Sababu likizo ya uzazi kwa watoto njiti kuongezwa

Dodoma. Kuna simulizi nyingi za baadhi ya wanawake kupoteza ajira baada ya kujifungua watoto njiti kutokana na kuhitaji muda wa ziada wa kulea watoto hao baada ya likizo ya uzazi ya miezi mitatu kumalizika.

Miongoni mwa wanawake hao ni Janeth Simon, anayesema baada ya kujifungua mtoto njiti na kutakiwa kurudi kazini baada ya miezi mitatu, aliamua kuendelea na malezi, hivyo kupoteza ajira.

“Likizo ilipokwisha nilimuomba mwajiri aniongezee muda, alikataa na kuniambia nichague kuendelea na kazi au nikalee mtoto. Nilichagua kwenda kumlea mtoto,” anasema.

Kilio hicho cha nyongeza ya uzazi hasa kwa waliojifungua watoto njiti ni cha muda mrefu, hasa kutokana na changamoto za malezi kwa watoto hao.

Wadau wa masuala ya uzazi wanapendekeza muda huo uongezwe kutoka miezi mitatu hadi sita, ili wanawake wenye watoto hao wapate muda zaidi wa kuwahudumia watoto.

Sababu hizo zinatajwa kuwa ni kutokana na mama kulazimika kukaa kwa muda mrefu wa hadi miezi mitatu hospitali na wataalamu wanahitaji kufuatilia maendeleo ya mtoto kila wiki na uangalizi maalumu wa mama anayefundishwa jinsi ya kumtunza.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha watoto njiti 210,000 huzaliwa kila mwaka nchini, huku 13,900 kati yao wakifariki dunia kwa kukosa huduma wakiwa hospitalini. Tanzania inatajwa kuwa nchi ya 12 kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto njiti duniani.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) mwaka 2020 inaonyesha kati ya watoto 10 wanaozaliwa, mmoja ni njiti na kila sekunde 40 mtoto mmoja kati ya hao hufariki dunia.


Changamoto za watoto njiti

Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa watoto, Albert Chota anasema watoto hao wanapozaliwa mifumo yote ya mwili, ikiwemo wa kujipatia joto na viungo ndani ya mwili vinakuwa havijakomaa.

“Wakati mwingine hawezi kunyonya wala kunywa, kwa hiyo hawezi kujitengenezea joto na hivyo anapata upungufu wa joto mwilini, sukari na maji. Ndani ya siku saba wengine hadi wiki mbili wanarudi nyuma (kupungua uzito),” anasema.

Anasema kutokana na kushindwa kunywa, watoto hulazimika kulishwa kwa mpira, huku mama akiwa amemkumbatia mtoto wake kwa staili ya kangaroo ili kumpatia joto ambalo anashindwa kulitengeneza.

Anatoa mfano wa mtoto aliyezaliwa na kilo 1.5 ndani wiki moja anaweza kupungua hadi kilo 1.2, hivyo hadi kurudia kilo alizozaliwa nazo inaweza kumchukua wiki tatu hadi nne kama wataalamu na mama hawajafanya kazi ya ziada.

Daktari huyo anasema hali hiyo inawafanya baadhi ya wanawake kukaa wodini kati ya miezi miwili hadi mitatu, hivyo kama ni likizo ya miezi mitatu inakuwa imekwisha.

Anasema kwa sababu hata wakitoka hospitali huwa wanafuatiliwa, hivyo inamlazimu mama ampeleke mtoto kliniki mara kwa mara hadi anapotimiza mwaka mmoja.

“Watoto hawa wanahitaji uangalizi wa mama kwa muda mrefu, akimwachia mtu mwingine anaweza kumpa maziwa kwa haraka ukakuta mtoto anapaliwa na kufa.

“Kina mama huwa tunawafundisha jinsi ya kukaa na mtoto na kumchunguza mara kwa mara,” anasema.

Hivyo anasema mama kwenda kazini wakati ndiye aliyefundishwa jinsi ya kumtunza akiwa hospitali inakuwa jambo gumu kufanywa na mtu mwingine.

“Kisaikolojia wanawake hawa wanaathirika, unakuta kila mara anatoa machozi, anachoka kukaa hospitali muda mrefu. Anavyomzoea mtoto anakuwa anaguswa sana. Sasa unapomtenganisha ukimwambia aende kazini (kabla ya hali ya mtoto kutengamaa) kisaikolojia hawezi kuwa vizuri wala kazi hataweza kufanya vizuri,” anasema.

Anasema likizo ndefu yenye malipo ambayo yatamsaidia kugharamia safari za hospitali kila mara na matunzo mengine ni muhimu kwa mama ili afya ya mtoto njiti iimarike.


Jinsi ya kuepuka kujifungua mtoto njiti

Zipo sababu nyingi zinazotajwa na wataalamu wa afya zinazochangia kuzaliwa kwa watoto hao na miongoni mwao ni unywaji wa pombe, uvutaji sigara, dawa za kulevya, upungufu wa damu, magonjwa ya zinaa, shinikizo la damu na msongo wa mawazo.

Sababu nyingine ni matatizo katika mji wa mimba na shingo ya uzazi kuwa dhaifu, hivyo kusababisha mtoto kuzaliwa kabla ya muda wake.

Dk Chota anasema, “kabla ya kuolewa mabinti wapimwe afya zao kwa sababu kuna matatizo yanaweza kukufanya kuashiria kuwa huyu anaweza kupata tatizo wakati wa ujauzito.

“Kabla ya kupata ujauzito yeye na mumewe wapime kwa sababu kuna magonjwa yanaweza kutibika na mtu asizae mtoto njiti.”

Anasema iwapo mama atapimwa mapema, kuhudhuria kliniki ipasavyo na kupimwa kikamilifu anaweza kuepukana na changamoto hiyo.

“Mama anatakiwa kupata faraja, utulivu wa akili, kusiwepo na ugomvi nyumbani, apatiwe matunzo na kupewa chakula anachotaka. Hii ni kwa sababu mama akipata ujauzito vile vichocheo mwilini vinabadilika, kwa hiyo hali yake kisaikolojia inabadilika, hisia zake zinakuwa juu,” anasema.

Dk Chota anasema mjamzito anatakiwa kutosimama na kufanya kazi kwa muda mrefu kwa sababu inasababisha mazingira yasiyo mazuri ya mtoto kukaa tumboni, hivyo kutoka kabla ya miezi tisa.

Kwa upande wake, daktari kutoka Shirika la Kimataifa la Save Children, Benny Ngereza anasema si watoto wala wanawake wote baada ya kumaliza likizo ya uzazi ya siku 84 (miezi mitatu) wanakuwa katika hali ya afya njema, ikiwemo watoto njiti.

Anasema baadhi ya watoto njiti hawapati changamoto siku za awali wanapozaliwa, lakini wanapata tatizo baada ya siku kusogea, hivyo wakati mama anamaliza likizo ya uzazi ndio mtoto anakuwa na changamoto, hivyo kuhitaji uwepo wake zaidi.

“Wakati wanarudi nyuma kiafya ndio likizo ya uzazi inaisha, lakini mwajiri anamhitaji kazini…Lakini hili suala linazungumzika,” anasema.


Harakati zinazoendelea

Taasisi ya Doris Mollel (DMF) ni miongoni mwa wadau wanaopigania suala la likizo ya uzazi kuongezwa kutoka miezi mitatu hadi sita kwa wanaojifungua watoto njiti tangu mwaka 2017.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Doris Mollel anasema mwaka 2021 waliamua kuita ajenda ya mtoto njiti ikiwa na mambo makuu matano ambayo ni Serikali itenge bajeti, bima za afya na elimu juu ya mtoto njiti ingizwe katika somo la baiolojia.

Jambo lingine ni kuruhusiwa kwa waliojifungua kuwahudumia wakiwa hospitali na likizo ya uzazi ili kuwezesha mama kumlea mtoto kwa utaratibu wa kangaroo kwa sababu tafiti na Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha ni njia nzuri ya kumtunza mtoto.

Hata hivyo, Doris anasema wamefanikiwa mambo matatu isipokuwa bima ya afya na kuongezwa kwa likizo ya uzazi ambayo liko kwenye mchakato mzuri wa kuwezesha marekebisho ya sheria.

Anasema kwa kushirikiana na wizara nyingine wamefanya uchambuzi wa sheria zinazoathirika kutokana na marekebisho hayo na kubaini kuwa zipo 13.

Doris anasema kinachosubiriwa sasa ni Serikali kutoa uamuzi kuhusu suala hilo kwa sababu uchambuzi na utafiti umeshafanyika na kwamba anatamani matokeo chanya ya harakati hizo angalau yaonekane mapema.

Anasema njia inayoshauriwa na WHO ya kumtunza mtoto njiti ni kangaruu ambayo inamfanya mama kuchukua muda mrefu hadi kutengamaa.

“Zipo kesi nyingi za waliojifungua watoto njiti kupoteza kazi zao wakati wakihangaika na watoto ili watengamae kabla ya kuwaacha na watu wengine nyumbani,” anasema.