Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tahadhari matumizi ya dawa za kikohozi kwa watoto msimu huu

Muktasari:

  • Magonjwa ya mafua na kikohozi mara nyingi huambatana na mabadiliko ya hali ya hewa, hali inayowasumbua watoto pamoja na watu wazima, kiasi kwamba matumizi ya dawa za kikohozi na kifua huongezeka.



Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea nchini kwa sasa, imebainika kuwa watoto wengi wanaugua magonjwa ya kifua, mafua na kikohozi.

 Hivi sasa ni kipindi cha kipupwe, hali inayochangiwa na upepo mwingi, vumbi na ubaridi hasa nyakati za jioni.

Aidha, magonjwa ya mafua na kikohozi mara nyingi huambatana na mabadiliko ya hali ya hewa, hali inayowasumbua watoto pamoja na watu wazima, kiasi kwamba matumizi ya dawa za kikohozi na kifua huongezeka.

Hata hivyo, wataalamu wa afya mara nyingi hawashauri matumizi ya dawa za kikohozi hasa kwa watoto wadogo kutokana na madhara yanayoweza kuwapata, hususan pale dawa hizo zinapotumiwa mfululizo. Wataalamu hao wanaeleza kuwa dawa hizo hazisaidii kutibu chanzo halisi cha tatizo.


Sababu kuzuiwa

Wataalamu wa afya nchini pamoja na mashirika makubwa duniani, ikiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO), wanatahadharisha matumizi ya dawa za kikohozi kwa watoto wadogo wakieleza kuwa dawa hizo si salama na zinaweza kuhatarisha maisha ya watoto, hasa walio chini ya umri wa miaka sita.

Aidha, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema zaidi ya watoto 300 duniani, wengi wao wakiwa chini ya miaka mitano, walifariki kati ya mwaka 2022 na 2023 kutokana na matumizi ya dawa za kikohozi zilizokuwa na kemikali hatari zinazoweza kuharibu figo na kusababisha kifo.

Dawa nyingi za kikohozi zina viambata vinavyoitwa opioid derivatives kama vile codeine, ambavyo hudidimiza mfumo wa upumuaji. Unapompa mtoto mdogo dawa za kikohozi, mara nyingi haisaidii kutibu chanzo cha tatizo kwa sababu kikohozi hicho kinaweza kuwa kimetokana na maambukizi.

Kutokana na maini ya watoto wadogo kutokuwa yamekomaa vizuri, matumizi ya dawa hizo yanaweza kusababisha madhara kama kushindwa kupumua vizuri, usingizi mzito, degedege na hata mapigo ya moyo kwenda kasi.

Aidha, madaktari wanaeleza kuwa kikohozi si ugonjwa wenyewe, bali ni njia ya asili ya mwili kujilinda. Mtoto anapokohoa, mwili wake husaidia kutoa makohozi na uchafu uliopo kwenye njia ya hewa ili aweze kupumua vizuri. Ukizuia kikohozi hicho kwa kutumia dawa zinazokandamiza kikohozi (cough suppressants), unazuia mwili kutoa makohozi hayo, jambo linaloweza kuongeza hatari ya maambukizi kwenye mapafu kama nimonia.

Kwa mfano, dawa zenye codeine au hydrocodone zinaweza kupunguza uwezo wa kupumua, ndiyo maana zimezuiwa kwa watoto katika maeneo mengi kutokana na hatari zake.

Tafiti nyingi za kisayansi pia zimeonyesha kuwa dawa za kikohozi hazisaidii kupunguza kikohozi kwa watoto wadogo zaidi ya jinsi ambavyo mwili ungeweza kupona wenyewe. Mara nyingi kikohozi kinachosababishwa na mafua ya kawaida huisha chenyewe ndani ya wiki moja hadi mbili.

Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Dar Group, Gloriamaria Kunambi, anasema matumizi ya dawa za kikohozi kwa watoto wadogo hayashauriwi kutokana na uwezo mdogo wa mifumo yao ya upumuaji pamoja na maini yao kuchuja sumu.

“Miili ya watoto wadogo bado haijakomaa vizuri kuweza kuchuja na kutoa kemikali za dawa kwa haraka kama ilivyo kwa watu wazima,” anasema Dk Kunambi.

Anaongeza kuwa dawa nyingi za kikohozi huwa na mchanganyiko wa dawa zaidi ya tatu ndani ya moja, zikiwamo dawa za mafua, maumivu na kikohozi.

“Ukimpa mtoto dawa hiyo na wakati huo huo ukawa unampa Paracetamol pembeni, ni rahisi sana kumuingiza kwenye sumu bila kukusudia kutokana na kuzidisha kiwango cha dawa,” anasema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, matumizi ya mara kwa mara ya dawa hizo yanaweza kushusha uwezo wa mtoto kupumua na kuathiri mfumo wa fahamu, jambo ambalo linaweza hata kusababisha kifo.

“Mama anaweza kutumia kijiko cha kawaida cha chakula kumpa mtoto dawa badala ya kifaa maalumu cha kupimia dawa. Hii husababisha watoto wengi kupewa kiwango kikubwa kuliko kinachotakiwa,” anaeleza.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Hospitali ya Epiphany, Faraja Kambona, akizungumza katika kipindi cha Medicounter cha UTV, anasema dawa nyingi za kikohozi huwa na viambata vinavyodidimiza usafirishaji wa taarifa kwenye mfumo wa fahamu wa ubongo, hali inayoweza kuathiri upumuaji wa watoto.

Anasema mara nyingi dawa hizo hushindwa kutibu chanzo halisi cha kikohozi, ndiyo maana madaktari wengi hawashauri matumizi yake kwa watoto wadogo.

“Kitaalamu, dawa hizi hushauriwa zaidi kwa watoto wenye umri wa miaka sita na kuendelea. Lakini hata hivyo, matokeo yake hayaleti tofauti kubwa kwa mtoto kama imemsaidia au haijamsaidia,” anasema Dk Kambona.

Aidha, anashauri matumizi ya asali, tangawizi na maji ya uvuguvugu kwa watoto wenye umri wa zaidi ya miaka miwili, akieleza kuwa vinaweza kusaidia kupunguza tatizo hilo.

“Unakuta mama anatumia dawa moja ya kikohozi, ikiisha akaona haijamsaidia anambadilishia nyingine. Badala ya kumtibu mtoto, anaendelea kumwongezea sumu mwilini wakati maini yake bado hayajakomaa vizuri kuhimili kiwango hicho,” anasema.

Mfamasia Mkuu wa JKCI – Dar Group, Baraka Mosi, anasema tafiti nyingi za kugundua dawa kwa binadamu hufanyika kwa makundi ya watu wazima.

Hivyo taarifa kuhusu ufanyaji kazi wake huwa sio za uhakika na ni vigumu kupata kipimo cha uhalisia kwa ajili ya mtoto. Hivyo mtoto anaweza kupata madhara kwenye matumizi ya dawa.

“Baadhi ya tafiti zinaonyesha hakuna matokeo ya kuridhisha kwa dawa hizo za kikohozi na kifua ukilinganisha na dawa tiba za majaribio isiyokua na kiambato (placebo) sababu matatizo mengi ya kifua husababishwa na virusi hivyo dawa za kikohozi kushindwa kufanya kazi yake,” anaeleza mfamasia huyo.

Kwa mujibu wa jarida la Medical News Today, mashirika kama FDA pamoja na madaktari wa watoto nchini Marekani yamekuwa yakionya dhidi ya matumizi ya dawa nyingi za kikohozi kwa watoto wadogo, hasa walio chini ya umri wa miaka minne hadi sita, isipokuwa kwa ushauri wa daktari.

Tafiti nyingi pia zinaonyesha kuwa dawa za kawaida za kikohozi kwa watoto hazina tofauti kubwa na placebo, yaani dawa isiyo na tiba halisi. Watoto wengi hupona hata bila kutumia dawa hizo.


Ushauri wa madaktari

Badala ya kutumia dawa za kikohozi, madaktari wanashauri mtoto anywe maji mengi, atumie mvuke au humidifier, matone ya chumvi (saline drops) kwa mafua, asali kwa watoto waliozidi mwaka mmoja na kupumzika kiasi cha kutosha.

Kwa watoto waliofikisha umri wa mwaka mmoja na kuendelea, nusu kijiko cha chai cha asali safi kinaweza kusaidia kulainisha koo na kupunguza kikohozi.

Hata hivyo, mtoto aliye chini ya mwaka mmoja hapaswi kupewa asali kwa sababu inaweza kumsababishia ugonjwa hatari wa kupooza misuli unaoitwa Infant Botulism.

 Matone ya maji ya chumvi maalumu ya hospitali, yanaweza kuwekwa puani mwa mtoto,  ili kulainisha makamasi yaliyoganda, kisha kusafishwa.

Mtoto apewe maji ya joto, maziwa ya mama kwa wanaonyonya au supu ya moto ili kusaidia kulainisha koo na makohozi.

Kumkalisha mtoto kwenye bafu lenye mvuke wa maji ya moto kwa dakika 10 hadi 15 au kutumia mashine ya kuongeza unyevu hewani,  kunaweza kusaidia kufungua njia za hewa.

Madaktari pia wanashauri mtoto apelekwe hospitali haraka ikiwa kikohozi kinaambatana na kupumua kwa shida, midomo kuwa ya bluu, homa kali, kifua kubana, kukohoa damu au kikohozi kinachodumu kwa muda mrefu.

Aidha, afya ya mtoto si jambo la kufanya majaribio. Kabla ya kumnunulia mtoto dawa yoyote ya kikohozi, ni muhimu kupata ushauri na maelekezo kutoka kwa daktari wa watoto.

Hata hivyo, mpaka sasa Tanzania haina takwimu rasmi zinazoonyesha idadi ya watoto walioathirika na dawa za kikohozi.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) ilishawahi kutoa tahadhari na kuondoa baadhi ya dawa za watoto sokoni, kutokana na hofu ya uwepo wa kemikali hatari zinazoweza kusababisha madhara makubwa au vifo.