Mzigo unavyowaelemea walimu wanaofundisha elimu ya awali

Dar es Salaam. Walimu wa madarasa ya awali katika shule za Serikali wanalazimika kufundisha wanafunzi takribani mara sita ya kiwango kilichowekwa na Serikali jambo ambalo wadau wametaka lishughulikiwe ili kupata matokeo tarajiwa.

 Mwaka 2022, mwalimu mmoja alikuwa akifundisha wanafunzi 142 ndani ya darasa moja ikiwa ni idadi kubwa kuliko wanafunzi 25 waliotakiwa kwa viwango vya Serikali, Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2022 inaeleza.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, walimu 10,093 waligawana wanafunzi milioni 1.435 waliosajiliwa mwaka 2022 katika shule hizo.

Wanafunzi waliosajiliwa mwaka jana ilikuwa ni ongezeko la asilimia 11.1 kutoka wanafunzi milioni 1.291 walioandikishwa mwaka 2021.

Hata hivyo, kati ya walimu tajwa hapo juu, 1,493 kati yao hawana sifa za kufundisha darasa la awali na wanaobakia ndiyo wenye sifa. Hiyo inafanya uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kuongezeka hadi kufikia wanafunzi 162 ndani ya darasa moja.

Uwiano wa walimu wenye sifa kwa wanafunzi waliodahiliwa unatajwa kupungua kutoka wanafunzi 180 waliokuwapo mwaka 2021 lakini jitihada zaidi zinapaswa kufanyika ili kuweza kupata matunda yaliyotarajiwa.

“Ongezeko la waliaondikishwa katika shule za awali lilitokana na kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo utekelezaji wa programu ya elimu msingi bila ada pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika upande wa walimu, Serikali ilisema inatokana na jitihada za Serikali kutoa ajira mpya za walimu.

Akziungumzia suala hilo, Mtafiti wa Elimu Muhanyi Nkoronko alisema uwekezaji katika elimu ya awali ni wa muhimu kwani ndiyo inayomjengea mwanafunzi uwezo wa kumudu masomo katika ngazi zinazofuata.

“Asipopata elimu stahiki ya awali hawezi kufanya vyema madarasa yanayofuata, Serikali iwekeze katika vitendea kazi ikiwemo walimu na si walimu tu walimu bali walio bora na wenye sifa za kufundisha madarasa ya awali,” alisema Nkoronko.

Alisema bila kufanya hivyo, maendeleo ya mtoto huathirika kielimu na kufanya ugumu katika kumudu masomo yao ya ngazi za juu.

“Idadi ya wanafunzi ikiwa wengi darasani mwalimu anashindwa kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja, uwekezaji uongezeke ikiwemo katika kujenga madarasa ili wakae wachache, mwalimu amfikie mwanafunzi mmoja mmoja kwa sababu anatakiwa kuweka juhudi zaidi kwa wenye uelewa mdogo na wa polepole (slow learner) kuliko yule anayeelewa haraka,” alisema Nkoronko.

Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Lyambene Mutahabwa alisema elimu ya awali ndiyo itakayomuandaa mtu anayehitajika ndani ya nchi kama ni mwalimu, mhandisi au mwanasayansi.