Ulaji wa chipsi unaofaa kuepuka maradhi

Muktasari:

  • Chipsi ni chakula maarufu ambacho kimeendelea kutengeneza ajira kwa vijana wengi mijini na hata wale wa vijijini.


Chipsi ni chakula maarufu ambacho kimeendelea kutengeneza ajira kwa vijana wengi mijini na hata wale wa vijijini.

Upatikanaji wake ni wa haraka, umeendelea kuwafanya vijana wa rika zote wa kike na kiume kuona chakula hicho ndio mkombozi wao wa haraka.

Kuna chipsi mayai ama maarufu kama chipsi zege, lakini chipsi zinaweza kuliwa na vyakula vingine kama kuku, soseji, nyama choma na maini.

Katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya mijini, biashara hiyo imeendelea kuota mizizi kuliko vijijini kutokana na utamu wake, upatikanaji wake wa haraka kuvutia watu wa rika zote kwenye jamii.

Matumizi ya chakula hiki ambacho huandaliwa kwa viazi na mayai ya kisasa, kinaendelea kuhusishwa au kuchangia vijana wengi kushindwa kuhimili tendo la ndoa, hatua ambayo imezidi kujenga hofu kwenye jamii juu ya wanaume kupoteza uwezo wao halisi wa kuzalisha.

Kushamiri kwa matumizi ya supu ya pweza, vumbi la kongo kwa lengo la kutafuta ustahimilivu kwenye tendo la ndoa kwa vijana ndicho kilichosababisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamiaji shughuli za lishe, kuhoji watafiti kuhusu ulaji wa chakula hicho kama inakwenda kujenga mwili.

“Chipsi zege imekuwa biashara kubwa sana, chipsi zege, sijui chipsi nini lakini je, chipsi ndio kila kitu na hiki ndio chakula kikubwa cha mabalehe wetu, ndio chakula kikubwa na ndio rahisi akitoka kwenye pilika zake weka chipsi zege bana anawekewe, chipsi zege na glasi ya juisi kajaza tumbo kapata nguvu anakwenda, lakini je, inakwenda kujenga mwili ipasavyo?” alihoji Rais Samia.

Chipsi na shida ya nguvu za kiume

Jackson Joseph, mkazi wa Tabata anasema ulaji wa chipsi unaonekana kuwa na madhara kutokana na vijana wengi kutokupenda mazoezi.

“Kama unakula unafanya mazoezi si tabu, mimi nakula na nipo vema, ukisema tule vyakula vya asili tutapata wapi? Mimi sijaoa, nategemea nikisikia njaa nile kwa wakati huo, sasa ni ngumu kusubiri chakula kwa muda mrefu ndio maana tunakimbilia huku,” anaeleza.

Japo ameacha kula chipsi, Robson Malik anasema baada ya kupitia shida ya kutohimili kushiriki tendo hilo kwa muda mrefu aliomba ushauri kwa wataalamu na kuambiwa apunguze vyakula vya mafuta.

“Nilikuwa nakula chipsi, nakunywa na soda, haiwezi kupita siku sijala, sasa nilivyoambiwa ni hatari kwangu, nilifuata ushauri kwa sababu mwenzangu kila mara nikikutana naye ananishangaa, namaliza ndani ya muda mfupi zaidi,” anasema.

Ofisa mtafiti mwandamizi wa lishe, Dk Hoyce Mshinda akizungumzia uhusiano wa ulaji wa chipsi na ukosefu wa nguvu za kiume anasema zipo sababu nyingi zinazochangia upungufu wa nguvu za kume, lishe duni ikiwa ni mojawapo ya sababu hizo.

Anasema ulaji chipsi mayai uliokithiri unachangia tatizo la ukosefu au upungufu wa nguvu za kiume.

“Ulaji chipsi mayai unaweza kusababisha magonjwa sugu yasiyoambukiza, hasa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari ambavyo vina uhusiano mkubwa na afya ya uzazi, ikiwemo uwezo wa mwanaume kitandani,” anaeleza.

Dk Hoyce anasema chipsi mayai si mlo kamili, hivyo huchangia utapiamlo (uzito uliozidi au kiriba tumbo) pamoja na ukosefu wa virutubishi muhimu mwilini, vikiwemo vitamini mbalimbali na madini ambavyo vina umuhimu mkubwa kwenye afya ya uzazi, ikiwemo uwezo wa mwanaume kitandani.

Anasema lishe bora ni muhimu katika kipindi chote cha maisha ya binadamu na uzazi kwa ujumla.

Kwa upande wake, ofisa lishe na mwanachama wa Chama cha Lishe Tanzania (TNDA), Johari Matiko anasema chakula hicho kipo kwenye kundi la wanga linalotokana na mizizi, ikijumuisha mihogo, viazi vitamu na mviringo.

Anasema kundi hilo la chakula linapaswa kuliwa, lakini ulaji wake unapozidi ndiko wataalamu wanasema si sahihi.

“Ukiangalia viazi vinaweza kuliwa kwa kukaangwa, kuchemshwa au kuchomwa, lakini vimekuwa vikiliwa sana vikiwa vimekaangwa kwenye mafuta mengi.

“Kwa hiyo kiazi kama kiazi hakina shida, shida inakuja kwamba ni yale mafuta yanayokuwepo, halafu kuna mayai ambayo mtu akila mara kwa mra anapata kilocalories nyingi,” anasema na kuongeza:

“Jambo lingine baya zaidi ni kula kila siku au mara mbili kila siku mchana na jioni, unakuta mtu anakula anakwenda kukaa bila kufanya kazi ambayo itaondoa ile nguvu iliyoingia,” anaeleza.

Johari anabainisha kuwa nishati hiyo ambayo huingizwa mwilini na kutotumika huchakatwa na kihifadhiwa kwenye mishipa ya damu ya moyo kama mafuta.

Madhara anayotaja Johari ni mishipa inayopata damu kubanwa na kushindwa kupitisha kama inavyopaswa.

“Ukiangalia kwenye tendo la ndoa lazima misuli ile ipitishe damu, na inapopitisha damu kwa kasi kijana anakuwa na uwezo wa kusimamisha uume,” anaeleza.

Hatari iliyopo kwa walaji wa chipsi anayoitaja Johari ni mafuta kujitengeneza na kuzunguka mishipa ya damu, hali ambayo hupunguza kasi ya damu na matokeo yake uume kushindwa kusimamia vema, jambo ambalo ni hatari kwa mwanamume.

Kula vyakula hivi

Johari anashauri badala ya kuzingatia ulaji wa chipsi mayai, ni muhimu mtu akaanza kutumia makundi matano ya chakula.

Makundi hayo anayotaja ni vyakula vya wanga ambavyo hupatikana kwenye mizizi na nafaka, akionya pia ulaji haupaswi kuwa ni kila siku.

Kwa wale wanaofanya kazi ofisini ambazo hazihusishi nguvu nyingi, anashauri waepuke ulaji mkubwa wa vyakula hivyo.

“Tule kwa kiasi ambacho hatutakuwa na hifadhi kubwa, tunapokula na kuzidisha kile kinachozidi kuna wakati yatatoka mwilini kama uchafu, lakini yapo yanayotunzwa kama mafuta,” anasema.

Aina nyingine anayotaja ni mboga zinazotokana na wanyama na mimea na kwenye kundi la wanyama zipo nyama za wanyama na samaki na dagaa.

Pia anashauri ulaji wa vyakula vitokanavyo na mimea jamii ya mikunde, mboga za majani na mbogamboga pamoja na matunda, akisema badala ya kunywa juisi, mtu anapaswa kula matunda halisi na matumizi ya sukari yawe kidogo pamoja na mafuta yazingatiwe kwenye milo.

Johari anakumbusha jamii kupendelea matumizi ya vyakula vilivyochemshwa na vya asili.

Usile mayai kila siku/punguza mafuta

Dk Mruma anasema mtu anaweza kula chipsi, lakini si kwa mazoea akionya mafuta yanayopaswa kutumika ni ya alizeti na mtumiaji ahakikishe anadhibiti mafuta.

“Pia mayai yasiliwe kila siku, chipsi inapaswa kuwa chakula cha dharura, walau mara moja kwa wiki. Pia upikaji wake uwe nyumbani na uambatane na vyakula vingine kama mboga na matunda.

“Kwa tafiti zilizofanyika zinaonyesha mbogamboga, matunda, korosho, karanga, mimea jamii ya mikunde, samaki na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu na nyama ya kwenye makopo kunapunguza uwezekano wa kupata tatizo la nguvu za kiume,” anasema.

Makundi matatu ya upungufu wa nguvu

Dk Mruma anaeleza kutokuwa na hamu ya kushiriki ngono ni dalili mojawapo ya upungufu wa nguvu za kiume, kwani hali hiyo inachangiwa na upungufu wa homoni za kiume ambazo hutambulika kwa jina la testosterone.

Mbali na homoni, kitu kingine anachotaja Dk Mruma ni ulevi, msongo wa mawazo na upasuaji wa tezi dume.

Kundi la pili ni kushindwa kusimamisha uume wakati wa kushiriki ngono, hali hii ndiyo Dk Mruma anaitaja kuwakumba vijana wengi.

Shida hii si kwa wanaume pekee, Dk Mruma anasema huwakumba pia wanawake ambao wao hushindwa kupata ute au kupata kiwango kidogo wakati akishiriki ngono.

“Karibu asilimia 10 mpaka 20 ya wanaume Marekani wanashindwa kusimamisha uume wakati wa kipindi chote cha kufanya ngono, utafiti unaonyesha asilimia kubwa hutokea kwa watu wanaovuta sigara na wenye uzito mkubwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anaeleza.

Eneo lingine analotaja ni matatizo ya kisaikolojia ambapo mwanaume kabla ya kukutana na mwanamke huwa na msongo wa mawazo au wasiwasi mkubwa.

Wasiwasi anaoutaja Dk Mruma ni wa mwanaume kushindwa kumridhisha mwanamke, hatua inayochangia kushindwa kuhimili tendo husika.

Kundi la tatu analotaja Dk Mruma ni kushindwa kufika kilele au kuwahi kufika kileleni, na shida hii ipo kwa wanaume na wanawake

“Asilimia tano ya wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 35 hawajawahi kufika kileleni, lakini kwa takwimu za jumla asilimia 30 ya kinamama hawajawahi kufika kileleni,” anasema.

Kwa upande wa wanaume anaeleza kuna tatizo la kuwahi kufika kileleni na kueleza kuwa mara nyingi tatizo hilo ni la kisaikolojia.