Sababu zinazochochea wanaume kufariki mapema

Kwa ujumla wanaume wanafariki mapema kutokana na kuwa na idadi kubwa ya vihatarishi, ikiwamo uasili wa kibailojia na kufanya kazi ngumu ambazo zinamweka katika hatari ya kifo.

Kazi hizo ni pamoja na za kijeshi vitani, polisi, zimamoto, kazi za ujenzi mkubwa, uchimbaji madini, kuendesha mitambo na vyombo vya usafiri na kutembea umbali mrefu katika maeneo hatarishi.

Mwanamume pia anaingia katika matatizo ya kitabia wakati wa balehe na kuendelea, hivyo kujikuta katika uhalifu, ugomvi, migogoro ya kimahusiano au kugombania mpenzi au mke.

Takwimu za kitafiti za wataalamu wa saikolojia na magonjwa ya akili zinaeleza kuwa wanaume wanajiua zaidi kuliko wanawake. Kwa kila watu wanne wanaojiua wanaume idadi ni watatu.

Inaelezwa kuwa wanaume wana kawaida ya kuficha vitu na kutosema wala kufika katika huduma za afya, hatimaye kuwaletea msongo mkali wa mawazo.
Matukio mengine ni pamoja kutumia vilevi au pombe kupita kiasi, kutumia dozi kubwai za matibabu kupita kiasi au dawa za kulevya.

Ukiacha mambo hayo, tukiangalia katika sababu za kiafya ambazo zinaweza kuchangia wanaume kufariki mapema, takwimu zinaonyesha wanaume wengi duniani wanaugua mara kwa mara magonjwa ya moyo kuliko wanawake.

Magonjwa ya moyo ndiyo yanashika namba moja katika kusababisha vifo vingi duniani, hiyo inawaweka kuwa katika hatari ya kufariki kwa magonjwa ya moyo kwa zaidi ya asilimia 50.

Hata katika utafiti wa kutazama, utagundua kuwa wanawake wajane wazee wenye miaka 60 na zaidi ni wengi zaidi kuliko wanaume katika jamii nyingi duniani, ikiwamo Tanzania.

Katika miaka mitatu iliyopita, ongezeko la wigo wa kufariki ni kubwa zaidi kwa wanaume duniani katika kipindi cha mlipuko wa mafua makali ya Uviko19.

Katika machapisho ya kitafiti ya Novemba mwaka 2023 katika jarida la JAMA, lilitoa taarifa ya kitafiti kuonyesha namna idadi kubwa ya wanaume walivyofariki kwa Uviko-19 kuliko wanawake.

Wanaume walikuwa na vihatarishi vingi mbalimbali, ikiwamo magonjwa yasiyoambukiza, hali iliyowafanya kufariki zaidi kipindi cha mlipuko huo.

Sababu za kimwili ni pamoja na mwanaume kuwa na upungufu wa chembe ya urithi ya “X” inayomfanya kupata mabadiliko zaidi katika jeni zake.
Hii ni moja ya sababu inayomfanya kuwa katika hatari ya magonjwa zaidi, ikiwamo kupata saratani kuliko mwanamke ambaye ana chembe “X” mbili.

Hatari ya kuzaliwa na hitilifa za kimwili katika nyumba za uzazi ni kubwa zaidi kuliko kwa mtoto wa kiume, hivyo kuwaweka katika hatari ya kufariki mapema zaidi.

Mwanamke kuwa na kichochezi cha kike kijulikanacho kama Eastrogeni ambacho kinawapa faida zaidi, kwani kinawapunguzia hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Sababu nyingine ni za kitamaduni, ikiwamo kuoa wanawake wenye umri mdogo, wanaume kutengwa kijamii na wanawake kupata huduma nyingi za afya zinazomjali zaidi mwanamke kama kundi maalumu.

Ili kupunguza vifo vya mapema na kupunguza wigo wa kufariki mapema duniani, inahitajika mwanaume kuwa na mienendo mizuri na mitindo mizuri ya kimaisha, ikiwamo kuepuka unywaji pombe kupita kiasi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, dawa za kulevya na ulaji holela wa vyakula.

Kufanya mazoezi mapesi ili kulinda wasipate unene, kulala na kupumzika, kujiepusha na vitu vinavyoleta msongo wa mawazo na wafanye mambo ya kuburudisha akili ili kuzuia magonjwa ya akili.

Vile vile kuepuka kufanya kazi ambazo zinamweka katika mazingira yenye ukaribu na sumu na mionzi hatari.