Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umoja wa Mataifa wapitisha azimio kuhusu magonjwa yasiyopewa kipaumbele

Hadija Mtitu, akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Mindutulieni Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, nchini Tanzania. Hadija ni miongoni mwa waathirika wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Picha kwa hisani ya Sam Vox/Uniting To Combat NTDs

Muktasari:

  • Magonjwa hayo ni pamoja na trakoma, kichocho, filariasis ya limfu, minyoo ya tumbo, ugonjwa wa ngozi wa ukoma na mengine yanayosababisha ulemavu wa kudumu, unyanyapaa, kupoteza kipato na wakati mwingine vifo vinavyoweza kuzuilika.

Dar es Salaam. Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) limeandika historia baada ya kupitisha kwa mara ya kwanza azimio linalotambua uhusiano wa moja kwa moja kati ya haki za binadamu na magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs), hatua inayotarajiwa kuimarisha juhudi za kimataifa za kutokomeza magonjwa hayo yanayoathiri zaidi ya watu bilioni moja duniani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tano za Afrika zilizofanikisha kupitishwa kwa azimio hilo, hatua inayotarajiwa kuimarisha juhudi za kutokomeza magonjwa hayo duniani.

Azimio hilo lililopitishwa jana Julai 7, 2026 mjini Geneva, Uswisi, liliongozwa na Malawi kwa kushirikiana na Tanzania, Kenya, Burkina Faso, Gambia na Morocco.

Kwa mara ya kwanza, Baraza la Haki za Binadamu limeeleza kuwa NTDs si changamoto ya afya pekee, bali pia zinahusisha haki ya kila mtu kupata huduma za afya, maji safi, mazingira salama, elimu na fursa sawa za maendeleo.

Hatua hiyo inakuja wakati zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaendelea kuishi na magonjwa yasiyopewa kipaumbele, ambayo huathiri zaidi jamii maskini na zilizo pembezoni kutokana na umaskini, ukosefu wa maji safi, huduma duni za usafi wa mazingira, makazi yasiyo salama na upatikanaji mdogo wa huduma za afya.

Hadija Mtitu, akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Mindutulieni Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, nchini Tanzania. Hadija ni miongoni mwa waathirika wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Picha kwa hisani ya Sam Vox/Uniting To Combat NTDs

Magonjwa hayo ni pamoja na trakoma, kichocho, filariasis ya limfu, minyoo ya tumbo, ugonjwa wa ngozi wa ukoma na mengine yanayosababisha ulemavu wa kudumu, unyanyapaa, kupoteza kipato na wakati mwingine vifo vinavyoweza kuzuilika.

Mbali na athari za kiafya, NTDs huwanyima waathirika haki ya kupata elimu, ajira na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo kuendeleza mzunguko wa umaskini na kutengwa.

Waziri wa Afya wa Malawi, Madalitso Chidumu Baloyi, amesema kupitishwa kwa azimio hilo ni ushindi mkubwa kwa mamilioni ya watu wanaoishi na magonjwa hayo.

"Kwa vizazi vingi Afrika imebeba mzigo mkubwa wa magonjwa haya, lakini pia imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuyatokomeza. Kupitishwa kwa azimio hili kunathibitisha kuwa hakuna mtu anayepaswa kunyimwa utu, afya au fursa kwa sababu ya ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika," amesema.

Kwa Tanzania, ushiriki wake katika kuandaa azimio hilo unaendana na juhudi za muda mrefu za kudhibiti magonjwa yaliyopuuzwa kupitia kampeni za utoaji dawa kwa jamii, upasuaji wa trakoma, udhibiti wa mbung'o na konokono wanaosababisha baadhi ya magonjwa hayo, pamoja na kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira.

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imepiga hatua katika kudhibiti baadhi ya magonjwa hayo kupitia Programu ya Taifa ya Kudhibiti Magonjwa Yaliyopuuzwa, ingawa baadhi ya magonjwa bado yanaendelea kuathiri wananchi katika maeneo yenye mazingira hatarishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, hadi sasa nchi 63 duniani zimefanikiwa kutokomeza angalau ugonjwa mmoja katika kundi la NTDs, jambo linaloonyesha kuwa uwekezaji, ushirikiano na dhamira ya kisiasa vinaweza kuleta mafanikio makubwa.

Hadija Mtitu, akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Mindutulieni Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, nchini Tanzania. Hadija ni miongoni mwa waathirika wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Picha kwa hisani ya Sam Vox/Uniting To Combat NTDs

Malawi, iliyoongoza mchakato huo, ilifanikiwa kutokomeza trakoma kama tatizo la afya ya umma mwaka 2022, huku pia ikiwa imeondoa filariasis ya limfu na ukoma kama matatizo ya afya ya umma.

Mkurugenzi wa Utetezi na Uhamasishaji wa Rasilimali wa taasisi ya Uniting to Combat NTDs, Stuart Halford, amesema azimio hilo litasaidia kuingiza haki za binadamu katika sera na mipango ya kutokomeza NTDs duniani.

Amesema hatua hiyo pia itaongeza uwajibikaji wa serikali, kuhamasisha uwekezaji zaidi na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya afya na sekta nyingine zinazochangia kudhibiti magonjwa hayo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia, Haki na Usawa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Alia El-Yassir, amesema azimio hilo linatoa fursa ya kuimarisha mifumo ya afya inayozingatia usawa na haki za binadamu, huku likishughulikia pia sababu zinazochangia kuendelea kwa magonjwa hayo, ikiwemo umaskini, unyanyapaa na ukosefu wa huduma muhimu.

Azimio hilo pia limeiagiza Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu (OHCHR) kufanya mashauriano ya kimataifa kuhusu uhusiano kati ya haki za binadamu na NTDs na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia serikali kuingiza misingi ya haki za binadamu katika sera na programu za kitaifa za kudhibiti magonjwa hayo.

Wataalamu wanaamini hatua hiyo itasaidia kubadili mtazamo wa dunia kuhusu NTDs, kutoka kuyaona kama magonjwa yanayohitaji matibabu pekee hadi kuyatambua pia kama changamoto ya maendeleo na haki za msingi za binadamu.

Kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika ambazo bado zinaendelea kupambana na baadhi ya magonjwa hayo, azimio hilo linatarajiwa kuongeza msukumo wa kisiasa na kifedha katika juhudi za kuhakikisha wananchi wote wanapata kinga, uchunguzi na matibabu bila ubaguzi, sambamba na kuboresha mazingira yanayochangia kutokomeza magonjwa hayo kwa njia endelevu.