Saratani inavyotesa watoto, KCMC kufanya utafiti
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga akizungumzia changamoto ya saratani kwa watoto wadogo.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Kulingana na takwimu mpya za Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) idadi ya wagonjwa wa saratani inaendelea kuongezeka nchini huku takribani wagonjwa wapya 6,000 wakiripotiwa kila mwaka hospitali hapo.
Moshi. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), imesema wataalamu wake watafanya utafiti kubaini sababu ya asilimia 40 ya wagonjwa 6,000 wanaopatiwa matibabu kila mwaka hospitalini kuwa ni kundi la watoto.
Uamuzi huo wanaufanya siku moja tangu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga kusema: “Asilimia 60 ya wagonjwa wa saratani wanahitaji tiba ya mionzi hapa KCMC miongoni mwao asilimia 40 ni watoto.”
Leo Jumatatu, Mei 18, 2026, Mwananchi limezungumza na Msemaji wa Hospitali hiyo, Gabriel Chiseo ambaye amefafanua sababu ya idadi ya watoto kuwa kubwa kwamba hawawezi kusema idadi hiyo ni kubwa hadi watakapofanya utafiti na wataalamu wao wanajiandaa kwa hilo.
Amesema huenda pia idadi hiyo imechangiwa na utoaji wa huduma hiyo hospitalini hapo kwani mwaka 2015 kurudi nyuma hawakuwa na huduma ya matibabu ya saratani.
"Miaka ya nyuma hatukuwa na matibabu ya saratani na wagonjwa wengi walikuwa wakienda Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dar es Salaam kupata matibabu na wengine wanabaki nyumbani.
"Ukaribu wa huduma nao unawafanya watu wengi kujitokeza tofauti na awali, kwa tathimini ndogo tulibaini jamii ya Wamasai ndio wanaopata shida hii ya saratani tutafanya utafiti kuangalia sababu," amesema.
Msemaji huyo amesema wananchi wanaposogezewa huduma kwa kiwango kikubwa hubainika kuwa na matatizo mengi ya kiafya.
Mei 17, 2026, Profesa Masenga alibainisha kiwango hicho wakati wa matembezi ya hisani ya kuchangia mahitaji ya watoto wenye saratani wanaotibiwa katika hospitali hiyo, yaliyoandaliwa na wa Waokaji Tanzania (Bakers Meetup Tz).
“Hapa KCMC tunaona wagonjwa wengi wa saratani kwa mwaka, wagonjwa wanaoonwa wanaweza kufikia hadi 6,000 kwa mwaka. Lakini wagonjwa wapya wanaweza kufika 1,500,” alisema Profesa Masenga.
Profesa Masenga alisema kwa sasa hospitali hiyo inatoa tiba kamili ya saratani na kwamba imekuwa na mafanikio makubwa zaidi kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu.
“Kama mnavyofahamu, saratani inatibika kwa mionzi, asilimia 60 ya wagonjwa wa saratani wanahitaji tiba ya mionzi hapa KCMC miongoni mwao asilimia 40 ni watoto. Sasa hivi haihitajiki tena kuwatuma wagonjwa wa saratani kwenda Ocean Road.
“Kutoa tiba kamili hapa KCMC imekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wanaoishi kanda hii ya Kaskazini,” alisema Profesa Masenga.
“Tuliamua kwenda kwa watoto kwa sababu tuliona kwamba saratani nyingi za watoto zinapona lakini watapona wakija mapema na kupata tiba kamili, na tiba kamili inachukua muda, kuna watoto pale wamekaa hadi miaka miwili lakini wengi ni miezi sita hadi mwaka mmoja.”
Profesa Masenga amesema saratani ambayo imekuwa ikiwasumbua watoto wengi ni ya damu ambayo matibabu yake yakiwahiwa inapona.
“Watoto wengi ambao tunawaona hapa ni wenye saratani ya damu (leukemia), macho na tezi lakini nyingi zinapona zikiwahiwa. Changamoto tunayoipata ni kwamba wengi wanakuja wakiwa wamechelewa kwa sababu ya utambuzi.
“Utambuzi umekuwa ni changamoto katika hatua ya familia na hospitali nyingi hizi za kati kwa sababu mtoto anaweza kuwa na homa isiyopona kumbe ana saratani,” alisema Profesa Masenga.
Profesa Masenga alisema tangu kuanza kutolewa kwa huduma ya tiba ya mionzi hospitalini hapo mwaka huu, watoto 80 wamefanikiwa kupata matibabu hayo.
Akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya damu na saratani za watoto wa hospitali hiyo, Dk Ester Majaliwa alisema saratani si laana wala uchawi, bali ni ugonjwa ambao unaweza kuwatokea watoto na ukigundulika mapema unatibika kabisa.
Aidha, aliwataka wazazi kuwa makini na kufuatilia mabadiliko ya afya za watoto wao, hasa wanapougua mara kwa mara bila kupona licha ya kupatiwa matibabu.
Alitaja baadhi ya dalili zinazopaswa kupewa uzito kuwa ni pamoja na mtoto kupungua uzito, kutapika mara kwa mara, kuchoka kupita kiasi na homa zisizoisha licha ya kutumia dawa.
“Mtoto anapoanza kuumwa na haponi ndani ya wiki ya kwanza au ya pili baada ya kupatiwa matibabu, wazazi wasichukulie hali hiyo kuwa ya kawaida, inaweza kuwa ni dalili ya saratani, hivyo ni muhimu mtoto kufanyiwa vipimo zaidi,” alisema Dk Majaliwa.