Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vituo vya mazoezi vinapogeuka fasheni na maonyesho

Muktasari:

  • Swali la msingi ni hili, Je, tunaenda gym kwa ajili ya mwili na afya zetu, au kwa ajili ya macho ya watu?

Dar es Salaam. Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojiunga na vituo vya mazoezi maarufu kama gym katika miji mikubwa na hata baadhi ya miji midogo nchini. 

Kutoka Dar es Salaam hadi Arusha na Mwanza, majengo yenye vioo vikubwa, muziki wa juu na mashine za kisasa yamekuwa sehemu ya mandhari ya kila siku.

Hata hivyo, nyuma ya mwonekano huo wa kisasa, kuna mjadala unaozidi kushika kasi: Je, watu wanaenda gym kwa ajili ya afya au kwa ajili ya kuonesha maisha fulani?

Je, vituo vya mazoezi vimebaki kuwa mahali pa kujenga mwili na afya, au vimegeuka kuwa sehemu ya fasheni na kile kijulikanacho kama 'mtoko'?

Taswira inayoonekana katika baadhi ya vituo vya mazoezi leo inaashiria mabadiliko ya dhana ya uwepo wa vituo hivyo. 

Wapo wanaoingia wakiwa wamevalia mavazi ya gharama kubwa, viatu maalumu vya mazoezi na vifaa vya kisasa vya kusikiliza muziki, lakini muda mwingi hutumika mbele ya vioo wakipiga picha au kurekodi video kwa ajili ya mitandao ya kijamii. 

Kwao, gym si tu sehemu ya mazoezi bali ni jukwaa la kuonesha mtindo wa maisha wanaotaka wengine wauone.

Mkufunzi wa mazoezi katika Jiji la Mwanza, Isaack Mwakalebela, anasema watu wanaokwenda gym wana malengo tofauti kulingana na mahitaji yao.

“Wapo wanaokuja kwa ajili ya afya, kama kupunguza uzito, kuepuka magonjwa kama kisukari na presha, kuongeza nguvu za mwili na hata kupunguza msongo wa mawazo. Lakini pia wapo wanaokuja kwa ajili ya mwonekano kupata mwili mzuri, kujiamini na kuvutia,” anasema.

Anaeeleza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuwavuta vijana wengi kuingia gym kwa lengo la kufanana na watu maarufu au kuendana na mitindo ya sasa.

Hata hivyio, mkufunzi mwingine, Innocent Kalonga anasema kwa sasa vijana wengi wanaingia gym kwa ajili ya fasheni zaidi kuliko afya.

Asilimia kubwa wanataka miili yao iwe na mvuto ili nguo ziwakae vizuri au wapate maumbo yanayovutia,” anasema.

Hali hii imeifanya gym kwa baadhi ya watu kuwa ishara ya hadhi. Kuonekana umejiunga na kituo fulani maarufu kunachukuliwa kama mafanikio ya kijamii. 

Wengine hujisajili bila hata kuwa na mpango wa mazoezi, wakiamini uwepo wao pekee unatosha kuwatambulisha kama watu wanaojali afya na mwonekano. Lakini ukweli unabaki kuwa mazoezi si mapambo ya hadhi bali ni hitaji la mwili.

Mtaalamu maarufu wa mazoezi kutoka Marekani, Jack LaLanne, aliwahi kusisitiza kwamba mazoezi ni mfalme na lishe ni malkia; na kwamba vikiunganishwa pamoja ndipo unapata ufalme kamili wa afya. 

Tafsiri ya kauli hiyo ni kwamba hakuna njia ya mkato katika kujenga afya. Lazima kuwe na juhudi, nidhamu na uelewa.


Kazi za gym

Kazi halisi ya kituo cha mazoezi ni kusaidia watu kuimarisha afya ya miili yao na akili zao. 

Ndani ya gym hupatikana vifaa vya kuongeza nguvu za misuli, kuboresha uwezo wa moyo na mapafu, kupunguza uzito na kuongeza unyumbufu wa mwili. Mazoezi ya mara kwa mara husaidia kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na matatizo ya moyo.

Aidha, husaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza hali ya kujiamini.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa mwili wa binadamu umeumbwa kwa ajili ya kushughulika.

Kukaa muda mrefu bila mazoezi huathiri mifupa, misuli na hata mfumo wa damu. Ndiyo maana vituo vya mazoezi vilianzishwa kama sehemu maalumu za kuwezesha harakati hizo kwa usalama na kwa mwongozo wa kitaalamu.

Mkufunzi mashuhuri wa mazoezi, Jillian Michaels, aliwahi kusema kwamba mazoezi si suala la kuwa bora kuliko mtu mwingine, bali ni kuwa bora kuliko ulivyokuwa jana. 

Kauli hii inabeba ujumbe mzito kwa wale wanaochukulia gym kama sehemu ya mashindano ya kuonesha miili au mavazi. Safari ya mazoezi ni ya mtu binafsi; ni mapambano ya kuboresha afya yako mwenyewe.

Changamoto inakuja pale ambapo lengo la msingi linapotea. Wapo wanaotumia muda mwingi kupiga picha kuliko kufanya mazoezi.

Wengine hujihusisha na mazoezi bila kufuata mwongozo sahihi, hali inayoweza kusababisha majeraha. Baadhi, wakitamani matokeo ya haraka ili waonekane wamebadilika, hujikuta wakitumia virutubisho visivyo salama au dawa hatarishi.

Bingwa wa zamani wa kujenga mwili na mwigizaji maarufu, Arnold Schwarzenegger, aliwahi kueleza kuwa upinzani unaokutana nao gym na ule wa maisha kwa ujumla ndiyo unaojenga tabia imara. 

Tafsiri ya maneno hayo ni kwamba mazoezi ni shule ya uvumilivu na nidhamu. Si mahali pa kujionyesha bali ni uwanja wa kujifunza kujishinda.

Ni muhimu pia kutambua kuwa si kila anayekwenda gym anafanya hivyo kwa lengo la kujionesha. 

Wapo wengi wanaotumia nafasi hizo kwa umakini, wakifuata ratiba maalumu, wakizingatia lishe na mapumziko, na hatimaye kuvuna matokeo chanya. 

Hawa ndio wanaothibitisha kuwa gym bado ina heshima yake kama kituo cha afya.


Tusiruhusu dhana potofu

Hata hivyo, jamii inapaswa kujiuliza kama tunaruhusu dhana potofu kutawala. 

Endapo gym itageuzwa kuwa eneo la burudani na maonesho, tutapoteza maana yake ya msingi. 

Afya haiwezi kujengwa kwa mitindo ya muda mfupi. Inahitaji uthabiti na uelewa wa kina.

Mwisho wa yote, gym ni chombo tu. Thamani yake inategemea namna tunavyokitumia. 

Inaweza kuwa daraja la kuelekea maisha yenye afya bora, au inaweza kuwa jukwaa la kujionesha lisilo na matokeo ya kudumu. Uamuzi unabaki kwa kila mmoja wetu.

Jamii ikirejea kwenye dhana sahihi ya mazoezi, vituo vya mazoezi vitaendelea kuwa sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya magonjwa na udhaifu wa mwili. Lakini kama vitaendelea kuchukuliwa kama fasheni, basi tutajikuta tukijenga taswira nzuri huku afya zetu zikiendelea kudorora.

Swali la msingi linabaki palepale: Je, tunaenda gym kwa ajili ya mwili na afya zetu, au kwa ajili ya macho ya watu?