Serikali itekeleze ahadi ya kuwainua vijana

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan aliwahi kusema ‘tuwaone vijana kama rasilimali na siyo tatizo’. Vijana wakitumika ipasavyo wana faida nyingi; kijamii na kiuchumi.

Kwa kutambua umuhimu, wingi na nguvu zao, mataifa makini duniani yanawekeza zaidi kwa vijana. Takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha zaidi ya watu bilioni 1.2 duniani ni vijana chini ya miaka 25. Takriban asilimia 90 kati yao, wanapatika katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan aliwahi kusema ‘tuwaone vijana kama rasilimali na siyo tatizo’. Vijana wakitumika ipasavyo wana faida nyingi; kijamii na kiuchumi.

Vijana wana shauku ya kuona misingi ya demokrasia inalindwa, uwapo wa uchumi endelevu na jamii yenye kujali uwiano kati ya wananchi. Vijana ni rasilimali ya kesho katika uongozi, ulezi wa familia na utumishi lakini ni mtaji wa leo unaotakiwa kulindwa na kuwezeshwa ipasavyo.

Takriban asilimia 50 ya watu wote duniani ni vijana. Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 Tanzania kulikuwa na watu milioni 22.5 wenye kati ya miaka sifuri mpaka 17 ambao ni sawa na asilimia 50.1 ya watu wote.

Vijana ni kundi ambalo lisipolelewa vizuri kuanzia ngazi ya familia linaweza kujiingiza kwenye unyang’anyi, ubakaji, wizi, vurugu hata kuanzisha na kuendeleza uasi na uhalifu mwingine kwenye jamii.

Vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa ajira, huduma za kijamii kama elimu, afya na ukosefu wa taarifa mbalimbali muhimu kwao.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na Idadi ya Watu (UNFPA) katika ripoti ya mwaka 2007, ilionyesha zaidi ya vijana 6,000 walikuwa wanaambukizwa virusi vya Ukimwi kila siku duniani.

Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015, imetoa ahadi kadhaa ambazo kila kijana anapaswa kushinikiza utekelezaji kwa njia sahihi na kwa kufuata taratibu bila kujali chama, dini, kabila, kipato au elimu.

Kwa kutaja kwa uchache ahadi za CCM 2015 kwa vijana zimetajwa katika ibara za 9, 10, 22(f,g), 25, 27, 29(g), 44, 47, 56, 57 g(vii), 59, 60 na 70. Ni vyema vijana tukajijengea utaratibu wa kusoma Ilani hii, ili tuweze kuhoji na kufuatilia utekelezaji wa Serikali.

Katika kukabilana na changamoto ya ajira Serikali imeahidi kuanzisha viwanda vidogo, kati na vikubwa. Pia, kuweka nguvu kubwa kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo zinaweza kuajiri vijana wengi.

Kipaumbele kitawekwa kwenye kilimo cha mbogamboga, matunda, maua, mbegu za mafuta na nafaka. Katika uvuvi, vijana watawezeshwa rasilimali za ufugaji wa samaki ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 10,000 mpaka tani 50,000.

Katika ufugaji, Serikali itawekeza kwenye vikundi vya vijana kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe, kuku, mbuzi na usindikaji wa mazao ya mifugo ikiwamo nyama, maziwa na ngozi.

Changamoto ya pili kwa vijana ni mitaji na Serikali imeahidi kupima mashamba ya wanyonge na maskini, ili waweze kupata hatimiliki ambazo wanaweza kutumia kupata mtaji kutoka kwenye taasisi za fedha.

Vijana kusaidiwa kwa kuunganishwa na wakati mwingine Serikali kuweka dhamana kwenye taasisi za fedha, ili waweze kupata mikopo ya pembejeo, zana bora na mashine za usindikaji kupitia Saccos.

Serikali kuhamasisha vijana waweze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuweza kunufaika na fursa mbalimbali ikiwamo mikopo nafuu inayotolewa. Pia, kuzielekeza halmashauri zote kwa vijana kupata zabuni za miradi ya Serikali inayotekelezwa vijijini.

Kuendelea kutoa asilimia tano ya mapato ya ndani ya kila halmashauri kwenda kwenye mifuko ya vijana. Pai, Serikali itaanzisha dirisha maalumu la mikopo kwa ajili ya vijana kwenye taasisi za fedha.

Hata suala mikopo limeahidiwa kwenye ilani hiyo. Serikali itahakikisha inatumia vyombo vyake kuwatafutia vijana masoko ndani na nje ya nchi watakayoweza kuuza bidhaa zao zitokanazo na kilimo, mifugo, uvuvi na ubunifu.

Ni mambo mengi ambayo CCM imeahidi na wakati mwingine inaendelea kuahidi kutekeleza kwa ajili ya vijana kipindi cha utawala huu.

Ni jukumu letu kufuatilia na kuihimiza Serikali kutekeleza ahadi zake kwa manufaa ya vijana wote. Pia, ni vyema kusoma na kuielewa ilani ya CCM ili tuwe na nafasi nzuri ya kuihoji Serikali kila tunapopata nafasi.

Kufaulu au kufeli kwa Serikali hupimwa kwa namna ilivyoitekeleza ilani yake ya uchaguzi, ambayo kwayo ilipewa ridhaa ya kuongoza nchi. Vijana ni nguvu kazi, tuwaamini, tuwashirikishe na kuwapa nafasi.

Naamini Serikali inatambua vyema umuhimu wa vijana katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Vijana wasitumike tu wakati wa uchaguzi, thamani yao itambulike na kuthaminiwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Kabla kampeni cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 haujasogea, kuna nafasi ya kutosha kuhakikisha ahadi zilizomo kwenye ilani zinafanyiwa kazi na Serikali.

Kwa wapiga kura makini na wote wenye ushawishi, walitumia ilani hiyo kuiwezesha CCM kupata ushindi ulioiwezesha kuendelea kushika dola hivyo ni wajibu wake kuhakikisha inatimiza ilichoahidi.

Vijana nasi tunapaswa kuwabana viongozi hawa kutekeleza haya badala ya kusubiri kutoa lawama baada ya kutotekelezwa kwa ahadi hizi.