Wenza wanavyoshirikiana asilimia 30 ya bakteria wa tumboni
Muktasari:
- Utafiti unaonyesha kuwa wanandoa wanaoshirikiana mazingira ya nyumbani, vyombo vya chakula, na hata ukaribu wa kimwili kama busu, huhamishiana mamilioni ya bakteria kwa kila mgusano
Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini kuwa watu wanaoishi pamoja kama wanandoa au wapenzi hushirikiana kiasi kikubwa cha vimelea vya asili mwilini mwao (microbiome), hususan bakteria wa tumboni.
Kwa mujibu wa wataalamu, wapenzi hushirikiana takriban asilimia 30 ya bakteria wa mfumo wa chakula, jambo ambalo lina athari za moja kwa moja kwa afya zao kwa ujumla.
Imekuwa ikifahamika kuwa mazingira na vinasaba ndivyo vinavyoamua afya ya mtu.
Hata hivyo, makala hii iliyotafsiriwa kutoka Jarida la The Conversation inaangazia jinsi ukaribu wa kimwili na maisha ya pamoja, vinavyoweza kubadili mfumo wa kinga na usagaji chakula wa mwenzako kupitia mabadilishano ya viumbe hao wadogo.
Siri ya "Microbiome" wa pamoja
Wataalamu wameeleza kuwa, ingawa mlo na mtindo wa maisha ndio vigezo vikuu vinavyoamua aina ya bakteria waliomo tumboni, kuishi na mtu mwingine kwa muda mrefu, kunaongeza ulinganifu wa viumbe hao.
Utafiti unaonyesha kuwa wanandoa wanaoshirikiana mazingira ya nyumbani, vyombo vya chakula, na hata ukaribu wa kimwili kama busu, huhamishiana mamilioni ya bakteria kwa kila mgusano.
Inakadiriwa kuwa busu moja la sekunde kumi pekee linaweza kuhamisha hadi bakteria milioni 80 kati ya wapenzi wawili.
Ugunduzi wa utafiti huu una pande mbili za sarafu linapokuja suala la afya:
Kwanza kuna faida ya uanuwai. Wanandoa wenye uhusiano wenye furaha na ukaribu wa juu wamebainika kuwa na uanuwai mkubwa wa bakteria (microbial diversity). Kitaalamu, uanuwai huu unahusishwa na kinga imara dhidi ya magonjwa ya mfumo wa chakula, magonjwa ya moyo, na kiwango bora cha sukari mwilini.
Upande wa pili ni kwamba, ikiwa mwenza mmoja ana bakteria hatari, kuna uwezekano mkubwa wa kumfanya mwenzake kuwa katika hatari ya kupata matatizo yale yale. Bakteria jamii ya Ruminococcus na Neisseria wanapotawala kwa wingi miongoni mwa wanandoa, wanaweza kuongeza hatari ya kisukari au matatizo ya meno na kinywa kwa wote wawili.
Mlo wa pamoja ni tiba
Watafiti wanashauri kuwa, kwa sababu wanandoa mara nyingi hula chakula cha aina moja, hii ni fursa nzuri ya kuboresha afya ya familia kwa pamoja.
Ikiwa mmoja ataanza kula vyakula vyenye nyuzinyuzi na vyakula vyenye uchachu, anaweza kusaidia "kupandikiza" bakteria wazuri kwa mwenzake kupitia maisha ya kila siku.
Hii ina maana kwamba afya ya utumbo sasa si suala la mtu binafsi tu, bali ni jukumu la pamoja ndani ya nyumba.
Makala haya yametafsiriwa kutoka Mtandao wa The Conversation.