Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tiba ya malaria kwa watoto wachanga yapatikana

Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Dawa hiyo iitwayo Artemether-lumefantrine imeelezwa kuwa ya kwanza kutengenezwa mahsusi kwa ajili ya watoto wachanga wenye uzito wa chini ya kilo tano, kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa katika hatari kubwa kutokana na kukosa dawa sahihi za matibabu ya malaria.

Dar es Salaam. Hatua ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuidhinisha kwa mara ya kwanza dawa maalumu ya kutibu malaria kwa watoto wachanga imeibua matumaini mapya katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari, huku wataalamu wa afya wakisisitiza mafanikio hayo yatategemea zaidi upatikanaji wake kwa wakati na matumizi sahihi katika jamii.

Dawa hiyo iitwayo Artemether-lumefantrine imeelezwa kuwa ya kwanza kutengenezwa mahsusi kwa ajili ya watoto wachanga wenye uzito wa chini ya kilo tano, kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa katika hatari kubwa kutokana na kukosa dawa sahihi za matibabu ya malaria.

Kwa mujibu wa WHO, kibali kilichotolewa kinaonesha dawa hiyo imekidhi viwango vya kimataifa vya ubora, usalama na uwezo wa kutibu malaria, hatua inayotarajiwa kuziba pengo la muda mrefu katika huduma za afya kwa watoto wachanga.

Hadi sasa, watoto wa kundi hilo walikuwa wakitibiwa kwa kutumia dawa zilizokusudiwa kwa watoto wakubwa zaidi, hali ambayo mara nyingi ilihusisha hatari ya kupatiwa dozi isiyo sahihi na kupelekea madhara, ikiwemo sumu mwilini au kushindwa kupata nafuu ipasavyo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kwa muda mrefu malaria imekuwa ikichukua maisha ya watoto wachanga na kuathiri familia na jamii, lakini sasa dunia inaanza kuona mabadiliko ya kweli katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

“Kwa karne nyingi, malaria imechukua uhai wa watoto na kuathiri matumaini ya familia nyingi. Lakini sasa tunaona mwelekeo mpya kupitia chanjo, vipimo vya kisasa na dawa bora zaidi,” amesema Tedros.

Ameongeza kuwa kutokomeza malaria si ndoto tena, bali ni lengo linalowezekana iwapo kutakuwa na utashi wa kisiasa na uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya.

Kwa upande wa wataalamu wa afya nchini Tanzania, hatua hiyo imeelezwa kuwa ni muhimu, lakini haitoshi bila kuhakikisha dawa hiyo inawafikia walengwa kwa haraka, hasa katika maeneo ya vijijini ambako malaria imeendelea kuwa tishio kubwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, Dk Latifa Msuya, amesema dawa hiyo inaweza kuleta mapinduzi makubwa katika kupunguza vifo vya watoto wachanga, lakini utekelezaji wake unahitaji maandalizi ya kina.

“Watoto wachanga ni kundi nyeti sana. Kwa muda mrefu tumekuwa tukilazimika kutumia dawa za watoto wakubwa, jambo ambalo si salama kwa asilimia zote. Hii dawa mpya ni hatua kubwa, lakini ni lazima tuhakikishe inapatikana katika vituo vyote vya afya,” amesema Dk Msuya.

Ameongeza kuwa, pamoja na dawa, ni muhimu kuimarisha huduma za uchunguzi wa mapema ili watoto wachanga waweze kugunduliwa mapema na kuanza matibabu haraka.


Tutaweza kuisambaza?

Mtaalamu wa afya ya jamii na magonjwa ya mlipuko, Dk John Mallya, amesema changamoto kubwa inayoweza kuathiri mafanikio ya dawa hiyo ni mifumo dhaifu ya usambazaji wa dawa katika nchi nyingi za Afrika.

“WHO imeshaeleza wazi kuwa zaidi ya asilimia 70 ya nchi duniani hazina mifumo madhubuti ya usimamizi wa dawa, chanjo na vifaa tiba. Hii ina maana hata kama dawa ipo, inaweza isiwafikie wanaohitaji,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwekeza zaidi katika miundombinu ya afya, mafunzo kwa wahudumu na ufuatiliaji wa matumizi ya dawa ili kuhakikisha hakuna upotevu au matumizi mabaya.

Takwimu za WHO zinaonesha mwaka 2024 kulikuwa na takribani wagonjwa milioni 282 wa malaria duniani, huku zaidi ya watu 610,000 wakipoteza maisha katika nchi 80.

Afrika inaongoza kwa kubeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo kwa asilimia 95 ya wagonjwa na vifo vyote.

Watoto walio chini ya miaka mitano ndio wanaathirika zaidi, wakichangia robo tatu ya vifo vyote vinavyotokana na malaria, hali inayofanya ugunduzi wa dawa kwa watoto wachanga kuwa hatua muhimu katika kupunguza vifo hivyo.

Dk Mallya amesema licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazoendelea kuathiri mapambano dhidi ya malaria, ikiwemo usugu wa dawa, kupungua kwa misaada ya kimataifa na ukosefu wa vipimo vya uhakika katika baadhi ya maeneo.

“Hatuwezi kuangalia dawa pekee. Mapambano dhidi ya malaria yanahitaji mkakati wa pamoja unaojumuisha kinga, uchunguzi na matibabu,” amesema.


‘Inaweza kuwa mkombozi’

Naye mkunga wa Kituo cha Afya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Neema Lwoga, amesema dawa hiyo mpya inaweza kuwa mkombozi kwa kina mama na watoto wachanga, hasa katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya malaria.

“Mara nyingi watoto wachanga wanapougua malaria hali yao huwa mbaya haraka. Kupata dawa maalumu kwao kutasaidia kuokoa maisha mengi,” amesema Neema.

WHO imesema ithibati ya dawa hiyo itaiwezesha sekta ya umma kununua na kuisambaza kwa wingi, hatua inayotarajiwa kuwafikia takribani watoto milioni 30 wanaozaliwa kila mwaka katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya malaria barani Afrika.

Hata hivyo, wataalamu wamesisitiza mafanikio ya dawa hiyo yatategemea pia elimu kwa jamii kuhusu dalili za malaria kwa watoto wachanga, pamoja na kuondoa dhana potofu zinazoweza kuchelewesha matibabu.

Aidha, juhudi za kinga kama matumizi ya vyandarua vyenye dawa, usafi wa mazingira na kudhibiti mazalia ya mbu zinaendelea kutajwa kuwa nguzo muhimu katika kupambana na malaria.


Hili linakuja katika kipindi ambacho takwimu mpya za malaria nchini zinaonesha mwanga katika vita dhidi ya ugonjwa huo, baada ya vifo na maambukizi kupungua kwa kiwango kikubwa ndani ya miaka mitano iliyopita.


Takwimu za vifo

Kwa mujibu wa tamko la Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, lililotolewa jana Jumamosi, Aprili 25, 2026, idadi ya vifo vinavyotokana na malaria imepungua kwa asilimia 50, kutoka vifo 2,460 mwaka 2020 hadi kufikia vifo 1,231 mwaka 2025.

Wakati huo huo, maambukizi katika jamii yameshuka kwa takribani asilimia 30, kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025.

Mbali na hilo, wagonjwa wanaothibitika kuwa na malaria katika vituo vya afya wamepungua kwa zaidi ya nusu, kutoka watu milioni 6 mwaka 2020 hadi milioni 2.8 mwaka 2025.

Idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini kutokana na malaria nayo imepungua kwa asilimia 35 katika kipindi hicho.