Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kona ya Wastaafu: ‘Wote ni wastaafu’, tofauti ya pensheni ya nini?

Muktasari:

  • Mstaafu wetu anajikuta akikubaliana na mtunzi wa hadithi moja ya Kiingereza huko duniani, George Orwell, aliyoiandika miaka 80 iliyopita na kutafsiriwa kwa Kiswahili chetu chema iitwayo ‘Shamba la wanyama’ au ‘Animal farm’ kuwa ‘kimbugu’ ambayo anaamini kuwa wastaafu wenzake walipata kuisoma enzi zilee darasa lilipokuwa na wanafunzi 45 tu na si haya tunayoyaona leo hii ya darasa moja kuwa na wanafunzi 70!

Ilikuwa ni hadithi njema, na mstaafu wetu anajikuta akikumbuka zaidi maneno ya mwandishi huyo aliyewatumia wanyama katika hadithi yake, ya kwamba “watu wote ni sawa, lakini kuna ambao wako sawa zaidi kuliko wengine”!

Mstaafu wetu anajikuta akiyatafakari na kuyakubali maneno ya mtunzi George Orwell aliyoyaandika miaka 80 iliyopita, hasa anapoangalia tofauti iliyopo kati ya malipo ya pensheni ya wastaafu waheshimiwa na wastaafu wa kima cha chini. Anaona mambo yale yale aliyopata kuandika George Orwell miaka 80 iliyopita ya “binadamu wote ni sawa, lakini kuna wengine wapo ‘sawa zaidi’ kuliko wengine wote”!

Inaeleweka, hapa kwetu ndivyo ilivyo. Mstaafu anajua kuwa hapaswi kutegemea pensheni anayopata ya Sh110,000 kwa mwezi ifanane na pensheni anayopokea waziri wa wizara yoyote au mkurugenzi mtendaji wa iliyokuwa National Bank of Commerce (NBC) ya enzi zetu au katibu mkuu wa wizara. Thubutuu! Shule na madarasa yanawatofautisha, japokuwa si lazima kwamba wakikimbilia umande!

Mstaafu wetu anakumbuka miaka michache iliyopita chama kilipokuwa kimeshika utamu, samahani… kilipokuwa kimeshika hatamu, na mwenyekiti wa chama wa tawi la shirika la umma aliyeishia darasa la saba alikuwa na sauti kuliko mkurugenzi mtendaji wa shirika mwenye “mapiechidii” yake!

Mstaafu wetu pia anaamini kuwa hapaswi kupinga waheshimiwa wastaafu kulipwa asilimia 80 ya mshahara wa mheshimiwa aliyempokea madaraka, wala hapaswi kuona donge waziri mstaafu au aliyekuwa mkurugenzi mtendaji akipokea pensheni ya mwezi ya asilimia 50 ya mshahara wa waziri aliyechukua madaraka, huku pensheni yake ikipata nyongeza kadri ya mshahara wa yule aliye kazini!


Katika yote haya, mstaafu wa kima cha chini anajikuta akibaki kukimbizana na Sh110,000 isiyohesabika kwa asilimia ya mshahara wa yule aliyempokea kazi, wala hapati nyongeza ya pensheni kama mshahara wa yule mwenzake unavyopata nyongeza kila baada ya miaka miwili mitatu, huku yeye akiwa amepokea pensheni hiyo kwa miaka 21 sasa.

Pamoja na hilo, hakuna mheshimiwa anayepiga mwingi kwake, bali wamekauka kushinda nguo ya mtumba, na inaishia kuwa ni kweli, “binadamu wote ni sawa, lakini wengine ni sawa zaidi” kuliko wengine!

Hili limeonekana vizuri zaidi mwezi uliopita wakati Bunge lilipotangaza kuwa Serikali inatoa nyongeza ya pensheni kwa wastaafu wanaopokea pensheni kutoka Hazina, kutoka Sh120,000 kwa mwezi kuwa Sh300,000 kwa mwezi kuanzia Julai, kwa kile kilichosemwa na Serikali kuwa ni kuwasaidia wastaafu hao wa Hazina kukabiliana na hali ngumu ya maisha!

Hii ndiyo “hali ngumu ya maisha”... ambayo sasa imefanywa kuwa inamkabili kila mtu kasoro mstaafu wa kima cha chini anayeaminika kuweza kuishi kimiujiza kwa pensheni ya Sh110,000 kwa mwezi, na wawakilishi wake wako bize kutaka magari yao yawe na namba maalumu za kuwatambulisha, badala ya kuwa bize kuwapigania wastaafu wa kima cha chini cha mshahara wapate kiwango cha mshahara kitakachowawezesha kupambana na hali ngumu ya maisha kweli na si bla bla!

Mstaafu wetu bado anakumbuka kuwa Serikali ilitoa tangazo kama hili Oktoba mwaka jana, ikisema kuwa ni katika kuwasaidia wastaafu wa kima cha chini cha pensheni kukabiliana na hali ngumu ya maisha, na ikawaongeza Sh50,000, rudia hapo Sh 50,000, ili ile pensheni waliokuwa wakiipata kwa miaka 21 nyuma, sasa iwe Sh150,000, na wakaambiwa nyongeza hiyo wataanza kuipata Januari hii, miezi mitatu baadaye!

Januari ilipofika, nyongeza ya Sh50,000 haikuonekana, bali wastaafu wakaambulia kupata kati ya Sh8,000 hadi Sh10,000 ili wastaafu waweze kupambana na hali ngumu ya maisha, na unaweza hata kuwa jasiri na kusema... inayoletwa na Serikali! Kukabiliana na hali ngumu ya maisha kwa Sh50,000? Je, wale wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kwa shilingi milioni… mama wee!... 14 kwa mwezi??

Mstaafu anasubiri hao wenzake wa Hazina walioongezwa Sh180,000 kuwafanya wapate Sh300,000 kwa mwezi na kuambiwa nyongeza hiyo itaingia mifukoni mwao mwishoni Julai, watapata ngapi? Wakati sisi wenzao wa kima cha chini tuliishia kupata nyongeza ya Sh10,000, na waheshimiwa wameuchuna!

Tuambiwe, wastaafu wa kima cha chini waliopewa nyongeza ya Sh50,000 kwa mwezi ambayo imeishia kuwa ‘maneno ya kanga’ tu, na hawa wa Hazina walioahidiwa kupata nyongeza ya Sh180,000 ili iwe pensheni ya Sh300,000 kwa mwezi, lakini Julai wanaweza wakaishia kupata ‘maneno ya kitenge’ tu, wana tofauti gani ya ustaafu inayowafanya watofautiane hivyo? Ndio mambo ya ‘gawanya utawale’ haya?

Wastaafu tuondoe woga. Tuiambie Serikali tunaidai. Bado tunahitaji malipo ya pensheni yanayoweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha kweli na si kutuletea mambo ya ‘Shamba la wanyama’ ambapo “binadamu wote ni sawa, lakini wengine wapo sawa zaidi” kuliko wengine!


0754 340606 / 0784 340606