Angela naye atua Basata kudai haki zake

Muktasari:

  • Bundi bado ametua kwenye lebo ya Konde Music, ndivyo unavyoweza kusema baada ya msanii kutoka lebo hiyo, Angelina Samson, maarufu Angela naye kuwasilisha malalamiko Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), akidai waachane naye rasmi.

Bundi bado ametua kwenye lebo ya Konde Music, ndivyo unavyoweza kusema baada ya msanii kutoka lebo hiyo, Angelina Samson, maarufu Angela naye kuwasilisha malalamiko Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), akidai waachane naye rasmi.

Madai ya Anjela kuachana na lebo hiyo rasmi badala ya ilivyo sasa kimyakimya, yamekuja wiki moja baada ya lebo hiyo kumalizana na wasanii wengine wawili Cheed na Killy, waliokuwa na malalamiko yanayofanana na hayo.

Kikizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina gazetini kwa sababu ya masuala ya kimkataba, chanzo cha kuaminika kimesema kuwa Novemba mosi Harmonize alitakiwa afike Basata kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo, lakini hakutokea.

Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa malalamiko ya Angela ni tofauti na Cheed na Killy, ambapo yeye anadai kupewa barua rasmi ya kuachana naye na kumrudishia digital platform zake.

“Mkataba ulikuwa unasema Angela akiuvunja atawalipa Sh bilioni moja, lakini wakiuvunja wao watamrudishia digital platform zake tu bila hata senti tano, sasa wanachokifanya ni uhuni, wameachana naye kimtindo ila hawataki kumalizana naye kila mmoja ashike njia yake.

“Kama ni fedha za nyimbo zake na lolote likitokea wanaendelea kunufaika wao na si Anjella ambaye wamemuweka kando,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Mbali na hilo, msanii huyo pia aliahidiwa na Harmonize kusaidiwa matibabu ya mguu, jambo ambalo halikufanyika.

Angela anasumbuliwa na mguu ambao kwa maelezo yake ulianza kumuuma tangu akiwa darasa la saba kwa kuvimba na mpaka anakutana na Harmonize alisema ilikuwa ni miaka minane amehangaika nao, mara ya mwisho alipewa majibu kuwa mishipa ya kusafirisha maji imeziba na hawana dawa zaidi ya kuuchua.

Mwananchi ilimtafuta Angela kujua ukweli wa malalamiko yake Basata, alijibu kwa kifupi: “Siwezi kulizungumzia hilo kwa sababu ni suala la mkataba na mkataba ni siri ya aliyesainishwa na aliyesaini. Pia sijui unazungumzia kitu gani”.

Sababu Harmonize kuachana na Anjela

Inadaiwa kuwa bosi huyo wa lebo ya Konde Music kutaka kuachana na Angela ni pamoja na kutorudisha faida ya kile walichowekeza kwake.

Nyota huyo alitambulishwa kwenye lebo hiyo Machi 11, 2021, ambapo aliachia wimbo ‘Kama’ aliomshirikisha Harmonize na mpaka sasa wimbo huo umeshatazamwa zaidi ya mara milioni tatu kwenye mtandao wa Youtube, mwingine ni ‘Sina Bahati’. Nyimbo zilizofanya vizuri kwa kupata watazamaji wengi Youtube ni ‘Nobody’ aliouachia mwaka 2021 uliotazamwa mara milioni nne na ‘Kioo’ aliomshirikisha Harmonize uliotazamwa mara milioni tano. Wimbo mwingine ni ‘Toroka’ na ‘Shulala’ ambao haujafanya vizuri mtandaoni.