambo kama kunawa mikono kwa maji safi na sabuni mara tu baada ya kutumia choo, kabla ya kuandaa au kula chakula, baada ya kugusa chakula kibichi, kuokota vitu mbalimbali.

Mengine ni kugusa takataka, kukohoa, kupiga chafya, kugusa sehemu yoyote ya mwili, kufanya usafi na kugusa vyombo vichafu. Ni muhimu kuepuka kushika kwa mikono chakula kilicho tayari kuliwa, isipokuwa kwa kutumia kijiko au chombo kingine kinachofaa.

Mwandaaji wa chakula anashauriwa kuwa msafi muda wote, kuvaa mavazi safi wakati wa kuandaa chakula na kuepuka kushika sehemu za vyombo ambazo hugusana na mdomo wa mlaji.

Suala lingine muhimu la kuzingatia katika eneo hili ni kuhakikisha kuwa maeneo yote ya kuandalia na kuhifadhi chakula kama vile jokofu na kabati vinatunzwa katika hali ya usafi.

Wadudu kama mende na wanyama wadogo kama panya hawatakiwi kabisa kuwapo katika maeneo ya kutayarishia chakula, hubeba vimelea vya maradhi.

Vyombo vya kuandalia chakula kama sufuria, sahani, vikombe, visu, meza za kuandalia chakula, vinapaswa kuwa kwenye hali ya usafi wakati wote wa maandalizi na wakati wa kutoa huduma ya chakula.

Kutenganisha chakula kilichopikwa na kibichi

Chakula kilichopikwa kihifadhiwe sehemu safi na kuhakikisha kuwa hakichanganyiki na chakula kibichi kwani chakula kibichi kina uwezekano mkubwa wa kuwa na vimelea vya magonjwa.

Wakati wa kupanga vyakula katika jokofu, vyakula vibichi viwekwe katika safu za chini ili kuzuia majimaji yake kuchuruzika na kuingia kwenye vyakula vilivyopikwa.

Vifaa vya kukatia nyama mbichi au samaki wabichi vinapaswa kuoshwa vizuri na kuhifadhiwa katika hali ya usafi. Inashauriwa kutumia vyombo tofauti kwa vyakula vilivyopikwa na vile vibichi.

Kupika chakula mpaka kiive

Suala la kupika chakula mpaka kiive vizuri hasa nyama, mayai na samaki ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula husika. Vyakula vilivyopoa na viporo vinatakiwa kuchemshwa kikamilifu kabla ya kuliwa ili kuua vimelea vya magonjwa.

Kuhifadhi chakula kilichopikwa kwa uangalifu

Chakula kiliwe mara baada ya kupikwa, yaani kikiwa katika hali ya ujoto. Endapo chakula kilichopikwa hakitaliwa mara baada ya kupikwa, chakula hicho kihifadhiwe kwenye chombo kinachohifadhi joto au kwenye jokofu ili kuzuia kuzaliana kwa vimelea vya maradhi.

Wakati wa kupanga vyakula katika jokofu, vyakula vibichi viwekwe katika safu za chini ili kuzuia uchafuzi wa vyakula vilivyopikwa.

Kutumia maji na malighafi safi

Ni muhimu kuhakikisha kuwa maji ya kunywa ni safi na salama.

Matunda na mboga za majani vioshwe kwa maji safi na salama. Kwa vyakula vilivyofungashwa, mlaji anapaswa kuhakikisha kuwa muda wa matumizi haujapita na vifungashio viko katika hali nzuri, bila kupasuka, makopo hayajapata kutu, hayajatoboka, hajapondeka au kutuna.

Usafi wa jiko unapoandaa chakula

Ikumbukwe kuwa jikoni ni sehemu ya mapishi na ndilo eneo linalopaswa kutumika kwa maandalizi ya chakula.

Sio tu kwamba ni rahisi zaidi kupika jikoni kukiwa kusafi, bali pia ni njia nzuri ya kuhakikisha familia yako inapata chakula kilicho safi na salama.

Usafi wa jikoni unatakiwa uwe ni wa mara zote na wa kudumu. Jiko likiwa safi kuandaa chakula na kukipika linakuwa jambo la kufurahisha na kupendeza.

Hakikisha vifaa vyote vya jikoni vinakuwa safi na vinahifadhiwa mahali panapohusika, siyo leo kipo kabatini, kesho mezani mara chini ya meza.

Kila unapomaliza kutumia safisha kikaushe na weka mahali pake.

Na unaposafisha sakafu hakikisha vitu vilivyowekwa kwenye sakafu vinasogezwa na safisha sakafu vizuri kisha rudishia mahali pake.

Jitahidi kila siku kabla ya kulala vyombo vyote viwe safi.

Epuka kulaza vyombo vichafu jikoni.

Ni vizuri kama kuna kitu kimemwagika iwe mezani, kabatini au juu ya jiko ukasafisha mara moja ili isije kuwa ngumu baada ya kukaukia hapo.

Vyombo ambavyo havitumiki mara kwa mara viwekwe kabatini kuepuka kupata vumbi na pia ili jikoni pawe na nafasi wazi saidi.