Profesa Mkumbo ataka hatua zaidi kudhibiti magonjwa ya moyo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akiwa na viongozi mbalimbali baada ya kuweka jiwe la msingi jengo la tiba la wanamichezo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI tawi la Dar Group
Muktasari:
- Amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la tiba la wanamichezo ikiwa ni maandalizi ya AFCON 2027
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mpango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ameitaka jamii kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, akisema maradhi ya moyo yanachangia asilimia 25 ya magonjwa yanayowakumba Watanzania.
Amesema licha ya magonjwa hayo kuzuilika, Serikali bado hutumia fedha nyingi kugharamia matibabu, hivyo ni muhimu Wizara ya Afya ikaendelea kuweka mkazo katika utoaji wa elimu ya kinga.
Profesa Mkumbo amesema hayo leo Julai 10, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la Tiba ya Michezo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Tawi la Dar Group, litakalotumika kwa matibabu ya wanamichezo ikiwa ni maandalizi ya miundombinu itakayotumika kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
"Katika kila watu 10 hapa nchini, wanne wanasumbuliwa na matatizo ya moyo. Wito wangu kwa Watanzania ni kuendelea kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa haya. Njia mojawapo ya kujikinga ni kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi," amesema.
Amesema duniani magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.9 kila mwaka, huku akisisitiza kuwa jukumu la Wizara ya Afya si kutoa matibabu pekee, bali pia kusimamia afya za wananchi kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia magonjwa ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kwenye matibabu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la Tiba la Wanamichezo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI
Akizungumzia ujenzi wa jengo la tiba kwa wanamichezo, Profesa Mkumbo amesema Serikali itaunga mkono jitihada za JKCI kwa kutoa Sh6 bilioni zitakazoongezwa kwenye Sh12 bilioni zilizotolewa na taasisi hiyo, kufikia Sh18 bilioni zinazohitajika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi.
Amesema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Katika Dira ya 2050 yapo maeneo mengi yanayohusu afya. Malengo makubwa ni kuhakikisha afya kwa wote, kukomesha vifo vya akina mama na watoto, pamoja na kuimarisha na kuhamasisha utalii wa tiba. Tunataka wageni wanaokuja nchini wakihitaji huduma za matibabu wakimbilie JKCI," amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, amesema uwekaji wa jiwe la msingi ni ishara ya kuimarishwa kwa huduma za matibabu, uchunguzi, elimu na tafiti.
"JKCI imekuwa tumaini kwa wagonjwa wa moyo na imepunguza safari za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Mafanikio haya yametokana na ushirikiano kati ya Serikali na wataalamu wa afya. Hapa hatuweki tu jiwe la msingi, bali tunafungua ukurasa mpya wa huduma za moyo nchini," amesema.
Amesema Tanzania inaendelea kujenga uwezo mpya wa kutoa huduma za matibabu kwa wanamichezo wa ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha huduma za matibabu ya moyo barani Afrika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema katika kipindi hicho, JKCI imeanzisha matawi sita nchini na kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka takribani 500 hadi zaidi ya wagonjwa 1,500 kwa mwaka.
"Kuanzishwa kwa matawi ya JKCI kumepunguza adha kwa wananchi kwa kuwa huduma sasa zinapatikana karibu na maeneo wanayoishi. Kutokana na ongezeko la magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, taasisi imefanya uchunguzi katika mikoa 23 na kuwafikia zaidi ya watu 3,200, wengi wao wakipewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya kibingwa," amesema.
Akizungumzia mradi wa kituo cha afya ya moyo kwa wanamichezo, Dk Kisenge amesema kitakuwa kituo cha pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya kilichopo Misri.
"Kituo hicho kitakuwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu, bwawa la kuogelea, ukumbi wa mazoezi pamoja na miundombinu mingine ya kisasa itakayowawezesha wanamichezo na wananchi kupata huduma za kiwango cha kimataifa," amesema.
Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi itagharimu Sh18 bilioni, ambapo Sh12 bilioni zinatokana na mapato ya ndani ya JKCI, huku Serikali ikiombwa kuchangia Sh6 bilioni.
Dk Kisenge amesema mradi huo utatekelezwa kwa awamu tatu kwa gharama ya jumla ya Sh71 bilioni, huku matarajio yakiwa kukamilisha awamu ya kwanza ndani ya miezi sita.
Aidha, amesema JKCI imewasilisha andiko kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa ajili ya kuanzisha kampuni tanzu itakayosaidia kuongeza mapato ya taasisi kupitia uwekezaji katika huduma mbalimbali za kitabibu.
Katika hafla hiyo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema ushirikiano kati ya sekta ya michezo na afya umeleta mafanikio makubwa katika kulinda afya za wachezaji, hususan afya ya moyo.
Washiriki mbalimbali wa hafla ya uzinduzi wa jengo la tiba la wanamichezo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Tawa la Dar Group
"Miaka ya nyuma taifa lilipoteza vijana wengi kutokana na matatizo ya moyo, lakini tangu kuanzishwa kwa ushirikiano na JKCI, wachezaji wa timu za Taifa pamoja na wale waliopo katika vituo vya mafunzo wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo mara kwa mara na kupatiwa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kupumzika na kujikinga na matatizo hayo," amesema.
Amesema wachezaji sasa wanatumia vifaa maalumu vinavyovaliwa mwilini vinavyotuma taarifa kwa wataalamu wa afya endapo vitabaini changamoto yoyote ya kiafya, hatua inayosaidia kuwakinga na madhara makubwa.
Aidha, Karia amesema kituo kipya cha afya ya moyo kitakachojengwa kitatumika wakati wa fainali za AFCON na kitaendelea kutoa huduma kwa wanamichezo wa ndani na nje ya Tanzania hata baada ya mashindano hayo.
Akizungumzia matibabu ya moyo kwa watoto, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI, Dk Naizhijwa Majani, amesema tatizo la magonjwa ya moyo kwa watoto bado ni kubwa nchini.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto 10,000 wanaozaliwa, takribani 30 huzaliwa na matatizo ya moyo, sawa na karibu watoto 4,000 kwa mwaka. Hii ina maana kuwa wastani wa watoto 40 huzaliwa kila siku wakiwa na matatizo ya moyo yanayohitaji matibabu ya haraka.
Dk Majani amesema mwaka 2023 walianzisha Heart Team Africa Foundation kwa lengo la kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo.