Simulizi aliyepona upofu uliosababishwa na kisukari

Matatizo ya macho yapo mengi katika jamii, yanatibika iwapo mgonjwa ataonana na daktari mara anapoona dalili, ikiwemo kupoteza uwezo wa kuona.

Ugonjwa wa kisukari unaweza kuathiri macho na kusababisha matatizo mbalimbali ya maono, ikiwemo  mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho unaorekebishika kwa miwani, shinikizo la macho na madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye macho.

Rashid Chande (60) maarufu kama “Babu kuku”, mkazi wa  Mtaa wa Pipeline, Kata ya Wambi  wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa, anasema alishindwa  kuona kwa muda wa miezi sita kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Chande anasema tatizo la kushindwa kuona lilianza baada ya kuanza kutumia dawa za kisukari, hali ambayo ilianza kidogo kidogo na mwisho kutoona kabisa. Kwa mujibu wa mgonjwa huyo, inaonyesha dawa alizokuwa akitumia ndizo zilizomsababishia kupata athari hiyo, hivyo alilazimika kwenda Hospitali ya Ikonda kwa ajili ya kupima ili atibiwe.

“Nilipata tabu sana kwa sababu mwazo nilikuwa naona, nilikwazika sana hadi roho ilikuwa inaniuma, lakini sikuwa na uwezo ila namshukuru mke wangu ameniuguza vizuri na kunipa imani kuwa ipo siku nitaona tena,” anasema Chande.

Baada ya kurudi kutoka hospitali ya Ilembula, alipata taarifa ya ujio wa madaktari bingwa wa macho katika chombo kimoja cha habari kilichopo wilayani hapa.

“Niliposikia taarifa hiyo nilisubiri hadi walipofika, nilipimwa na kufanyiwa upasuaji, nashukuru sasa naona, naendelea kusimamia shughuli zangu kama kawaida,” anasema.

Tatizo la kuona alilipata Machi mwaka huu na alifanyiwa upasuaji na madaktari hao Julai mwaka katika kituo cha Afya Tumaini Jipya.


Daktari ataja chanzo

Daktari wa macho katika Hospitali ya Mji Mafinga, Dk Robert Michael anasema dawa za kisukari haziwezi kusababisha tatizo la macho,  lakini  ugonjwa huo ndio unaweza kusababisha tatizo hilo.

Anasema mtu akiwa na kisukari anaweza kupata tatizo la mtoto wa jicho au shinikizo la macho (glaucoma), hivyo ni vizuri jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.

“Wanajamii wawe na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara, ikiwemo shnikizo la damu pamoja na sukari kwa sababu magonjwa hayo yanakuwepo bila kuonyesha dalili zozote,” anasema Dk Michael.

Pia anasema ni jambo zuri kwa mgonjwa mwenye kisukari kupima presha ya macho mara kwa mara pamoja na kutumia dawa alizopewa kwa usahihi, kwani magonjwa hayo yanaweza kusababisha uoni hafifu yasipodhibitiwa.

“Mfano, mgonjwa unayemzungumzia atakuwa alianza kutumia dawa za sukari wakati ugonjwa huo umeshafanya uharibifu kwenye macho yake, ndio maana alipata ugonjwa wa glaucoma,” anasema. Daktari huyo anasema presha au sukari ikishafanya uharibifu kwenye macho (uoni  hafifu) ni vigumu kurudi katika hali yake ya awali kwa sababu inakwenda kuharibu mishipa ya jicho, hivyo mgonjwa anaweza kupata glaucoma.


Baada ya kuona

“Kitu cha kwanza ambacho nilitamani kuona wakati nilipokuwa sioni ni biashara yangu ya chips kuku namna inavyoendelea, mke wangu alikuwa anaisimamia, lakini wafanyakazi walikuwa hawamsikilizi vizuri, tofauti na jinsi wanavyonisikiliza mimi,” anasema.

Kutokana na hali aliyopitia, anaishauri jamii kuwa na utaratibu wa kuwaona wataalamu wa macho, badala ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutibiwa magonjwa hayo.

Khadija Rajabu (45), mke wa Rashidi anasema, “nilikuwa najisikia vibaya huku nikimuomba Mungu amfanyie miujiza, bado siamini kama anaona tena.”

Anawashauri wanawake kukabiliana na changamoto katika maisha ya ndoa, hivyo hawapaswi kumkimbia mwenza anapopata matatizo.