PIRAMINDI YA AFYA: Uhusiano baina ya TB na Ukimwi

Kifua Kikuu (TB) ni ugonjwa nyemelezi unaoongoza kusababisha vifo kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Wengi wenye TB duniani wamegundulika kuwa na VVU, hii ni kutokana na ukweli kuwa pale kinga ya mwili inaposhuka ndipo vimelea vya TB hupata nafasi ya kuushambulia mwili kwa kasi.
Vijidudu hivi huambukizwa kwa njia ya hewa, pale mwili unapokuwa na kinga imara huweza kudhibitiwa, lakini kinga ikitetereka kama ilivyo kwa waathirika wa VVU huweza kuibuka.
Mgonjwa mwenye TB pamoja na VVU uwezekano wa kupata TB kali au hai ni mara 21 hadi 34 ukilinganisha na mtu asiye na VVU.
Pale inapotokea uwepo wa maambukizi ya VVU, kinga ya mwili nayo hutetereka na kushuka hivyo mwili hukosa kinga na ugonjwa wa TB hupata nafasi ya kushambulia mwili.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kila mwaka watu milioni 10.5 huambukizwa kifua kikuu huku kati yao milioni 1.6 hufariki kila mwaka. Takwimu za hapa nchini zinaonyesha watu 70 hufariki kila siku kutokana na TB na watu 25,800 hufariki kila mwaka kwa ugonjwa huo.
Ingawa vifo hivyo ni sawa kwa wanawake na wanaume duniani, lakini kwa Bara la Afrika vifo hivyo ni zaidi kwa wanawake kuliko kwa wanaume.
Wengi wa wagonjwa wa VVU wanakumbana na udharula unaotishia maisha yao kutokana na kuwapo kwa TB sugu na isiyotibika hata kwa dawa mchanganyiko.
Hapa ndipo uhusiano wa karibu wa VVU na TB unapotokea na kushirikiana kuushambulia mwili, hatua za haraka zisipochukuliwa basi mtu huweza kudhoofu haraka na kupoteza maisha.
Dalili za ugonjwa wa TB ni kukohoa zaidi ya wiki mbili, uzito wa mwili kupungua kwa zaidi ya asilimia 10, kupumua kwa shida, maumivu ya kifua, kukohoa damu, kichwa kuuma, homa kali, kutokwa na jasho hasa nyakati za usiku, uchovu, kuvimba tezi za shingo na kwapani. Jambo la msingi na muhimu ni kuwahi kufika katika huduma za afya mapema unapoona dalili hizo. Na wale wote waliokatisha matibabu ya TB wafike katika vituo vya afya kwa ajili ya ushauri na matibabu.
Uwepo wa VVU na TB ni hatari zaidi, kwani husababisha mwili kudhoofu haraka na endapo hali hiyo isipodhibitiwa hatari ya mgonjwa kufariki ni kubwa zaidi ukilinganisha na yule mwenye TB bila VVU.
Hakikisha pale unapoona unakohoa zaidi ya wiki mbili unafika katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Ikumbukwe kuwa si kila mwenye TB ana VVU na pia si kila anayeishi na VVU ana TB.