Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tobo: Operesheni mpya inasaidia kupunguza ukubwa wa kidonda

“Kamera maalumu iliyounganishwa na video husaidia kukuza maradufu picha za viungo vya ndani. Pia kamera hii huunganishwa na taa yenye mwanga mkali ili kumulika tumboni. Hata hivyo kwa uchunguzi wa kawaida tundu moja hutosha, lakini  kwa matibabu kufanyika tundu zaidi ya moja huhitajika,” Dk Muganyizi Kairuki

Muktasari:

  • Hii ni aina ya kisasa ya upasuaji ambayo imeanza kutumika nchini ikiwa na faida nyingi kama vile kumpunguzia mgonjwa maumivu, kupona ndani ya siku mbili na kusaidia kubaini tatizo lililoshindikana kwa vipimo vya CT scan au utrasound.

Operesheni mpya inayotumia njia ya kutoboa badala ya kupasua sasa umeanza kuzoeleka katika hospitali kubwa tatu nchini.

Aina hii ya operesheni maarufu kama laparoscopia haisababishi vidonda au kovu kubwa kwenye mwili wa mgonjwa.

Oparesheni hiyo mara nyingi hutumika kwa watu wenye tatizo tumboni kwa kutoboa tumbo na kuingiza kifaa kidogo chenye kamera ya video ambayo huchukua picha na kuzionyesha kwenye kompyuta.

Kupitia kompyuta, mtaalamu wa afya huweza kugundua tatizo kwenye tumbo la mgonjwa.

Upasuaji wa kawaida wa tumbo huweza kupasua urefu wa sentimita tano au zaidi ili kupata eneo kubwa la kuona ndani ya tumbo.

Katika upasuaji huu mpya ambao katika miaka ya karibuni umekuwa ukitumika sana katika nchi za magharibi na Asia, tobo la kati ya nusu sentimita mpaka sentimita moja na nusu, huweza kutumika.

Hili ni tobo lenye nafasi sawa na ya kupitisha kidole ukilinganisha na operesheni zilizozoeleka zinazopasua ukubwa wa kupitisha hadi viganja viwili kutoa nafasi ya kuona vizuri ndani. Kwa hapa nchini, operesheni hii ya kisasa imeanza  kutolewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Kairuki na KCMC.

Daktari bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Kairuki, Muganyizi Kairuki anasema upasuaji huu ni mgeni kiasi kwa wataalamu wengi bingwa nchini.

Anasema japokuwa umekuwepo kwa takribani miaka 20 iliyopita, umekuwa wa kusuasua kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vifaa, mafunzo na uchache wa wataalam.

“Lakini hivi sasa upasuaji huu umeanza kufanyika na wataalamu wa kizazi cha sasa,” anasema Dk Kairuki akifafanua:

“Hospitali ya Kairuki tulishawahi kufanya upasuaji wa aina hii miaka 15 iliyopita, lakini kutokana na sababu mbalimbali tulisitisha na sasa tumeanza tena.

“Tunachokifanya sasa ni kutengeneza timu ya madaktari kadhaa ambao watakuwa mabingwa wa upasuaji huu.”

Kuhusu uzoefu wake katika utabibu huo, Dk Kairuki anasema: “Mpaka sasa nimeshawahi kufanya upasuaji kwa njia ya matobo kwa wagonjwa zaidi ya 1000 nchini Afrika Kusini na kwa hapa nchini tangu tumeanza nimewafanyia kwa wagonjwa zaidi ya 80 na leo tunavyozungumza nina ratiba ya watu wawili.”

Anasema operesheni hiyo inaweza kukamilisha kazi yake ndani ya dakika 15 hadi 50.

Operesheni ya tobo

Anasema  wakati upasuaji mara nyingi  matundu kuanzia moja mpaka matano kutegemeana na aina ya upasuaji.

Operesheni hiyo anasema hufanyika ndani ya tumbo lakini unaweza kufanyika pia kifuani lengo likiwa ni kuchunguza ndani.

Dk Kairuki anasema upasuaji kwa njia ya matobo hufanywa kwa kutumia vifaa vyenye gharama kubwa ikiwa ni pamoja na vifaa maalumu kama vile mkasi mrefu, sindano na kamera.

Anasema kwa kutumia kompyuta huweza kukuza picha ya kile kitu wanachokitibu tumboni na kukiona kwa ukubwa unaowezesha kazi yao kufanyika kwa umakini zaidi.

Pamoja na vifaa hivyo, anasema wakati wa upasuaji kunatakiwa kuwepo na mtambo wa kufyonza maji au damu na kuosha tumbo.

Anasema mtambo huo pia huandamana na taa yenye mwanga mzuri kuwezesha kuona ndani vizuri, lenzi maalum yenye uwezo wa kukuza picha na mtambo wa kujaza gesi ukaa (carbon dioxide) ili kutunisha tumbo wakati wa upasuaji.

Upasuaji unavyofanyika

Dk Kairuki anasema jopo la madaktari na wauguzi wasiopungua wanne, huhitajika ili kurahisisha upasuaji huu.

Mgonjwa hulazwa kwa kupewa dawa za usingizi kama  ilivyo katika upasuaji wa kawaida.

“Kazi inayofuatia huwa ni usafishaji wa tumbo. Tumbo husafishwa kama kawaida kuua vijidudu, kisha matundu madogo hutobolewa kwenye ngozi kisha gesi ya carbon dioxide huingizwa tumboni ili kulitanua na kuongeza nafasi ndani ya tumbo mithili ya puto kwa ajili ya kurahisisha upasuaji,” anasema na kuongeza:

“Kamera maalum iliyounganishwa na video husaidia kukuza picha za viungo vya ndani maradufu. Pia kamera hii huunganishwa na taa yenye mwanga mkali ili kumulika tumboni, hata hivyo kwa uchunguzi wa kawaida tundu moja hutosha, lakini  kwa matibabu kufanyika tundu zaidi ya moja huhitajika.

“Vifaa mbalimbali maalumu kwa upasuaji huo, hutumika kuondoa tatizo lililopo tumboni, mfano mikasi mirefu na myembamba,” anasema.

Manufaa yake

Kwa mujibu wa Dk Kairuki upasuaji wa matobo hupunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa damu ukilinganisha na upasuaji wa kawaida hivyo kupunguza mahitaji ya kuongezewa damu.

“Haupotezi damu nyingi na pia uzuri au umaridadi wa mtu kubaki kama zamani kwa kuondokana na makovu makubwa yanayochukiza.

“Pia hupunguza kwa kiwango kikubwa maumivu yanayotokana na upasuaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kupona kwa haraka sana kwa jumla ukilinganisha na upasuaji wa kawaida, ambapo mwili huhitaji muda mrefu zaidi kurudia katika hali ya kawaida.

“Mgonjwa hupona kwa siku mbili, huku oparesheni ya kawaida hupona baada ya siku 10, hivyo kupunguza muda wa kulazwa hospitalini na gharama kupungua,” anasema Kairuki.

Anasema upasuaji huo hupunguza athari  za vidonda kupata maambukizi, kupunguza mwili uzito wa kutoa vimeng’enyo inasaidia uponaji, pia picha za viungo vya ndani kuonekana vizuri, husaidia kugundua tatizo haraka zaidi.

Anasema pia hii ni njia nzuri kwa wanafunzi wa udaktari katika viwango mbalimbali kuona kwa halisi viungo vinavyofanana wakati wa upasuaji.

Changamoto

Dk Kairuki anasema upasuaji kwa njia ya matobo una changamoto zake kama ilivyo kwa njia ya kawaida.

Anasema huu ni wa gharama kubwa ukilinganisha na wa kawaida kwa sababu ya vifaa na mafunzo yake.

Hata hivyo Dk Kairuki anasema kuna hatari katika upasuaji wa aina hii kama ilivyo kwa njia ya kawaida kama vile kutoboa viungo vya ndani, mfano utumbo mpana au mwembamba hasa mwanzoni wakati daktari akijaribu kutoboa tumbo kuweka gesi ya CO2.

Tatizo lingine anasema ni kuumiza mishipa ya damu kwa kiasi fulani na kwamba ni hatari kwa wagonjwa wembamba waliowahi kufanyiwa upasuaji wa awali.

Anasema wagonjwa hawatastahili kufanyiwa upasuaji wa aina hii iwapo hakutakuwa na mjuzi wa upasuaji wa aina hiyo.

Vitu vingine vinavyoweza kuzuia upasuaji wa aina hii ni kutokuwepo kwa vifaa kamili kwa upasuaji, mgonjwa mwenye shinikizo la damu, mgandamizo kubwa ndani ya fuvu ama ubongo, matatizo ya mapafu, mwenye mimba kubwa au uvimbe mkubwa.

Wanaofaa kwa matobo

Dk Kairuki anasema upasuaji wa aina hii ni mashuhuri kwa watu wazima zaid kuliko watoto.

Anasema watoto wadogo ni nadra kufanyika kutokana na mashaka ya kitaalamu na manufaa watakayopata.

Pamoja na malumbano hayo ya kitaalamu aina hii ya operesheni imeonekana ni nzuri kufanyi mtoto iwapo ana tatizo la kidole tumbo.

Anasema kuwa aina hiyo ya operesheni imekuwa ikisaidia

Kuondoa tatizo ambalo limeshindikana kuonekana kwa mashine za uchunguzi CT scan au ultrasound, mfano saratani  za tumbo au kongosho.

Anasema pia njia hiyo huweza kutumika ili kuchunguza  kiwango cha usambaaji wa ugonjwa mwilini hasa tumboni.

Anasema njia hii ya operesheni pia hutumika katika upasuaji wa kuondoa mawe katika mfuko wa nyongo, kuondoa kidole tumbo, kutibu ngiri; hasa ile  iliowahi kupasuliwa na ikajirudia, kurekebisha ngiri zinazojitokeza mara baada ya upasuaji wa mwanzo, na kushona tumbo lililopasuka kutokana na vidonda  vya  tumbo.

Anasema upasuaji huo pia hufanyika kwa kuondoa bandama yenye ugonjwa, kusaidia katika upasuaji wa utumbo mdogo na mkubwa, kuachanisha utumbo uliyoganda mara baada ya upasuaji wa mwanzo na kuondoa tumbo la uzazi.

Faida nyingine anasema ni kuondoa uvimbe mbalimbali katika viungo vya uzazi vya wanawake, ushonaji wa viungo mbalimbali vilivyochanika kutokana na na ajali na pia upasuaji wa tumbo kupunguza uzito uliokithiri.

Historia yake

Upasuaji wa aina hii ulianza kufanyika katika Bara la Ulaya katika miaka ya 1902 ambapo walianza kwa kupasua wanyama kama mbwa.

Mwaka 1910 upasuaji wa binadamu ulifanyika. Toka miaka Hiyo mpaka sasa vifaa Vingi vya upasuaji huu vimegunduliwa na watafiti mbalimbali  katika kuboresha aina hii ya operesheni.

Aina hii ya operesheni ilianza kutumika miaka ya 1990, hasa katika uchunguzi wa magonjwa ya kinamama.

Kwa sasa magonjwa mengi ndani ya tumbo yanaweza kutibiwa kwa njia hii.

Barani Afrika, ni nchi chache zimeanza kutumia njia hii ya operesheni ukilinganisha na zile za Magharibi na Asia.