Njia bora wenye maambukizi ya VVU kujifungua watoto salama
Dodoma. Mapambano ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, yanaweza kufanikiwa kwa kipindi kifupi kama wajawazito watahudhuria kliniki kwa mara ya kwanza chini ya wiki 12, ili kuanza utekelezaji wa afua za kuwakinga watoto iwapo atagundulika kuwa na virusi hivyo.
Pia mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) husisitiza umuhimu wa kufika kliniki kwa mara ya kwanza kabla ya wiki ya 14 ya ujauzito. Hii kwa hesabu ya miezi, ni sawa na miezi mitatu ya mwanzo.
Wakati akisoma bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2022/23, Waziri Ummy Mwalimu alisema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, wajawazito milioni 1.78 walihudhuria kliniki na kupatiwa huduma za afya.
Alisema asilimia 99.7 ya wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi ikilinganishwa na asilimia 85 mwaka 2020.
Hata hivyo, Ummy alisema changamoto iliyopo ni wanawake kuchelewa kuhudhuria kliniki wapatapo ujauzito.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wajawazito milioni 1.78, ni wajawazito 656,040 sawa na asilimia 37.6 walianza kupata huduma za wajawazito chini ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito, ikilinganishwa na asilimia 36 ya kipindi kama hiki mwaka 2020.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hakutazaa matunda iwapo wanawake hawatahudhuria kliniki mapema ndani ya wiki 12.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kiwango cha maambukizi wakati wa ujauzito (katika uterasi) ni asilimia 5 hadi 10, leba na kuzaa ni asilimia 10 hadi 15, wakati wa kunyonyesha baada ya kuzaa ni asilimia 5 hadi 10 na hatari ya kijumla bila kunyonyesha asimilia 15 hadi 25.
Takwimu zinaonyesha hatari ya maambukizi ya VVU kijumla na kunyonyesha hadi miezi sita ni asilimia 20 hadi 35, hatari ya kijumla na kunyonyesha hadi miezi 18 mpaka 24 ni asilimia 30 hadi 45 na jumla ya hatari ya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto asilimia 20 hadi 40.
Pia Waziri Ummy alinukuliwa hivi karibuni akisema watoto 6,000 nchini huzaliwa kila mwaka wakiwa na maambukizi ya VVU.
Akizungumza na Jarida la Afya, Daktari Bingwa wa Wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis Ifakara, Dk Elias Kweyamba anasema wanashauri mwanamke anapopata ujauzito kuwahi kwenda kliniki, kwa sababu kwa kufanya hivyo kunapunguza uwezekano wa kumwambukiza VVU mtoto.
“Akienda kliniki mapema anapimwa VVU na magonjwa mengine, iwapo amegundulika kuwa ameambukizwa VVU anaanzishiwa dawa za kufubaza virusi (ARVs), kwa hiyo uwezekano wa kumuambukiza mtoto akiwa tumboni ama wakati anazaliwa unapungua kwa sababu mama atakuwa anaendelea kutumia dawa,” anasema.
Dk Kweyamba anasema faida ya kuwahi kliniki si hiyo tu, bali na kumkinga mtoto na magonjwa mengine, ikiwemo kaswende kwa sababu mama anapogundulika huanza matibabu mapema.
Hali ikoje
Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto wa Mkoa wa Dodoma, Nice Moshi, akizungumza na Jarida la Afya, anasema suala la kuanza kliniki kabla ya wiki ya 12 baada ya mama kupata ujauzito bado halina viashiria vizuri kwa Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, wanawake waliohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza chini ya wiki 12 tangu wapate ujauzito, mwaka 2020 walikuwa ni asilimia 32.8 na idadi hiyo iliongezeka mwaka 2021 ambapo ilikuwa asilimia 39.9.
Anasema ongezeko hilo ni kutokana na afua zilizochukuliwa na mkoa ili kuongeza wajawazito wengi wanaohudhuria kliniki chini ya wiki 12 tangu wapate ujauzito.
“Na kila robo ya mwaka tunapeana ripoti, hivyo kinachofanyika ni kutoa elimu katika redio za mkoani hapa na kupitia kwa maofisa afya jamii umuhimu wa kuwahi kliniki wakati wanapojihisi kuwa ni wajawazito,” anasema.
Katika wilaya saba za Dodoma, Wilaya ya Kondoa katika eneo la Kondoa mji, anasema bado ipo nyuma kwa mahudhurio ya wajawazito kwa mara ya kwanza chini ya wiki 12.
Baadhi ya sababu zinazotajwa na wanawake kutowahi kliniki ni pamoja na kuhisi watachoka kama wakiwahi kuanza kliniki, sababu ambayo kwa wataalamu wa afya wanasema haina uzito.
Mbali na changamoto hiyo, Nice anataja pia kukosekana kwa uwazi. Anasema jambo hili limewafanya kuhimiza wanaume kushiriki katika afya ya uzazi na mtoto, ili kuwezesha kuwepo kwa uwazi katika afya za watu hao kwa wenza wao.
“Unaweza ukamshauri amshirikishe mwenza wake kufuatilia afya ya mama na mtoto inakuwa ngumu. Mwingine unaweza kumshauri akapima na kukutwa na maambukizi, lakini kwenda kumwambia mwenza wake inahitaji ujasiri wa pekee.
“Kama wenza wangekuwa wanashiriki kwenye afya ya uzazi na mtoto wangepata elimu kwa pamoja na kushauriwa kwenda kupima na hivyo hata wakigundulika kuwa na maambukizi ya VVU watakuwa wanatumia dawa kwa pamoja na kushirikiana, hivyo mwisho wa siku tunapata watoto wasiokuwa na maambukizi,” anasema.
Alipoulizwa utaratibu wa kuwataka wajawazito kwenda na wenza wao kama ulisaidia, Nice anasema utaratibu huo katika baadhi ya maeneo ulisababisha wanawake kukodisha wanaume baada ya wenza wao kukataa na hivyo kutoleta matokeo mazuri kama ilivyotarajiwa.
Afua zinazotekelezwa vituoni
Nice anasema lengo la kuhudhuria kliniki ni kuwezesha mama kupimwa afya yake na anapogundulika kuwa na VVU anafanyiwa ushauri na kuanzishiwa dawa za kupunguza makali ya VVU.
“Umuhimu kumwanzishia dawa mama mjamzito anayeishi na VVU ni kufanya maandalizi ya mtoto asipate maambukizi, hivyo mama anakuwa monitored (anafuatiliwa) katika kipindi chote cha ujauzito, huku anaendelea kupata dawa,” anasema.
Anasema mtoto pia hupewa dawa kinga inayojulikana kama profilaksisi na Neverapine Syrup ambayo hutumia kwa wiki sita, baada ya hapo ataendelea na Septine Syrup.
“Huyu mtoto sasa tunamfanyia vipimo, inategemea status (hali) ya huyu mama, kwa wale ambao ni high risk (wana vihatarishi vikubwa) tunachukua vipimo cha damu mbichi. Lakini kama mama hayuko katika tabia hatarishi, mtoto anachukuliwa vipimo akiwa katika wiki ya nne hadi sita,” anasema.
Anasema wakati huo wote wanaendelea kumshauri mama kunyonyesha mtoto maziwa yake tu bila kuchanganya na chochote kwa miezi sita.
Anasema hiyo inapendekezwa ili kuepuka kuleta michubuko katika tumbo la mtoto kwa kuwa linakuwa halijakomaa na baada ya miezi sita huchanganyiwa vyakula vingine kama mtoto mwingine asiyezaliwa na mama mwenye VVU.
Hata hivyo, anasema mtoto akishafikisha mwaka mmoja, mama anaacha kumnyonyesha mtoto ili kuepuka hatari ambazo huongezeka kadiri umri unavyokua.
Anasema mtoto anapofikisha miezi tisa huchukuliwa kipimo, wiki sita baada ya kunyonyeshwa na akifika miezi 18 ambacho ni kipimo cha mwisho kuonyesha kuwa hana maambukizi ya VVU.
Mratibu huyo anasema kipimo cha kwanza hakiwezi kuthibitisha afya ya mtoto aliyezaliwa, hivyo kuwataka wanawake wanapokutana na majibu tofauti kuendelea na hatua za kumkinga mtoto na VVU hadi kipimo cha mwisho kitakapotoa matokeo.
Sababu kutokwenda kliniki mapema
Naomi Malaji, mkazi wa kijiji cha Nguji kata Mndemu wilayani Bahi, anasema kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya wanawake wengi kutohudhuria kliniki kwa muda wote ni umbali mrefu wa kutoka katika kijiji hicho kwenda kwenye Zahanati ya Mndemu.
“Umbali wa kwenda hadi kwenye zahanati ni kilomita 12, ni vigumu kwa mwanamke asiyekuwa na fedha kwenda mara zote kliniki. Usafiri tu wa bodaboda ni Sh15,000, kwa hiyo tunaamua kwenda mara tatu hadi unajifungua hapo umejitahidi sana,” anasema.
Anasema pia wakati mwingine unaweza kukosa huduma za afya na hivyo unalazimika kutafuta usafiri wa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.