Serikali yatoa wito uchangiaji damu wa hiari
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika Juni 14, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema Serikali inaendelea kuimarisha vituo vya damu salama nchini, kununua vifaa vya kisasa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu na mazao yake.
Dar es Salaam. Serikali imewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi na mara kwa mara kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya maelfu ya wagonjwa, hususan akina mama wajawazito, watoto wenye upungufu wa damu, wagonjwa wa saratani na wenye ugonjwa wa selimundu.
Wito huo umetolewa leo Jumapili, Juni 14, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, Dk Samizi amesema uchangiaji damu ni tendo la utu na uzalendo linalochangia kuokoa maisha ya Watanzania wengi wanaohitaji huduma za matibabu.
"Kitendo cha kuchangia damu ni alama ya mshikamano wa kitaifa na ni tendo la utu linaloacha alama ya kudumu katika maisha ya wagonjwa. Tunawashukuru wachangia damu wote kwa moyo wa kujitolea na kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu," amesema.
Amesema damu ni tiba ya kipekee ambayo haiwezi kutengenezwa viwandani, hivyo wagonjwa wanaopoteza damu kutokana na ajali, akina mama wakati wa kujifungua, watoto wenye malaria kali, wagonjwa wa saratani na wenye selimundu hutegemea moyo wa kujitolea wa wachangia damu.
Dk Samizi amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha damu inayopatikana inatumika kwa ufanisi pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ya damu ikiwemo chembe nyekundu za damu, chembe sahani (platelets) na plasma.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika Juni 14, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
"Serikali inaendelea kuimarisha vituo vya damu salama nchini, kununua vifaa vya kisasa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu na mazao yake. Lengo ni kuhakikisha damu salama inapatikana kwa wingi na wakati wote," amesema.
Amesema mtu mwenye umri wa miaka 18 hadi 65, uzito wa kuanzia kilo 50 na afya njema anaweza kuchangia damu, huku wanaume wakishauriwa kuchangia kila baada ya miezi mitatu na wanawake kila baada ya miezi minne.
Katika hatua nyingine, Dk Samizi amesema Serikali haitavumilia vitendo vya baadhi ya watumishi wasio waadilifu wanaodaiwa kuuza damu katika baadhi ya vituo vya afya.
"Serikali imekuwa ikichukua hatua kali dhidi ya wanaobainika kufanya vitendo hivyo. Tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa kupitia Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) ili kukomesha vitendo vinavyohujumu juhudi za Serikali," amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam, Betia Kaema amesema taasisi hiyo ni mdau katika kuhakikisha damu salama inapatikana nchini kwa kuwa husambaza bidhaa zote muhimu zinazotumika katika ukusanyaji, uchunguzi na uhifadhi wa damu.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika Juni 14, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kaema amesema kwa miaka mingi MSD imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo bila changamoto.
"Mahitaji yaliyowasilishwa yalikuwa takribani vipande 7,600 vya bidhaa mbalimbali lakini MSD iliweza kusambaza zaidi ya vipande 9,000. Hii inaonyesha kuwa tumejipanga vyema kuhakikisha upatikanaji wa vifaa hivyo wakati wote," amesema.
Kaema amesema kupitia kanda 10 za MSD nchini, bidhaa zote zinazohitajika katika ukusanyaji na uchakataji wa damu zinafikishwa hadi katika vituo vya afya vya mijini na vijijini.
Maadhimisho ya mwaka huu yamekusanya wachangia damu, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji damu wa hiari na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa damu salama katika kuokoa maisha.