Tamu, chungu mtoto kusoma bweni

Tuache mjadala nani anapaswa kusoma shule ya bweni nani hapaswi. Hata mjadala wa umri wa mwanafunzi kwenda bweni unaweza kutafutiwa siku yake!

Makala hii inajikita kuangalia kwa kina faida na hasara za mwanafunzi kwenda shule ya bweni na mustakabali wa shule hizo katikati ya janga la uporomokaji wa maadili, hasa baada kuibuka mjadala mzito uliotokana na agizo la Serikali kupiga marufuku wanafunzi wenye umri mdogo kukaa bwenini.

Machi 1 mwaka huu Serikali kupitia Kamishna wa elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa ilitoa waraka uliopiga marufuku shule za bweni kwa wanafunzi chini ya darasa la tano kwa lengo la kuwapa watoto fursa ya kushikamana na familia na jamii zao, kujenga maadili na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendelo ya familia na jamii zao.

Waraka huo unaelekeza huduma za bweni zitolewe kuanzia darasa la tano na kuendelea. Hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne isipokuwa kwa kibali maalumu kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi rasmi kutoka kwa mdau husika.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule uliotolewa na Wizara mwezi Novemba, 2020. Shule zote ambazo zinatoa huduma ya bweni kwa madarasa yasiyoruhusiwa zimetakiwa kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.


Faida shule za bweni

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus anaeleza kuwa shule za bweni zina faida kubwa katika mchakato wa kujifunza kuliko hasara zake.

Anasema shule hizo zinasaidia katika kuwajengea watoto uwezo wa kukua kiakili, kisaikolojia na kijamii, kwa sababu wanapata maarifa na stadi za maisha za namna ya kuchangamana na wengine.

“Ndiyo maana Nyerere alikuwa anapendelea kuwapeleka wanafunzi shule za bweni zilizo mbali na maeneo ya kwao kama njia mojawapo ya kulijenga taifa moja lisilo na ukabila. Mtoto anapotoka Kigoma kwenda Mara, Ruvuma, Tabora, au Kagera kwenda Mtwara anajifunza kuhusu jamii nyingine tofauti na za kwake na hivyo kuondoa dhana potofu za kikabila alizojifunza nyumbani kwake kama vile wazazi kumwambia watu wa kabila fulani hawafai,’’ anaeleza.

Mbali na hilo, Dk Kristomus anasema shule za bweni zinasaidia kupanua jiografia ya mtoto na kumfanya ajue maeneo mengine zaidi ya aliyozoea na hata akiwa mkubwa hawezi kuogopa kusafiri nje ya mazingira ya wazazi wake.

“Shule za bweni zinamjengea mtoto uwezo wa kujiamini na kujitegemea. Anapata muda wa kutosha wa kujifunza tofauti na akiwa nyumbani ambako kuna mambo mengi ya kumfanya asipate muda wa kujifunza peke yake na kujifunza na wenzake.

“Mazingira ya nyumbani kuna runinga, redio, simu, kazi za nyumbani, watoto wenzake na kadhalika. Hayo yote yatamfanya asijielekeze katika kufanya mazoezi ya darasani kwa ufanisi,” anasema.

Hata hivyo, anatahadharisha kuwa umri mzuri wa mtoto kwenda bweni ni zaidi ya miaka 12, kwani huo ni umri wa yeye kuweza kujitambua zaidi na kuchangamana vizuri na watoto wenzake.

Jumanne Mangage ni miongoni mwa waliopita shule za bweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, anasema binafsi imemsaidia kujiamini na kuwa na mpangilio wa vitu vyake ikilinganishwa na vijana wengi wa kiume ambao wamesoma shule za kutwa.

“Kila mtu ana namna anavyoyachukulia mambo, binafsi shule ya bweni imenisaidia kujua jinsi ya kupangilia vitu na mambo yangu. Siwezi kuondoka chumbani kwangu bila kutandika kitanda, kufanya usafi na kuweka vitu kwenye mpangilio, hivi vyote nilijifunzia shule za bweni. Pia kwenye suala la kutunza muda niko vizuri, yani hakuna dakika ninayotaka ipotee bila sababu ya msingi, tulikuwa tunafundishwa kutunza muda.

“Changamoto niliyoiona kwenye shule za bweni kama mwanafunzi hawezi kujisimamia maisha yanaweza kuwa magumu kwake, maana huko bwenini huishi na mwalimu hivyo ni lazima wewe mwenyewe uwe imara. Unajua kila sehemu kuna wababe, sasa kama ukiwe mzembe utakuwa mnyonge wao, utafulishwa nguo na kuwafanyia usafi, kuwabebea chakula na mambo kama hayo,” anasema Mangage.

Naye Vestina John anasema shule ya bweni imemfanya kujifunza kuishi na watu katika mazingira yoyote, jambo ambalo linamsaidia kwenye maisha yake ya sasa.

Anafafanua: “Bweni kunakuwa na mchanganyiko wa watoto waliotoka katika maisha tofauti, wapo kutoka familia zenye uwezo, wengine hali zao ni duni zaidi, wapo pia wanaotoka mijini na vijijini, hapa kwa pamoja mnakutana, binafsi nilijifunza kuchangamana na watu wa aina tofauti. Shule niliyosoma tulikuwa tunafundishwa kazi za mikono mfano kulima bustani, kufanya usafi, hivi vyote vinanifaa, kwa sasa nikiamua kuwa na bustani yangu ya mbogamboga naweza. Kingine ambacho hadi kesho nashukuru nilichojifunza ni ushirikiano, upendo na utayari wa kusaidia wengine, hivi ndivyo tulivyokuwa tunaishi bwenini.”


Wasemavyo wazazi

Akizungumza sababu ya kupendelea shule za bweni kwa watoto wake, Stella James anasema hufanya hivyo kwa sababu ya malezi kutokana na kukosa muda wa kutosha wa kuwa na watoto.

“Binafsi huwa naangalia performance (utendaji) ya shule na malezi, lakini kwa shule wanazosoma watoto wangu wala performance haiko juu, nimeangalia zaidi malezi, kutokana na maisha yalivyo sasa ni nadra kupata wasaa wa kusimama kikamilifu kwenye malezi, ndiyo maana huwa tunawakimbiza kwenye zile shule ambazo tunaamini watapata malezi yaliyo bora,’’ anasema na kuongeza:

“Kuliko kumuacha mtoto ajilee mwenyewe ni bora umpeleke sehemu sahihi. Hata hizi shule pia zina utofauti, sasa hapo ni wajibu wako mzazi kufanya utafiti kuipata ile ambayo inaweza kumlea mtoto katika misingi bora; mimi binafsi napendelea shule za kanisa,” anasema Stella.

Kwa upande wake, Victor Kasekwa anasema anapendelea shule za bweni kwa sababu zina uhakika wa mazingira bora ya mwanafunzi kujisomea tofauti na ilivyo kwa shule za kutwa ambapo wanafunzi hutumia muda mwingi wakiwa barabarani.

Anasema kutokana na uchovu wanafunzi wengi wa shule za kutwa hushindwa kujisomea wanapokuwa nyumbani na ndiyo mwanzo wa kutopata matokeo mazuri kwenye mitihani yao.

“Mwanafunzi anaamka alfajiri anaanza kuhangaika na usafiri, kuna uwezekano pia akafika shuleni kwa kuchelewa na mwalimu hawezi kurudi nyuma kwa sababu yake. Jioni hivyo hivyo anajikuta amefika nyumbani usiku, kwa mtindo huu ni vigumu kujisomea, tofauti na wanafunzi wa shule za bweni wana muda mwingi wa kujisomea.


Hasara nazo…

Mwanasaikolojia John Ambrose anasema zipo faida na hasara za kisaikolojia mtoto anapokaa shule ya bweni, huku akieleza hatari ni kubwa zaidi kwa watoto wenye umri mdogo kwa sababu endapo mazingira ya shule hayatakuwa yanawaruhusu kupata lishe bora upo uwezekano wa kudumaa.

“Mtoto anavyokua unatakiwa uwepo uwiano kati ya mwili na umri, sasa kama atakuwa hapati lishe bora ni rahisi kudumaa na hii tunazungumzia udumavu wa mwili hata akili. Hili linatokea zaidi kwa nchi maskini, hali ni tofauti kwa nchi zilizoendelea, huko suala la lishe kwa watoto ni kipaumbele mahali popote.

“Ukiachana na suala la lishe, mtoto mdogo anatakiwa kulelewa na wazazi wake ili iwe rahisi wao kumkuza katika miongozo na misingi wanayoitaka, sasa kama mtoto mdogo anaelelewa bweni kuna uwezekano mkubwa asiwe na misingi wala tabia za wazazi wake. Mtoto anakuwa na tabia kulingana na mazingira anayoishi, yale anayoyaona,” anasema Ambrose.

Kwa upande wake, Vestina anabainisha kuwa kama walimu na uongozi wa shule hawana ufuatiliaji wa karibu, shule za bweni zinaweza kuwa kichocheo kwa mwanafunzi wa bweni kuharibikiwa, endapo atafuata mkumbo wa makundi ya wanafunzi wenye tabia zisizofaa.

“Kama ambavyo nilisema awali watoto kutoka katika maisha na mazingira mbalimbali wanakutana pamoja, hivyo ndani yao kuna wanaokunywa pombe, wanaovuta bangi na hawa siku zote watataka kupata wenzao. Haya masuala ya usagaji yalikuwepo tangu miaka hiyo, ingawa nasikia siku hizi vijana wengi wa kiume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja walianzia huko kwenye shule za bweni,” anaeleza.