Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya hapa mapendekezo ya HakiElimu kwenye bajeti ya elimu 2026/2027

Muktasari:

  • Inasisitiza bajeti ya mwaka 2026/27 ni ya maandalizi ya kuanza utekelezaji wa madarasa ya mkupuo kwa mwaka 2028, hivyo ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa sasa, mfumo wa elimu unaweza kukumbwa na changamoto ya msongamano wa wanafunzi na uhaba wa rasilimali.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) sambamba na mtaala mpya, Shirika la HakiElimu limesema bila mipango madhubuti ya bajeti, mabadiliko hayo yanaweza kuyumbisha mfumo mzima wa elimu nchini.

Shirika hilo limebainisha sekta ya elimu kwa sasa inakabiliwa na mabadiliko mawili makubwa ya kimuundo, ikiwemo kupunguzwa kwa muda wa elimu ya msingi kutoka miaka saba hadi sita, na kuanzishwa kwa mkondo wa elimu ya amali katika shule za sekondari.

Katika tamko lililotolewa na shirika hilo na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Mary Ndalo, limeeleza pia mapendekezo mengine kwenye bajeti ya elimu kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Mageuzi hayo yanahitaji maandalizi makubwa ya kifedha ili kuepusha sekta hiyo kukumbwa na msongamano na upungufu wa rasilimali.

Shirika hilo limebainisha kuwa mabadiliko hayo yanatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya miundombinu, walimu na vifaa vya kujifunzia, huku yakibadilisha kabisa mwelekeo wa utoaji wa elimu nchini.

Moja ya changamoto iliyoibuliwa ni uwepo wa kundi la wanafunzi wa mkupuo wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya wanafunzi milioni 1.6 wa ziada wataingia sekondari kwa wakati mmoja, hali inayotarajiwa kuongeza presha kubwa kwa shule zilizopo sasa.

Kutokana na hali hiyo, HakiElimu imeitaka Serikali kutenga angalau Sh2.12 trilioni katika bajeti ya mwaka 2026/27 ili kuweka maandalizi ya kutosha kwa mabadiliko hayo.

Kiasi hicho kinajumuisha gharama za ujenzi wa madarasa mapya, vyoo, maabara, ununuzi wa vitabu pamoja na ajira ya walimu wapya.

Kwa mujibu wa makadirio hayo, shule za sekondari zitahitaji kujengwa vyumba vya madarasa 35,564, vyoo zaidi ya 72,000 na kuajiri walimu wapya takribani 35,000 ili kufikia uwiano unaokubalika wa mwanafunzi na mwalimu.

Gharama za miundombinu pekee zinakadiriwa kufikia zaidi ya Sh1.06 trilioni, huku ujenzi wa maabara ukihitaji takribani Sh bilioni 449.57.

Aidha, gharama za vitabu vya kujifunzia kwa wanafunzi hao wa ziada zinatarajiwa kufikia Sh240 bilioni, wakati mishahara ya walimu wapya inaweza kufikia zaidi ya Sh362 bilioni kwa mwaka, kulingana na makadirio ya wastani wa mshahara wa mwalimu.

Pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali, ikiwemo kutenga Sh1.77 trilioni kwa ajili ya maandalizi, shirika hilo limesema fedha hizo bado hazitoshelezi kukidhi mahitaji yote, hasa upande wa rasilimali watu na uendeshaji wa mfumo mpya wa elimu.

Akizungumza bungeni Aprili 2, 2026, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali tayari imeanza kufanya tathmini ya mahitaji ya miundombinu ya elimu katika ngazi za mikoa na halmashauri.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kugharimu takribani Sh1 trilioni, fedha zitakazotumika katika ujenzi wa madarasa, maabara pamoja na miundombinu mingine muhimu katika shule za sekondari.

Moja ya mikakati mikubwa inayotekelezwa na Serikali ni kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya sekondari.

“Kutokana na mpango huo, kila kijiji kinatarajiwa kuhitaji angalau madarasa matatu ya ziada ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi watakaojiunga na sekondari,” amesema Dk Mwigulu.

Alisema tathmini ya awali inaonyesha kuwa ili kufanikisha mpango huo, nchi itahitaji kujenga zaidi ya madarasa 23,200 pamoja na maabara mpya 9,300.


Msisitizo kwenye elimu ya amali

Mbali na hilo, shirika hilo limependekeza kuanzishwa kwa kifungu maalum cha bajeti kwa ajili ya Mageuzi ya Elimu ya Amali ili kuhakikisha mkondo huo mpya haukwami.

Hadi sasa, ni asilimia 4.1 tu ya shule za sekondari nchini ndizo zina uwezo wa kutoa elimu ya amali, hali inayotajwa kuwa ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya taifa.

“Elimu ya amali inahitaji uwekezaji mkubwa zaidi, ikiwemo ujenzi wa karakana, ununuzi wa mitambo na vifaa vya ufundi, pamoja na ajira ya walimu wenye ujuzi maalum. Kuendelea kutegemea bajeti ya mkondo wa taaluma pekee kutadhoofisha utekelezaji wa mabadiliko hayo.

“Bajeti ya mwaka 2026/27 ni ya maandalizi. Ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa sasa, mwaka 2028 mfumo wa elimu unaweza kukumbwa na changamoto kubwa ya msongamano na uhaba wa rasilimali,” imeeleza sehemu ya uchambuzi huo.

Pendekezo lingine lililotolewa ni kuongeza uwekezaji katika sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu kwa kuimarisha hadhi ya kitaasisi ya sayansi, teknolojia na ubunifu (STI).

Shirika hilo limeeleza ipo haja ya kuwa na wizara au sekta inayojitegemea au mamlaka ya uratibu yenye nguvu sawa inayowajibika kwa sera za STI, ufadhili, udhibiti na uendelezaji wa ubunifu kibiashara.

“Ikiwa Tanzania ina dhamira ya kweli ya kuwa uchumi wa kipato cha kati cha juu unaoendeshwa na maarifa, ufadhili wa STI lazima uondoke pembezoni mwa bajeti ya elimu na kuwekwa katikati ya ajenda ya kitaifa ya mageuzi.

“Hii itasaidia kuzuia STI kumezwa na mahitaji mengi yanayoshindana ndani ya sekta ya elimu na kutoa mwelekeo mkubwa zaidi wa kisera kwa masuala yanayoibuka kama akili mnemba, utawala wa kidijitali, usalama wa mtandao, uendelezaji wa matokeo ya utafiti kibiashara na ujuzi wa nguvu kazi ya baadaye.”


Elimu jumuishi

Katika eneo la elimu jumuishi, shirika hilo limependekeza bajeti ya 2026/27 kutenga fedha zitakazosaidia mchakato wa kuifanya Lugha ya Alama (SL) kuwa somo la msingi katika mtaala wa shule za msingi na sekondari.

Sambamba na hilo, limependekeza kutengwa kwa bajeti maalumu kwa ajili ya ununuzi wa zana za kufundishia lugha ya alama, vifaa saidizi vya kidijitali na uajiri wa wataalamu wa lugha ya alama watakaopangiwa katika shule na taasisi zote za kujifunzia.

Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanafunzi wenye na wasio na ulemavu wa kusikia kuwasiliana, hivyo kuondoa ubaguzi na kuimarisha ujumuishi.


KKK

Shirika hilo limependekeza bajeti ya 2026/27 ianzishe fungu maalumu kwa Mkakati wa Kisayansi wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, fedha hizo zinapaswa kutengwa kwa ajili ya mafunzo ya walimu katika mbinu za ufundishaji za “kisayansi” na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia vinavyoendana na umri wa watoto.

“Tunaihimiza Serikali kuweka kipaumbele katika uajiri wa walimu waliobobea katika elimu ya awali. Kwa PTR ya sasa ya 1:151, ni vigumu kutoa msaada kwa mwanafunzi mmoja mmoja unaohitajika kwa ujifunzaji wa awali wa kusoma, kuandika na kuhesabu. Kwa hiyo, bajeti inapaswa kuweka mpango halisi wa kupunguza uwiano huu kuelekea lengo la 1:45 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

“Kwa kuzingatia uwiano wa darasa wa 1:81, bajeti ya 2026/27 lazima itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ‘rafiki kwa watoto wa elimu ya awali’ yanayokidhi mahitaji ya kipekee ya watoto wenye umri wa miaka 5, hususan vijijini na maeneo yasiyohudumiwa vya kutosha.”