Tumia tangawizi badala ya chai

Muktasari:

  • Tofauti na vyakula vingine kama kitunguu swaumu, tangawizi husaidia kutengeneza harufu nzuri na pia husaidia msukumo wa damu mwilini kwa sababu huupa mwili joto ambalo mara nyingi mwili huhitaji.

Tangaziwi ni kiungo kinachotumika kwenye chakula, lakini pia kwenye chai. 

Pia tangawizi inaweza kuwa ni dawa au kinga ya maradhi mbalimbali kwa wagonjwa wa kisukari, kwani husaidia kuweka sawa kiwango cha sukari kwenye damu.

Kutokana na hilo, wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kutumia tangawizi badala ya chai.

Pindi sukari ikiwa juu hufanya kinywa kuwa na harufu mbaya, tangawizi huondoa changamoto hiyo.

Tofauti na vyakula vingine kama kitunguu swaumu, tangawizi husaidia kutengeneza harufu nzuri na pia husaidia msukumo wa damu mwilini kwa sababu huupa mwili joto ambalo mara nyingi mwili huhitaji wakati wa usukumwaji wa damu mwilini.

Wagonjwa wengi wa kisukari wanapata changamoto ya kukosa hamu ya kula, lakini matumizi ya tangawizi huongeza hamu ya kula chakula.

Kwa wale wenye mfumo mbaya wa umeng’enyaji wa chakula wanashauriwa kutumia tangawizi, ili kupata mfumo mzuri wa mmeng’enyo wa chakula.

Kuna wagonjwa wa kisukari wanaopata kiungulia au kuchefuchefu pindi sukari inapokuwa juu, hivyo wanaweza kutumia tangawizi kuondokana na hali hiyo.

Kunywa maji ya moto ya tangawizi pia hutuliza kidonda cha koo kutokana na mkusanyiko wa kamasi.

Pia husaidia kupunguza magonjwa ya asubuhi kama uchovu na mning’inio. Kwa wajawazito, tangawizi huwapunguzia homa za asubuhi.

Tangawizi ina vitamini A, C, E, B-complex, chuma, zinki, magnesium, phosphorus, sodium, calcium, na beta-carotene. Pia ina madini ya manganese ambayo ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Hutibu homa ya kichwa, maumivu ya tumbo wakati wa hedhi, hupunguza homa ya baridi yabisi, huimarisha afya ya figo, hulinda kuta za moyo, mishipa ya damu na mishipa ambayo mkojo hupita.

Angalizo kwa wagonjwa wa kisukari, tangawizi si tiba ya kisukari isipokuwa inasaidia kuukinga mwili na dhidi ya maradhi mbalimbali, hivyo msiache dawa au sindano za insulin bila mwongozo wa daktari wako.