PIRAMIDI YA AFYA: Dawa ya mtu mwenye tatizo la nguvu za kiume hii hapa

Muktasari:

  • Uchovu au mwili kuchoka sana huchangia mtiririko wa tendo la ndoa kuathirika.

Yawezekana kuwa tuna majukumu mengi na tunafanya kazi sana ili kujipatia kipato, lakini katika kufanya kazi huko, huwa tunafanya kazi nzito zinazouchosha mwili kupita kiasi.

Kiasilia wanaume ndiyo wanaofanya kazi ngumu zinazochosha mwili zikiwamo za kuendesha magari makubwa kwa umbali mrefu, kazi za ujenzi, kubeba mizigo mizito kama ilivyo kwa makuli wa bandarini na sokoni.

Pia, kazi zingine ni zakutumia akili zaidi kama ya uhandisi wa mawasiliano na kazi za usanifu majengo.

Wanaume hufanya kazi zaidi na kutembea umbali mrefu ukilinganisha na mwanamke, hivyo hutumia nguvu nyingi kuyafanya mambo haya hali inayomletea uchovu mkali wa mwili.

Uchovu na mashinikizo ya kimwili nimojawapo ya mambo yanayochangia kwa wanaume wengi kupungukiwa na nguvu za kiume.

Unapokuwa katika hali hiyo ni vigumu kupata msisimko wa kimwili wa kufanya tendo la ndoa.

Kutumika sana kwa viungo vya mwili ikiwamo ubongo na misuli ya mwili baadaye humfanya muhusika kubaki na uchovu mkali uliotokana na matumizi yaliyopitiliza ya maeneo hayo mwilini.

Uchovu au mwili kuchoka sana huchangia mtiririko wa tendo la ndoa kuathirika.

Mwili unapochoka unashindwa kuwa na nguvu za kiume za kutosha hivyo kushindwa kwenda mizunguko kadhaa ya tendo la ndoa.

Kama tulivyoona katika Makala nilizowahi kueleza kuwa tendo hili linahusisha mfumo wa fahamu yaani ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, mfumo wa damu na moyo na misuli ya mwili.

Misuli hiyo ikiwamo ile ya uume, homoni za mwilini pamoja na kemikali zilizomo katika damu na sehemu za mwilini navyo vinahusika.

Uchovu mkali uliotokana na kufanya kazi ngumu bila kupata usingizi au mapumziko huwa  na mwingiliano na mtiririko mzima wa tendo hilo kwa ujumla.

Kupumzika ni kuutuliza mwili pasipo kujongesha viungo vya mwili wala kutukutisha, mfano unapoamua kukaa na kutulia hapo umepumzika, kitendo cha kulala ni kupumzika kwa mwili huku mwili ukiwa umezima mawasiliano ya nje ya mwili.

Kuupumzisha mwili kwa kulala usingizi kuna faida kubwa sana kiafya, kitaalamu kulala kunauwezesha mwili ulio mchovu kupata mapumziko.

Kulala peke yake kunaupa nafasi mwili kupata utulivu, kuukarabati na kuujenga, vilevile kupambana na maradhi na hitilafu mbalimbali zilizojitokeza mwilini.

Tafiti mbalimbali za kiafya zimeonyesha kuwa kulala kwa zaidi ya saa Sita kuna faida kubwa kiafya. kwani kunaonyesha kiwango cha homoni ya kiume iitwayo Testosterone mwilini huongezeka.

Kupanda kwa homoni hiyo ni faida kubwa kwa mwenye upungufu wa nguvu za kiume na hata asiye na tatizo naye hufaidika.

Homoni hii ndiyo inayosababisha tabia zetu za kiume ikiwamo yakuweza kupata hisia za tendo la ndoa, hivyo basi kuweza kuwa na nguvu za kiume imara.

Kitaalamu mwanadamu anatakiwa kupumzika kwa saa Sita hadi Nane, muda huo ndiyo unaweza kumtosheleza mwanadamu kupumzisha mwili wake na kuepukana na uchovu.

Ni vema wale wenye tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kujijengea mazoea yakulala kwa saa nyingi za kutosha ikiwa ni mojawapo ya mbinu rahisi za matibabu kabla ya kumfikia daktari.

Piga na sms kwa simu: 0763-296752