Aeleza alivyofukuzwa kwao alipofaulu sekondari

Mtwara. Mtoto mwenye umri wa miaka 16 (jina tunalihifadhi)ameeleza adha aliyoipata baada ya kufukuzwa nyumbani kwao na wazazi wake baada ya kufaulu kuingia kidato cha kwanza.

Akizungumza na Mwananchi juzi, mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Naishero alisema alilazimika kuishi kwa rafiki zake ambako alitakiwa achangie Sh1,000 kila siku, ili apewe chakula huku akishawishiwa kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na wenyeji wake.

“Nilipofaulu wazazi wangu walinitolea maneno makali, hali iliyonifanya nijihisi vibaya ndio maana hata waliposema niondoke, kweli niliondoka na kwenda kuishi na watu baki.
“Wazazi walisema hawana uwezo wa kunisomesha, nilipokutana na mwalimu aliwahoji kwa nini hawanipeleki shule.

“Usiku wake walinisema sana, kisha wakaniambia ikifika asubuhi nichukue kila kilicho changu nitafute pa kwenda,” alisema.
Hivyo, aliamua kwenda kwa rafiki yake na baadaye akaripoti jambo hilo kwenye ofisi za ustawi wa jamii.

“Nilikwenda ofisi za ustawi wa jamii nikawaelezea wakanipa Sh20,000 nikaenda kununua sare za shule na madaftari matano.

“Lakini nikiwa nyumbani kwao rafiki yangu, walikaa na kuzugungumza wakaanza kunishawishi nishiriki mambo mabaya kuwa kama sichangi Sh1,000 sili chakula katika nyumba hiyo,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliamua kwenda kwa rafiki mwingine aliyekaa naye hadi Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo alipomchukua na kuanza kuishi nyumbani kwake.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa wilaya hiyo, Chaurembo alisema mpaka sasa zaidi ya asilimia 97 ya wanafunzi wameripoti shuleni, ingawa zipo changamoto kwa watoto wengine ikiwamo kupata ujauzito.

Kuhusu mwanafunzi huyo alisema alipata taarifa zake baada ya kutembelea shule aliyopangiwa.
“Nilipata taarifa ya mtoto aliyependa kusoma, lakini bahati mbaya anaishi kwa marafiki, hali iliyonisukuma kuonana naye.

“Nikiwa kiongozi na mzazi pia niliona kuna umuhimu wa kumsaidia, ili kumuepusha na vishawishi vya marafiki zake waliomtaka achangie pesa ili aweze kuishi katika nyumba yao,” alisema.
Alisema mtoto huyo aliishi kwake kwa siku tano na ndipo wazazi wake walikwenda kuandika maelezo kuwa wako pamoja na mtoto wao, watamsomesha.

“Nikamruhusu arejee ili tusimtenganishe na wazazi na niliwataka watu wa ustawi wa jamii kumuangalia kwa ukaribu mtoto huyo,” alisema.

Hata hivyo, mama mzazi wa mtoto huyo, Singiziwa Ally alikanusha kumfukuza akisema alimtaka aende kwa baba yake mzazi anayeishi mbali na kijiji chao.

“Sisi tulimtaka aende kwa baba yake mzazi kumwambia mahitaji yake, lakini cha ajabu mtoto akaenda kukaa kwa marafiki, hata sisi tulishangaa,” alisema. Akimzungumzia mtoto huyo, mkuu wa Shule ya Sekondari Naishero, Mariam Msanya alisema alimpokea akiwa na barua kutoka ustawi wa jamii, baada ya mahojiano alimuona ni mtoto anayependa shule.

“Huyu mtoto anajitahidi katika masomo, licha ya changamoto anazopitia, anahitaji msaada wa wazazi na jamii,” alisema.

Ofisa ustawi wa jamii wa wilaya hiyo, Johari Rashid alisema shule ilipofunguliwa mtoto huyo alikwenda baada ya kusikia agizo la mkuu wa wilaya kwenda shuleni hata kama hawana sare.