Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Udumavu ulivyoacha makovu ndani ya jamii -2

Muktasari:

  • Ufuatiliaji wa kina wa ukuaji wa watoto, elimu ya lishe na msaada wa kijamii unahitajika katika kukabiliana na udumavu.

Iringa. “Nilikuwa nimemshika mtoto, nikahisi moyo wangu haufanyi kazi. Daktari akaniambia uzito wake ni mdogo kulinganisha na umri wake. Sikuwahi kupata taarifa kuhusu tatizo hilo hapo awali.”

Ni simulizi ya mama anayekumbuka siku aliyompeleka mtoto wake wa kike wa miezi tisa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, baada ya usiku wa hofu kutokana na mtoto kuugua mafua makali, kupumua kwa shida na kushindwa kunyonya.

“Daktari aliuliza uzito wa mtoto, nikajibu: ‘Kilo sita na nusu.’ Daktari akasema ni mdogo kwa mtoto wa umri huu. Nilihisi hofu na kujiuliza ni wapi nilipokosea,” anasema Devotha Sebastian, akiwa katika Manispaa ya Iringa.

Kwa umri huo, uzito wa chini unaokubalika kwa mtoto wa kiume ni kilo 7.1 na wa juu ni kilo 11, huku kwa mtoto wa kike uzito wa chini ni kilo 6.5 na wa juu ni kilo 10.5.

“Baada ya vipimo vya maabara, nilielekezwa kwenda kuonana na mtaalamu wa lishe. Daktari alinieleza mtoto hakuwa na maambukizo yoyote isipokuwa alikuwa na utapiamlo wa kiwango cha kati,” anasema Sebastian, ambaye kwa sasa anaishi jijini Dar es Salaam.

“Alimpima na kunifafanulia chati ya ukuaji. Hapo ndipo nilipogundua kuwa udumavu si jambo linaloweza kubainika kwa kumtazama mtoto kwa macho,” anasema.

Anasema aliandikiwa kupata vitamini na kupewa ushauri wa kuboresha lishe, ikiwamo matunda na milo ya kila siku. Vilevile alipangiwa tarehe ya kurudi kliniki ya lishe kwa ajili ya ufuatiliaji.

“Ilikuwa mara ya kwanza kuelezwa kuhusu ukuaji wa mtoto kwa usahihi. Kabla ya hapo, ziara za kliniki zilihusisha chanjo au magonjwa pekee. Sikujua kuwa ukuaji unapaswa kufuatiliwa kwa karibu,” anasema Sebastian, mzaliwa wa Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa, ambaye alihamia Dar es Salaam baada ya kuolewa.

“Ulikuwa uzazi wangu wa kwanza, hivyo nilihitaji mwongozo. Nilitamani kuendelea na kliniki ya lishe, kwani ukuaji wa mtoto si jambo la kubahatisha, ni lazima lifuatiliwe,” anasema.

Simulizi ya Sebastian inatokana na uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Manispaa ya Iringa, Wilaya ya Kilolo na Iringa Vijijini kati ya Oktoba na Desemba 2025.

Katika uchunguzi huo, imebainika kuwa lishe si sababu pekee ya utapiamlo unaohusisha udumavu, kukonda na uzito mdogo, bali kuwalea watoto katika maeneo ya kazi na kuwapa vileo walio chini ya umri wa miaka mitano kumechangia kuwapo kwa kiwango kikubwa cha udumavu miongoni mwao mkoani Iringa.

Wakati kiwango cha udumavu nchini Tanzania kikiwa juu ya wastani wa dunia wa asilimia 22, Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa yenye viwango vya juu zaidi, ukiwa na asilimia 56.9, licha ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula nchini. Wastani wa kitaifa ni asilimia 30.

Takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS) zinaonesha kuwa udumavu unaathiri asilimia 56.9 ya watoto chini ya miaka mitano mkoani Iringa, ukifuatiwa na Njombe kwa asilimia 50.4 na Rukwa asilimia 49.8. Kati ya watoto waliodumaa Iringa, asilimia 17.3 wameainishwa kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu.


Simulizi ya Tweve

Enock Tweve, ambaye sasa ana miaka minne, alimpoteza mama yake kwa ugonjwa akiwa na miezi minne.

Hakupata malezi ya wazazi, hivyo bibi yake, mkazi wa Ilula wilayani Kilolo, Salome Mlula, alimchukua na baadaye alihamia mjini Iringa kutafuta msaada.

Machi 2023, Enock akiwa na miezi 11, hali yake kiafya ilizorota zaidi na akaandikishwa katika mpango wa lishe wa Shirika la Call Africa.

Uzito wake ulikuwa kilo 4.1, mzunguko wa mkono wa eneo la juu (MUAC) ulikuwa sentimita 10.1 (eneo jekundu) na urefu sentimita 59.1, akiwa na viashiria vya wazi vya utapiamlo mkali.

“Hakuwa akinyonya, alikuwa dhaifu muda wote. Nilijua kuna tatizo kubwa sana,” anasimulia Mlula akizungumza na Mwananchi.

Mhudumu wa afya ya jamii katika Mtaa wa Frelimo, Manispaa ya Iringa, ndiye aliyemwelekeza Mlula kwenda Call Africa, ambako alipata elimu ya lishe, ufuatiliaji wa kitabibu na msaada wa kiuchumi. Alisaidiwa katika ufugaji ili kuongeza upatikanaji wa chakula katika kaya.

Anasema alipofikisha umri wa miaka miwili, Enock alionesha kupona kwa kiwango kikubwa, uzito ukiongezeka na kufikia kilo 9.7, MUAC sentimita 13.3 (eneo la kijani) na urefu kufikia sentimita 75.1.

“Hawakumtibu mtoto pekee, walinifundisha pia jinsi ya kumtunza. Msaada huo uliokoa sana maisha yake,” anasema.

Katika Mtaa wa Mkimbizi Shule, Manispaa ya Iringa, Edister Mbimbi anazungumzia changamoto ya kulea wajukuu wake pacha wakati wazazi wao wakiwa kwenye majukumu ya kikazi.

“Wakati fulani pacha walibaki na uzito uleule kwa takribani miezi 10. Nilihama kutoka kliniki moja hadi nyingine kwa sababu niliogopa wauguzi wangenisema vibaya kutokana na watoto kutoongeza uzito,” anasema.

Anaeleza kuna wakati alimwomba mume wake awapeleke watoto kliniki, akiamini asingelaumiwa.

“Kwa bahati nzuri, mwezi huo uzito wao ulikuwa umeongezeka,” anasema, huku akiongeza kuwa alihisi kuna jambo halikuwa sawa.

“Daktari alituambia kila kitu kiko sawa, lakini mjukuu wangu wa kiume alikuwa mdogo sana kulinganisha na dada yake pacha. Tofauti ilikuwa kwamba huyu wa kiume hakupenda kula,” anasema.

Ili kukabiliana na hali hiyo, anasema alibadilisha lishe nyumbani.

“Nilikuwa nikisaga samaki na nyama ili iwe rahisi kwake kula, nikaongeza mayai kwenye uji wa mahindi, na kusaga mboga pamoja na matunda ili kutengeneza juisi. Taratibu alianza kupata hamu ya kula na ukuaji ukaongezeka,” anasema.

Kwa anachoeleza Mbimbi, changamoto za ukuaji wa watoto zinaweza kubaki siri hata pale wanapokuwa ndani ya viwango vya kawaida vya kitabibu, hususan ufuatiliaji unapokuwa hafifu na walezi wanapoogopa lawama badala ya msaada.

Mbimbi anasisitiza kuwa elimu ni muhimu badala ya vitisho, akisema: “Kinamama wanahitaji mwongozo wa nini wafanye tofauti, si kusemwa. Haitaboresha hali ya mtoto, huleta hofu na mkanganyiko zaidi.”


Uzito, onyo la kwanza

Wataalamu wa tiba wanaeleza kuwa utambuzi wa mapema wa tatizo la ukuaji mara nyingi huanzia kliniki.

Daktari wa watoto katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Joseph, Peramiho mkoani Ruvuma, Jida Said, anasema ingawa udumavu hupimwa kwa urefu kulingana na umri, uzito wa mtoto mara nyingi huwa kiashiria cha kwanza cha matatizo ya ukuaji na lishe.

“Kliniki tunatumia kadi ya afya ya mtoto inayorekodi uzito dhidi ya umri,” anaeleza na kuongeza:

“Chati ina maeneo matatu makuu: kijani, kinachoashiria uzito mzuri; kijivu, kinachoonesha uzito usioridhisha; na nyekundu, ambayo huashiria hali hatarishi.”

Dk Said anasema kadi ya mtoto inapokuwa katika eneo jekundu mara nyingi hulazwa pamoja na mama yake kwa uangalizi wa karibu wa kitabibu na lishe, huku vipimo zaidi au rufaa zikifanyika inapobidi.

“Pia inawezekana mtoto kuwa na uzito unaoonekana sahihi lakini urefu usioendana na umri wake. Ndiyo maana uzito pekee hautoshi kuthibitisha uwepo wa udumavu kwa mtoto,” anasema.

Anasisitiza kuwa ni jukumu la wazazi kutambua dalili za awali.

“Iwapo mzazi au mhudumu wa afya atahisi kuna tatizo, vipimo vya ziada hufanyika ili kuelewa chanzo chake,” amesema.

Hata hivyo, anakiri kuwapo kwa changamoto za kimfumo akisema: “Kwa kuzingatia namna kliniki zinavyoendeshwa na idadi kubwa ya watoto wanaohudumiwa kwa siku, si rahisi kupima uzito na urefu kila mtoto anapotembelea. Ndiyo maana kina mama hufundishwa dalili hatarishi na kushauriwa kurejea mara moja wanapoona mabadiliko.”

Programu za ufikiaji wa jamii, kama za Songea mkoani Ruvuma, anasema zimethibitika kuwa na ufanisi katika kuwafikia kina mama wanaokosa kuhudhuria kliniki na kuhakikisha watoto hawapotei katika mifumo.

Dk Said anasisitiza umuhimu wa huduma yenye heshima akisema: “Watoa huduma za afya lazima waeleze taratibu kwa uwazi na waepuke kuwakaripia kina mama, kwa sababu ukali huwafanya waogope kuhudhuria kliniki.”


Ugunduzi wa mapema

Kama alivyosimulia Sebastian, kinamama wengi hugundua matatizo ya ukuaji wanapotembelea kliniki kwa sababu nyingine, kama vile chanjo au matibabu ya magonjwa.

Mkazi wa Kata ya Kihesa, Joyce John, anakiri kuwa jukumu la kuwapeleka watoto kliniki limehamia kwa ndugu wa familia.

“Mtoto wangu analelewa na mama yangu, ambaye mara nyingi humpeleka kliniki wakati wa kampeni za chanjo au siku za kupewa vitamini. Kama mtoto anaonekana mchangamfu na mzima, hupangiwa siku nyingine na kuondoka,” anasema.

Anaungwa mkono na mkazi wa Kata ya Ilula, Janeth Mhondele, anayesema elimu ya lishe mara nyingi hulenga watoto ambao wameonesha matatizo.

“Sisi ambao watoto wetu wanaonekana sawa tunaachwa,” anasema na kueleza kuwa watoto wanaweza kuonekana wenye afya lakini bado wakawa na matatizo ya ukuaji, jambo linalopuuzwa mara nyingi katika ushauri wa kawaida.

Uzoefu wa kinamama na walezi unaonesha uhitaji wa dharura wa ufuatiliaji wa kina wa ukuaji wa watoto, elimu ya lishe na msaada wa kijamii.

Bila hayo kufanyika, watoto wengi wako katika hatari ya athari za maisha yote zitokanazo na udumavu, hata pale mwonekano wao wa nje unapoonesha wako salama.

Iringa, kama ilivyo maeneo mengi ya Tanzania, bado ina changamoto, lakini simulizi za ustahimilivu, kujifunza na dhamira walizonazo kinamama kama Sebastian, Mlula na Mbimbi zinaonesha kuwa msaada kwa wakati, elimu na programu za kijamii vinaweza kuleta tofauti kati ya mtoto anayeteseka kimya kimya na mtoto anayenawiri.


Itaendelea kesho...