Usugu wa dawa za VVU waibua changamoto mpya za matibabu
Dar es Salaam. Asilimia 5.8 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (waviu) na wanaotumia dawa, wanakabiliwa na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo, utafiti mpya umeonyesha.
Usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa ni changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa.
Lakini usugu wa virusi vya Ukimwi (VVU) dhidi ya dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo, yaani ARV ni changamoto mpya kwa wanasayansi, wakiwa bado hawajapata suluhu ya tiba ya ugonjwa huo.
Usugu wa dawa ARV pia umetajwa kuwaathiri wenye maambukizi mapya, ambao wamekuwa wakipata changamoto wanapoingizwa katika matibabu.
Kisayansi, virusi vinapojenga usugu dhidi ya dawa za ARV, maana yake ni kuwa hazitaweza tena kupambana na VVU, hivyo kuendelea kuzaliana na kinga za mgonjwa ‘CD4’ kushuka na hatimaye ataanza kupata magonjwa nyemelezi, yaani Ukimwi.
Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ulionyesha asilimia 5.8 ya waviu na wanaotumia dawa, wanakabiliwa na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.
Mtafiti Mwandamizi Kitengo cha Maikrobaiolojia na Kinga MUHAS, Dk Doreen Kamori, anasema walifanya utafiti huo mwaka 2020 katika mikoa 22 Tanzania Bara, ikiwamo Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe.
Dk Kamori anataja sababu zinazochangia tatizo hilo ni pamoja na kuingizwa nchini dawa ambazo zinachangia usugu na watu kutokuwa wafuasi wazuri wa kutumia dawa.
Hata hivyo, anasema dawa kujenga usugu humaanisha mtu aliyeathirika anatumia ile dawa inakua haina nguvu ya kuzuia vile virusi kuendeea kukua na kuzaliana kwenye mwili.
"Tunatarajia akinywa dawa izuie kukua na kuzaliana kwa virusi, akipata usugu kwa maana haifanyi kazi au isifanye kazi inavyotakiwa au ikapunguza nguvu yake," anasema.
Anaelezea ukubwa wa tatizo hilo, "Kwa wanaoishi na VVU wanaotumia dawa kati ya waviu 100 kuna asilimia zaidi ya 94 dawa zinafanya kazi vizuri, lakini asilimia 5.8 dawa haifanyi kazi vizuri, hiyo asilimia ndogo wengi wao wana usugu wa dawa, kwa hiyo ni zaidi ya asilimia 70 yao," anasema.
Dk Kamori anatoa ushauri kwa Serikali wanapofikiria kubadilisha dawa au kuingiza nchini ni vyema kuweka miongozo na kufanya utafiti kufahamu wingi wa VVU kwa wagonjwa na kuangalia namna ya kuboresha
"Ni vyema kuweka miongozo na kujiandaa vizuri kumudu tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya VVU au kudhibiti kabla ya dawa hizo kuleta madhara," anasema.
Hata hivyo, usugu wa dawa huleta tathmini ya gharama kwa mtu au jamii anayoipata kutokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa kutumia gharama kubwa kutibu usugu wa vimelea hivyo.
Hali ilivyo nchini
Mpaka sasa Tanzania inatumia dawa za mistari mitatu pekee, ambapo ili mtu ahame kutoka mstari mmoja kwenda mwingine ni mpaka wataalamu wajiridhishe kuwa dawa ya mstari husika imeshindwa kumtibu (imejenga usugu).
Wakati changamoto hiyo ikitokea, takwimu zinaonesha anayeishi na virusi vya Ukimwi akitumia ARV hutumia dawa zenye thamani ya mpaka Dola 58.20 kwa mwezi, sawa na Sh135,780.
Alipoulizwa kuhusu changamoto hiyo, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi anakiri uwepo wa changamoto hiyo, akisema usugu husababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.
Iwapo mtu ametumia dawa pasipo kupima, kutumia dawa za mtu mwingine huku akitaka hatua za kuchukua ni kurudi kwenye matumizi sahihi.
"Virusi huwa vinatafuta namna mpya ya kuishi, kuna dawa mpya zinaendelea kuibuliwa kama mnaziona zinatangazwa, tunaendelea kukabiliana na hilo tatizo.
"Kwenye matibabu ya ugonjwa wa Ukimwi kinachofanyika unafika tunakupima, tukibaini una maambukizi unaanzishiwa dawa za mwezi mmoja.
"Ukirudi kliniki kuna vipimo vinafanyika vya ini, namna mwili ulivyopokea dawa wanaangalia virusi kushuka, kupungua vyote vinapimwa, kama hakuna matokeo huyu mtu tunamhamisha kwenda kundi la pili la dawa," anasema.
Mfamasia huyo wa Serikali anasema wamekuwa wakibadilisha dawa kwa waviu kulingana na mwenendo wa dawa husika alizoanza nazo na iwapo hazijaonyesha ufanisi.
"Kuna wimbi zile dawa za mwanzo zimeshindwa kumsaidia mgonjwa, kuna changamoto zinaendelea ambazo zinatatuliwa.
“Kwa kadIri anavyohudhuria kliniki tunakuwa tunamuangalia je, dawa tunamzompa zinamsaidia au hazimsaidii, kwa maana kuna dawa kundi la kwanza kila mtu anaanza nazo hizo, zisipomsaidia wanampa kundi la pili na zikikataa kundi la pili anaanza kutumia za kundi la tatu,” anasema.
Anasema kwa kawaida mviu dawa anazotumia zinapaswa kushusha idadi ya virusi na kuongeza kinga za mwili CD4 na ikiwa zinaongeza virusi na kushusha kinga hapo ndipo hulazimika kubadilishiwa dawa.
Hata hivyo anasema, “Mviu hubadilishiwa dawa siyo tu ikiwa hazitomsaidia, bali pale zinapoanza kuwa na madhara makubwa kwenye mwili wake. Kuna utaratibu wa kubadilisha dawa ambao TMDA ‘Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba’ wanakuwa na fomu kadiri yale madhara yanavyoripotiwa, baadaye wanaona hii dawa athari zake zimekuwa ni kubwa miongoni mwa watumiaji, hivyo inaondolewa sokoni.”
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Said Aboud, anasema tatizo la usugu wa ARV linazidi kuongezeka kwa sababu waviu wanaendelea kutumia dawa maisha yao yote, hivyo ni muhimu kuweka mikakati, ikiwamo kufuata maelekezo ya daktari na mwongozo unaotakiwa wakati wa kutumia dawa hizo.
Anasema mviu anapaswa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu kutoka kwa daktari badala ya kutumia dawa kiholela.
"NIMR inatekeleza Mpango wa Taifa Kudhibiti Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza, yakiwamo maambukizi ya VVU na Ukimwi, tunatekeleza afua mbalimbali katika mapambano hayo ili kuwasaidia kuboresha maisha yao na kuchangia nguvukazi ya taifa," anasema Profesa Said.
Tafiti
Utafiti uliofanywa katika mikoa 19 nchini mwaka 2019 ulionyesha baadhi ya wajawazito wenye maambukizi ya VVU wamejenga usugu wa dawa ya Dolutegravir (DTG).
Matokeo ya utafiti yalionyesha ARV zimejenga usugu kwa asilimia 27.5 kwa kinamama waliogundulika na maambukizi wakati wa ujauzito ambao hawajaanza kutumia dawa na asilimia 79.2 kwa wale ambao tayari walikuwa kwenye matumizi ya ARV.
Utafiti huo uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Management Development for Health (MDH) na Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa Marekani (CDC) ni miongoni mwa tafiti tatu zilizofanywa nchini kuangalia udhibiti wa mlipuko, kinga na tiba ya VVU wakati wa ujauzito na kunyonyesha.
Utafiti huo ulisajili wajawazito 459 ambao hawakuwa katika matumizi ya dawa na 543 walio na uzoefu wa matumizi ya dawa kwa pamoja kutoka kliniki 52 zilizochaguliwa bila mpangilio maalumu katika mikoa 19 kuanzia Aprili hadi Septemba, 2019.
Mabadiliko ya ARV
Kumekuwa na mabadiliko ya dawa tangu zilipoanza kutolewa rasmi nchini mwaka 2004, ambapo nchi ilitumia dawa zilizoitwa Dolutegravir, ambazo ndani yake kulikuwa na dawa za Tenofovir 300mg/, lamivudine 300mg/ na dolutegravir 50mg ambazo kwa sasa hivi hazitumiki kutokana na madhara anuai.
Dawa ya Tenofovir ilikuwa na madhara kwa watu wakati ilipokuwa ikitumika, lamivudine ilikuwa dhaifu na ilisababisha mabadiliko makubwa ya mwili wa aliyekuwa akiitumia, ikiwemo kupoteza nuru, kukonda na mafuta kwenye mwili kurundikana sehemu moja.
Anasema kutokana na madhara hayo, Serikali iliziondoa dawa hizo na kuleta aina nyingine, lakini kuanzia mwaka 2005 mpaka 2019 haijawahi kufanya kipimo cha kuangalia usugu wa dawa, bali kuangalia madhara pekee na iwapo CD4 zinapanda au hazipandi.
Mkuu wa kitengo Idara ya Maabara ya kifua kikuu Mbeya katika Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR), Dk Bariki Mtafya anasema maabara hiyo iliyopo Nyanda za Juu Kusini ni kubwa kwa uwezo wa kutambua ugonjwa, kubaini usugu wa dawa.
Anasema maabara hiyo inaweza kutambua iwapo mgonjwa ana usugu kwenye dawa za awali za kutibu ugonjwa huo au hana usugu na inaamua ni dawa ipi anaweza kutumia ili aweze kupona.
“Kama ana usugu tayari basi anatakiwa kuanza kutumia dawa za kundi la pili, sampuli tunazipata kutoka katika hospitali mbalimbali na tunakuja nazo maabara kupima.
“Tukishachakata sampuli inasaidia sana pia kugundua wagonjwa wa Ukimwi ambao pia wana maambukizi ya kifua kikuu, pia inasaidia kuweza kuwatibu, hasa kuwaanzishia dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi yaani ARV,” anasema.