Umuhimu wa chanjo ya HPV kwa wanawake
HPV ni kifupisho cha kitabibu cha Human Papilloma Virus ambavyo ni aina ya virusi ambavyo ni kihatarishi kikuu kwa maelfu ya wanawake wanaopata saratani ya mlango wa kizazi.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), karibu kila mwaka wanawake 300,000 wanapoteza maisha kwa sababu ya saratani hii.
Wengi wa wanawake hawa wanatoka nchi zenye uchumi wa chini mpaka wa kati, hasa nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania na nchi za Afrika Mashariki.
Katika kuelekeza mapambano dhidi ya ugonjwa huu, wanasayansi nguli, Profesa Ian na Dk Jian Zhou kutoka Chuo Kikuu cha Queensland cha nchini Australia walitengeneza virusi bandia (chanjo) mwaka 1990.
Ugunduzi wa chanjo dhidi ya virusi vya HPV ndiyo sasa umeleta matumaini makubwa kwa kizazi cha watoto wa kike, kwani chanjo hii inakadiriwa kuzuia uambukizi wa virusi hivi na hatua za mwanzo za saratani kwa karibu asilimia 100.
Kawaida chanjo hii inafanya kazi na kumkinga mtu ambaye hajawahi kupata uambukizi wa virusi vya HPV.
Chanjo hii imetengenezwa na kuzuia virusi vya HPV namba 16 na 18 na kuzuia uambukizi mpaka asilimia 70 ya saratani ya mlango wa kizazi.
Vilevile aina nyingine ya chanjo hizo huweza kuzuia pia aina nyingine ya HPV namba 6 na 11 na kuzuia kwa asilimia 95 ya sunzua, kwa kitabibu Genital-warts.
Sunzua ni tatizo la kiafya la juu ya ngozi linalosababishwa na virusi hawa wanaosababisha saratani ya mlango wa kizazi, huwa na mwonekana kama vile vichuguu vikavu mfano wa kuta za chupingi.
Virusi hawa huambukiza kwa njia ya kujamiiana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa kugusana na ngozi na maji maji ya sehemu za siri ya mtu mwenye maambukizi.
Ukiacha uharibifu wa ngozi na saratani ya mlango wa kizazi, vilevile virusi wa HPV wanahusishwa na saratani za sehemu za siri na kinywa (mdomo).
Ikumbukwe watu walio katika hatari ya kupata saratani ya kinywa ni wale wanaojamiiana kwa njia ya mdomo na mtu mwenye uambukizi wa HPV.
Chanjo hii ambayo ina baraka zote toka WHO imeshaanza kutolewa hapa nchini kwa watoto wa kike walio shuleni wenye umri kati ya miaka 9-14.
Chanjo hii hutolewa kwa awamu mbili, ya kwanza katika umri wa miaka 11-12 na ya pili hutolewa baada ya miezi 12-24 tangu kuchanjwa ya kwanza.
Pamoja na mafanikio haya, chanjo hii imewahi kupata upinzani kwa baadhi ya wadau wa afya kuhusu usalama wake, lakini kwa mujibu wa WHO na Wizara ya Afya chanjo ni salama kwa binadamu.
Madhara machache yanayojitokeza mwilini hayaondoi thamani ya kitiba ya chanjo hii inayozuia saratani inayoua maelfu ya wanawake duniani.
Madhara hayo machache yenye kuvumilika na kuzuilika ni pamoja na homa, kuvimba na maumivu eneo lilipochomwa sindano, kuwashwa, kutoka vipele, mwili kuuma, kizunguzungu, kichefuchefu na kutapika.
Wagonjwa wachache wanaweza kupata tatizo la kupoteza fahamu na degedege.
Tangu kuanza kutolewa chanjo hii nchini, hakuna madhara makubwa yanayojitokeza kwa muda mfupi ambayo yameripotiwa kutokea kwa watoto wa kike waliochanjwa.
Ili kuepukana na kuenea kwa maambukizi ya HPV, ni vizuri kuepukana na kujamiiana bila kinga, kuepuka kujamiiana na wapenzi wengi na kuepukana na kujamiiana katika umri mdogo.
Kinga ni bora kuliko tiba, muhimu wasichana kuitikia mwito wa kitaifa wa chanjo hii pale wanapohitajika kuchanja.