Athari za moto masoko ya Mbeya bado zipo

Muktasari:
Miaka karibu 10 iliyopita, Mkoa wa Mbeya ulikumbwa na jinamizi la kuungua moto kwa masoko ambayo ndiyo kitovu cha uchumi wa wananchi na halmashauri.
Kwa kipindi cha miaka 10, Jiji la Mbeya liliunguliwa na masoko manne makubwa na maarufu, likiwamo la Mwanjelwa ambalo lilikuwa na wafanyabiashara karibu 9,00.
Baadaye wafanyabiashara hao walipewa eneo la Sido ambako soko la muda lilijengwa kwa vibanda vya mbao.Hata hivyo, soko hilo nalo liliungua baada ya mwaka mmoja na kusababisha wafanyabiashara 700 kupata hasara kubwa.
Haikutosha, soko jingine kubwa na la zamani kuliko masoko yote la Uhindini, liliungua katika kipindi hichohicho na kusababisha wafanyabiashara zaidi ya 600 kupoteza mali na fedha zao.
Jinamizi la moto likazidi kuyafuatilia masoko mengine, kwani baadaye soko dogo la Forest lilishika moto na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wasiozidi 200.
Soko la Tunduma katika wilaya ya Momba nalo lilishika moto na kusababisha Watanzania wengi kuamini kwamba moto huo ulikuwa na mkono wa mtu.
Tangu mwaka 2006, mpaka sasa, Jiji la Mbeya halina soko kuu licha ya wananchi wengi kupata huduma katika masoko madogomadogo ya Soweto, Uyole na Soko Matola.
Matumaini ya kurudi kwenye soko kuu la Mwanjelwa yananza kuonekana, kwani ujenzi unaoendelea sasa unatarajia kukamilika Aprili mwakani.
Hata hivyo, wafanyabiashara waliokuwa kwenye soko la Uhindini sasa wamekata tamaa, kwani hata dalili za kuwapo maandalizi ya ujenzi hazionekani.
Kwa hali hiyo vidonda vya kuungua kwa masoko bado vinawaumiza wafanyabiashara wakubwa na wamachinga pamoja na halmashauri.
Vidonda vya moto
Mfanyabiashara wa eneo la Sido, Atuganile Simambwe anasema kuungua kwa masoko kumesababisha apate hasara ya Sh30 milioni ambazo mpaka sasa hajazirudisha.
Tumpe Sanga wa Makungulu jijini hapa, anasema kuungua kwa soko la Mwanjelwa kumesababisha vijana wengi waliokuwa wakilizunguka soko kibiashara kupoteza mwelekeo.
Kwa upande wake, Efraem Mwamakamba wa Majengo, anasema tangu kuungua kwa soko la Uhindini kumempotezea mwelekeo wa maisha kwani mbali ya kuungua bidhaa zake, alipoteza wateja wa bidhaa waliokuwa wakitokea nchini Zambia.
“Jiji la Mbeya limejaa wamachinga barabarani kwa sababu masoko makubwa hayafanyi kazi, lakini kama masoko ya Mwanjelwa na Uhindini yakijengwa upya, upo uwezekano wa Wamachinga wote kurudi kwenye masoko hayo na jiji litarudi kwenye usafi,’’ anasema Mwamakamba.
Freddy Mwakasala wa Mwanjelwa anasema kuungua kwa masoko ya Mbeya kumekwamisha maendeleo ya jiji na wananchi wake.
Mwakasala anatoa mfano wa soko la Mwanjelwa ambalo anasema awali lilikuwa na wateja wengi kutoka Malawi, Zambia na DRC –Congo ambao kwa sasa hawapo.
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza anasema, moto uliounguza masoko hayo umesababisha athari kubwa kwa maendeleo ya jiji.
Anasema tangu kuungua kwa masoko hayo, mapato kupitia ushuru yaliyokuwa yakipatikana sokoni yalipungua kwa asilimia karibu 60.
Kwa mfano, ripoti ya utekelezaji wa kazi za jiji kwa kipindi cha Julai hadi Novemba 2013, inaonyesha jiji lilipanga kukusanya ushuru wa Sh10.8 bilioni kutoka vyanzo vyake, lakini katika kipindi hicho lilifanikiwa kukusanya Sh1.6 bilioni tu.
Jiji la Mbeya kwa sasa halipati ushuru wa kutosha kwa sababu wafanyabiashara wengi ni waathirika wa moto, hivyo hawalipi ushuru kwa madai walijenga vibanda kwa mikataba ya kipindi maalumu.
Tahadhari ya moto katika masoko
Pamoja na vidonda vya moto wa masoko Mbeya, jiji limefanikiwa kusimamia ujenzi wa soko kubwa la kisasa la Mwanjelwa kwa kupitia mkopo wa mabilioni ya fedha kutoka Benki ya CRDB.
Soko hili linatarajiwa kumalizika Aprili, 2015 na huenda likawarudisha wafanyabiashara waliotapakaa mitaani kwenye eneo moja.
Msimamizi mkuu wa ujenzi wa soko hilo, Joseph Sebe anasema soko hilo ni la kisasa na limewekewa vifaa maalumu vya kinga za moto.
‘’Jengo lina akiba ya lita za ujazo 200,000 za maji katika tanki na pia lina mipira 24 karibu kila kona ya jengo kwa ajili ya kutoa maji ya kuzima moto kama ukitokea,’’ anasema.
Sebe anasema jengo hilo pia limejengewa mitambo maalumu 10 ya kuzima moto unaotokana na umeme.
Kaimu Mkurugenzi wa jiji hilo, Dk Samuel Lazaro, anasema wanajenga soko hilo kwa tahadhari zote za kuzuia moto.
Kuhusu tahadhari ya moto katika masoko mengine yakiwamo ya Sido, Soweto, anasema kwa kushirikiana na wafanyabiashara, jiji limezuia upikaji wa vyakula kwenye masoko hayo.
‘Ni kweli ukipita katika soko la Sido yapo matangazo mengi yanayozuia kupika au kuwasha mishumaa au kufanya shughuli zozote zinazohusiana na moto ndani ya soko,’’ anakiri Ifumu Mwaibwe anayeishi eneo la Mwanjelwa.