Sonona tatizo la kiafya lisilopewa uzito na wanajamiii

Muktasari:

  • Tatizo hili huathiri afya ya akili na mwili kwa ujumla. Takwimu zinaonyesha kuwa athari zake hujitokeza kwa asilimia 10 ya jamii fulani duniani. Mara nyingi, huwakumba zaidi watu wenye umri kati ya miaka 10 na 24.

Yapo matatizo ya kiafya ambayo jamii imekuwa ikiyapuuza kuwa siyo changamoto kubwa. Mojawapo ni Sonona ingawa kwa lugha ya kitabibu hujulikana kama Depression.

Tatizo hili huathiri afya ya akili na mwili kwa ujumla. Takwimu zinaonyesha kuwa athari zake hujitokeza kwa asilimia 10 ya jamii fulani duniani. Mara nyingi, huwakumba zaidi watu wenye umri kati ya miaka 10 na 24.

Depression kama wengi walivyozoea ni tatizo linalosababisha kushuka kwa hisia au mihemko ya kimwili hivyo mhusika kutojihusisha na shuguli yoyote suala linalomuathiri kimawazo, kitabia na hisia za mwili na kutojiona sawa kama walivyo watu wengine wanaomzunguka.

Mtu mwenye Sonona hukosa furaha, huwa muoga na kukosa matumaini. Mara kadhaa huwa hana msaada, hukerwa bila sababu za msingi, hujiona mkosefu, mwenye kuaibisha na asiye mtulivu.

Mtu mwenye tatizo hili anaweza pia kukosa hamu ya kujishughulisha na chochote ikiwa ni pamoja na kufanyakazi ambayo awali alikuwa akiipenda na kuifurahia.

Vilevile anaweza kukosa hamu ya kula au kula kupita kiasi. Anakosa umakini wa mambo, anashindwa kukumbuka masuala binafsi kwa kina na pia na mara nyingine akawa na tabia za kujaribu kujiua.

Mambo mengine yanayoweza kumpata mtu huyu ni kukosa usingizi, kulala kulikopitiliza, mwili kuumwa na uchovu mkali. Wakati mwingine huweza kuwa na matatizo ya usagaji chakula au nguvu za mwili kupungua.

Kupata Sonona ni zaidi ya kuwa na huzuni, kwa maana nyingine ni kukosa raha kulikopitiliza. Tatizo hili linamtokea mtu akiwa amepata dalili hizi mfululizo kwa zaidi ya wiki mbili.

Sababu zinazochangia kutokea kwa tatizo hili ni zile za kimwili (kibailogia) na kisaikologia. Kimwili ni pamoja na mabadiliko katika ubongo, kemikali zinazosafirisha taarifa na homoni (lakini bado haijulikani kwa kina sababu zakibailogia/kimwili zinavyosababisha sonona kutokea).

Mazingira tunayoishi ndiyo huwa chanzo cha matatizo ya kisaikolojia ambayo huweza kuwa kufiwa au kumpoteza mtu wa karibu, kupoteza kazi, kufilisika, kupokea taarifa mbaya na kuwa katika mazingira magumu.

Endapo hatua za makusudi hazitachuliwa kwa haraka mhusika huwa kwenye hatari ya kujiua au kuchanganyikiwa kiasi cha kupata uwendawazimu wa kudumu.