Serikali yauwekea vigezo vipya uvunaji misitu Sao Hill

Muktasari:
- Msitu huo unakusanya mamilioni ya miti aina ya misindano na mikaratusi ndani ya shamba mojawapo kubwa la miti kwenye ukanda wa Afrika Mashariki linalomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
- Kutokana na umuhimu wake katika maeneo ulipo, hususan kwa jamii zinazouzunguka, Serikali imekuwa ikiweka mipango mbalimbali ikiwamo ile ya uvunaji na udhibiti wa moto, ambapo jamii inashirikishwa kama walinzi wa eneo hilo.
Sao Hill ni msitu mkubwa nchini uliopo wilayani Mufindi mkoani Iringa, ukiwa unaonekana vizuri pale mtu unapokuwa ukitumia usafiri wa barabara kutoka Iringa mjini kwenda Mbeya au utokapo mkoani Mbeya kwenda Iringa.
Msitu huo unakusanya mamilioni ya miti aina ya misindano na mikaratusi ndani ya shamba mojawapo kubwa la miti kwenye ukanda wa Afrika Mashariki linalomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Kutokana na umuhimu wake katika maeneo ulipo, hususan kwa jamii zinazouzunguka, Serikali imekuwa ikiweka mipango mbalimbali ikiwamo ile ya uvunaji na udhibiti wa moto, ambapo jamii inashirikishwa kama walinzi wa eneo hilo.
Katika shamba hilo, hekta 55,617.22 zimepandwa miti aina ya misindano na mikaratusi huku hekta 48,200 zikiwa na misitu ya asili ambazo ni kwa ajili ya vyanzo vya maji, ilhali hekta 29,933 ni kwa ajili ya upanuzi wa upandaji miti na 1,700 ni maeneo ya makazi na matumizi ya mengineyo. Miaka ya nyuma jamii inayoishi jirani na msitu huo iliwahi kushirikishwa katika upandaji wa miti kwa kugawiwa maeneo ili kuimarisha ujirani mwema baina ya msitu huo na wananchi.
Vigezo vipya uvunaji misitu
Kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, utaratibu wa uvunaji rasilimali katika msitu huo hazikujikita kufuatilia kwa kina nyaraka za wavunaji, ambapo waliotaka kufanya hivyo walifuata taratibu na kisha kupata vibali, lakini hakukuwa na uhakiki iwapo walikuwa na viwanda vya uchakataji miti au mbao.
Baada ya kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano, imeweka utaratibu maalumu unaopaswa kufuatwa na wavunaji wa mazao ya misitu lengo likiwa ni kuwatambua wahusika pamoja na kusukuma mbele dhamira ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.
Kwa mujibu wa utaratibu wa uuzaji wa malighafi katika mashamba 18 ya miti yanayomilikiwa na Serikali uliotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe mwezi uliopita mjini Dodom, msitu wa Sao Hill umewekewa utaratibu maalumu.
Profesa Maghembe anasema kanuni za misitu na mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu kuanzia sasa zinamtaka kila mwenye kuomba kuvuna miti kuwa na kiwanda cha kupasua magogo.
“Utaratibu wa vibali huwavutia waombaji wengi (wenye viwanda na wasio na viwanda) kwa kuwa kila mwombaji huona ana sifa stahiki. Kutokana na wingi wa waombaji uchambuzi wa kina unakosekana kubaini wenye sifa kwa kuwa wengi wa waombaji hudanganya kwa kujaza taarifa zinazoonyesha wamewekeza katika uchakataji wa magogo,” anasema Profesa Maghembe.
Waziri huyo anasema, uzoefu unaonyesha mwombaji mmoja anaweza kujaza fomu nyingi kwa majina tofauti ili kuongeza uwezekano wa kupata mgao, jambo ambalo husababisha waombaji wasio na sifa kupewa mgao na kusababisha waliowekeza kwenye teknolojia ya uchakataji magogo kupewa mgao kidogo.
“Viwanda vingi hufungwa muda mfupi tu baada ya kuanza uzalishaji kwa mwaka kutokana na uhaba wa malighafi. Tathmini iliyofanywa ilibaini kuwa asilimia 45 ya viwanda vya misitu 630 vimefungwa, huku asilimia 10 vikiwa vimekufa kabisa,” anasema.
Waziri anasema hali hiyo inainyima Serikali mapato na kuwa na wawekezaji wasio na matumaini na uhakika wa uwekezaji wanaoufanya.
“Ikiwa utaratibu huo utaendelea kwa kiasi kikubwa utaathiri uwekezaji kwenye sekta ya misitu na kusababisha ajira nyingi kupotea, hivyo kuongeza umaskini kwa familia mojamoja,” anasisitiza Profesa Maghembe.
Pia, anasema kwa kuwa waombaji wengi huwa hawajawekeza kwenye teknolojia za uchakataji magogo utaratibu huo huzalisha kundi la kati ambalo hufanya ulanguzi wa vibali, jambo linalolazimu kuuza vibali vyao kwa wale wenye viwanda.
“Biashara hii hufanyika kwa kificho. Utafiti unaonyesha biashara haramu ya vibali inasababisha kuongezeka kwa gharama kwa walaji. Kwa mfano, kwa mwaka 2015/16 kibali kimoja cha mita za ujazo 200 kiliuzwa kwa wastani wa Sh13.5 milioni,” anasema waziri huyo na kuongeza kuwa:
“Ikiwa mwenye kiwanda atauziwa kibali hicho bado atalazimika kulipia tena miti hiyo kwa bei ya Serikali na hivyo kufanya gharama nzima kufikia Sh27.3 milioni. Hii ni wastani wa Sh136,646 kwa mita za ujazo badala ya Sh60,000 ikiwa mnunuzi angepata kibali moja kwa moja toka serikalini.”
“Kuanzia sasa, mgao wa kuvuna miti katika mashamba ya Serikali utatolewa kwa wenye viwanda vya kuchakata magogo tu vilivyosajiliwa na kuhakikiwa na TFS. Kiasi cha mgao kwa kila mwombaji kitategemea ukubwa wa kiwanda, teknolojia, mahitaji kulingana na soko pamoja na wigo wa ajira anazozitoa. Utaratibu huu ukizingatiwa viwanda vitafanya kazi muda mrefu kwa mwaka kuliko hivi sasa.”
Kutokana na utaratibu huo mpya, Serikali imeazimia kuwa hakutakuwa na utaratibu maalumu kwa makundi ya kijamii au taasisi za dini kupatiwa mgao wa kuvuna bila kuwa wamekidhi masharti ya kuwa na kiwanda cha kuchakata magogo na kuhakikiwa.
“Hii inatokana na ukweli kwamba mahitaji maalumu sio kigezo cha kisheria na pia uzoefu umeonyesha kuwa kutoa mgao kwa makundi maalumu ni sehemu ya chanzo cha kuwepo biashara haramu ya kuuza vibali na kuikosesha Serikali mapato,” anasema Waziri Maghembe.
Ofisa Habari wa TFS, Tulizo Kilaga anasema shamba la Sao Hill limewekewa utaratibu maalumu unaotofautiana kidogo na yale mengine kwa kuwa ndilo kubwa, lakini pia linao wadau wengi zaidi sambamba na changamoto zilizopo.
“Mapendekezo mahususi kwa ajili ya shamba hili pamoja na kukidhi mahitaji hapo juu yatakuwa ni pamoja na kuwa na asilimia 10 ya mita za ujazo wa miti zitakazokuwa kwenye mpango wa uvunaji kwa mwaka husika ambazo zitavunwa na Serikali,” alisema Kilaga.
Kilaga alisema miti na magogo yatakayovunwa kwa utaratibu huo yatauzwa kwa wamiliki wa viwanda vya misitu watakaohitaji nyongeza kutoka mgao wa awali au kwa watakaokosa kwenye utaratibu wa awali na kwamba, mauzo hayo yatafanyika kwa kuzingatia bei ya soko na gharama za uzalishaji.
Wadau wapongeza mpango huo
Mpango mpya wa Serikali kuhusu uvunaji wa rasilimali za misitu umeungwa mkono na wadau ambao wanaona kwamba iwapo utasimamiwa ipasavyo, utakuwa mwarobaini wa matatizo yaliyowahi kujitokeza siku za nyuma.
Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wavunaji Sao Hill (Uwasa), Dk Bazil Tweve anasema kupitia barua yao kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo kuwa mpango huo mpya utagusa wahitaji halisi wa shughuli za uvunaji kwa maana ya wamiliki wa viwanda na misumeno.
“Pili, tangazo hili (la wizara) limetoa nafasi ya wadau kusoma majina na wale wanaoamini walistahili kuwepo na wana sifa kupitia ofisi ya meneja wafike kwenye ofisi kuthibitisha ustahili wa kuwepo kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002,” anasema.
Pia, anasema utaratibu huo utawapa nafasi nzuri ya kujieleza wale wenye sifa na kutambulika, jambo ambalo litamaliza malalamiko ya kipindi kirefu na kuiomba Serikali kuendelea kusimamia vyema mpango huo na wao kama wavunaji halali wapo tayari kutoa ushirikiano utakapohitajika.