Tanzania miongoni mwa vinara vifo vya malaria; Ripoti
Mbu aenezae Malaria. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Ripoti ya ‘World Malaria Report 2025’ inaonyesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa vifo na maambukizi ya malaria duniani. Licha ya juhudi changamoto kama usugu wa dawa, mabadiliko ya tabianchi na uelewa mdogo wa jamii zinaendelea kuathiri mapambano dhidi ya malaria nchini.
Dar es Salaam. Tanzania imetajwa miongoni mwa nchi nne zinazoongoza kwa idadi ya vifo vinavyotokana na malaria duniani, zikichangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vilivyoripotiwa mwaka 2024, kwa mujibu wa ripoti (World Malaria Report 2025).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya vifo 600,000 vilivyotokea kwa mwaka 2024 Nigeria iliongoza kwa asilimia 30.3 ya vifo vyote, DRC asilimia 11.1, Niger asilimia 5.8 na Tanzania ilikuwa na vifo asilimia 4.3.
Tanzania imeorodheshwa kama nchi yenye maambukizi makubwa barani Afrika, ikichangia takribani asilimia 3.3 ya visa vyote vya malaria duniani na karibu asilimia 4.3 ya vifo vinavyotokana na malaria.
Kwa miaka ya karibuni, nchi ilikuwa miongoni mwa chache (ikiwemo Nigeria na DR Congo) zinazobeba zaidi ya nusu ya vifo vya malaria duniani.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi kwa miaka ya hivi karibuni, ugonjwa huo bado ni tishio kubwa kwa afya ya umma hasa katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Wakati ripoti ikieleza hayo, Aprili 17, 2026 Wizara ya Afya ilisema itaendelea kutumia afua mbalimbali za kukabiliana na malaria ikiwamo teknolojia mpya ya kubadili vinasaba vya mbu wanaoeneza ugonjwa huo, ili kutokuwa na uwezo wa kuueneza (Gen drive).
Ripoti hiyo inaonyesha takribani asilimia 93 ya Watanzania wanaishi katika maeneo yenye maambukizi ya malaria. Mwaka 2023 kulikuwa na karibu visa milioni 3.8 na vifo zaidi ya 25,000 vinavyohusishwa na malaria nchini.
Pia. inaonyesha watoto chini ya miaka mitano ndio wanaoathirika zaidi, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika.
Ripoti inaonyesha kuwa Afrika inachangia zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi yote na vifo vya malaria duniani, nchi 11 za Afrika zinabeba karibu theluthi mbili ya mzigo wote wa malaria duniani, na Tanzania iko kwenye kundi hili la mzigo mkubwa.
Imeonyesha changamoto mpya zinazotishia mafanikio kwa Tanzania ikiwemo, usugu wa dawa za malaria unaoongezeka, usugu wa viuatilifu kwa mbu unaopunguza ufanisi wa vyandarua, mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa mbu wapya mijini pamoja na upungufu wa fedha za kudhibiti malaria.
Hatua zinazochukuliwa
Katika hatua zinazochukuliwa, zinazoigusa pia Tanzania katika ripoti inaonyesha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinaanza kutumia vyandarua vipya vinavyofanya kazi zaidi dhidi ya mbu sugu, chanjo za malaria ambazo zimeanza kuingizwa katika programu za chanjo na upanuzi wa tiba kinga kwa watoto.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mwanasayansi Kiongozi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) na Naibu Mkuu wa Idara ya Afya ya Mazingira na Sayansi za Ikolojia (EHES), Brian Tarimo amesema hali ya malaria duniani imeonyesha ongezeko la wagonjwa na vifo, ambapo kwa Tanzania kulikuwa na vifo 26,000 kwa mwaka 2024.
Amesema ongezeko hilo linachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo mbu na vimelea vya malaria kuanza kuonesha usugu dhidi ya dawa na hata vipimo vya ugonjwa huo.
Amesema hali hiyo inasababisha wagonjwa kushindwa kugundulika mapema, jambo linalochelewesha matibabu sahihi.
“Kuna wagonjwa wanaenda hospitali, lakini vipimo haviwezi kuonesha maambukizi, hivyo inakuwa changamoto kujua namna ya kumtibu,” amesema.
Aidha, amesema majanga kama vita na mafuriko yamekuwa yakikwamisha usambazaji wa vyandarua na dawa, huku mabadiliko ya tabianchi yakichochea mazalia ya mbu kutokana na ongezeko la joto.
Ameongeza kuwa kupungua kwa ufadhili wa kimataifa pia kumeathiri mapambano dhidi ya malaria, akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia vyandarua vyenye dawa, kumaliza dozi na kuchukua tahadhari binafsi ili kudhibiti ugonjwa huo.
Hatua hizi zinakwenda sambamba na msisitizo wa viongozi wa kitaifa, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akihimiza uwekezaji zaidi katika tafiti za ndani na matumizi ya sayansi katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kupunguza na hatimaye kutokomeza malaria nchini Tanzania, bado kuna changamoto nyingi zinazoendelea kukwamisha mapambano hayo.
Mazingira mengi, hasa maeneo yenye maji yaliyotuama na mifereji isiyotunzwa vizuri, yanaendelea kutoa fursa kwa mbu kuzaliana kwa wingi, ikiwemo maeneo ya mijini.
Akizungumzia hali hiyo, Mtaalamu wa Sosholojia ya Afya katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Mwanza, na Ofisa wa Ushirikishwaji wa Wadau katika Transmission Zero, Justina Mosha, amesema pamoja na uwepo wa mikakati kama ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu, bado matumizi yake hayaridhishi.
Amebainisha kuwa baadhi ya wananchi wanadharau matumizi ya vyandarua, huku wengine wakiwa na imani potofu kwamba kutumia chandarua kunaweza kupunguza nguvu za kiume.
“Wapo wanaotumia lakini si kwa usahihi. Mfano, mtu analala chini ya chandarua lakini hakifungi vizuri au anakiacha kikiwa kimeshushwa muda wote bila kukitunza, hali inayopunguza ufanisi wake,” anasema.
Justina ameongeza kuwa hata kwa wale wanaotumia vyandarua ipasavyo, bado kuna changamoto kutokana na mabadiliko ya tabia za mbu.
Tofauti na zamani ambapo mbu wengi walikuwa wanauma usiku, sasa baadhi yao wanaweza kung’ata muda wowote, hata kabla mtu hajaingia kulala. Hali hii inawaweka hatarini watu wanaokaa nje usiku kwa muda mrefu.
Pia, ametaja kuchelewa kwa wananchi kutafuta matibabu kuwa ni tatizo jingine kubwa. Wengi wanapopata dalili za malaria hudhani ni homa ya kawaida na kuchelewa kwenda hospitali, jambo linalosababisha kuenea kwa maambukizi kwa watu wengine wa karibu.
Kwa upande wa kisayansi, Justina ameeleza kuwepo kwa changamoto ya usugu wa dawa na viuatilifu.
“Baadhi ya mbu wameanza kuonyesha usugu dhidi ya viuatilifu vinavyotumika, na pia vimelea vya malaria vinaonyesha usugu dhidi ya baadhi ya dawa. Hii inafanya maambukizi kujirudia mara kwa mara.”
Aidha, ukosefu wa elimu kwa jamii kuhusu namna sahihi ya kujikinga na kutibu malaria unaendelea kuwa kikwazo. Sababu za kiuchumi pia zinachangia, ambapo baadhi ya wananchi wanashindwa kumudu gharama za kujikinga au kupata matibabu kwa wakati.
Hata hivyo, Justina amesisitiza kuwa pamoja na juhudi za kisayansi zinazoendelea, ushirikiano wa jamii ni muhimu zaidi.
Ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua binafsi kama kuhakikisha mazingira yao ni safi, kuondoa maji yaliyotuama, kutumia vyandarua ipasavyo, na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
“Mapambano dhidi ya malaria hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa jamii. Tunahitaji kuongeza nguvu kwa pamoja Serikali, wanasayansi na wananchi ili kufikia lengo la kutokomeza malaria,” amesisitiza.
Changamoto kubwa imekuwa ni matumizi yasiyo endelevu ya njia hizi pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu namna sahihi ya kujikinga.
Mosha, amesema kuwa watu wengi wana mtazamo potofu kuhusu kinga ya malaria, “Ukweli ni kwamba malaria ni ugonjwa unaoweza kujirudia mara nyingi. Kinga yake inahitaji jitihada za pamoja na matumizi ya mbinu mbalimbali kwa wakati mmoja na kwa usahihi.”