Ndani ya Habari: Hivi ndivyo watoto nchini wanavyoenda shule

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyeburu wakigombania kuingia kwenye daladala ambalo limeshajaa abiria kama walivyokutwa juzi katika kituo kilichopo Chanika, Dar es Salaam. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Wanafunzi wa ngazi hiyo wanaoishi mijini wanatumia wastani wa dakika 25.5 kufika shuleni ikilinganishwa na mwaka 2014/2015 ambapo walitumia dakika 22.5, takwimu hizi zinaonyesha kuwa muda umeongezeka kidogo.

Wakati Serikali ikiendelea kuboresha sekta ya elimu nchini na kutoa huduma hiyo bila malipo, muda na usafiri unaotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi nchini kufika shuleni umeendelea kuwa mwiba kwao.

Ripoti ya utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2020/2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha asilimia 92.6 ya wanafunzi wa shule za msingi nchini wanaenda shuleni kwa miguu.

Takwimu hizi ni sawa na kusema kati ya wanafunzi 10 wa shule za msingi nchini, tisa wanaenda shuleni kwa kutembea (kwa miguu), kitendo ambacho kinasababisha muda wa kufika shule kutokea nyumbani kwao uongezeke.

Ripoti ya NPS ya mwaka 2014/2015 ilionyesha wanafunzi hao wanatumia wastani wa dakika 27.6 kufika shuleni huku muda ukiongezeka hadi kufikia dakika 29.9 mwaka 2020/2021.

Hata hivyo, ripoti hiyo mpya imeonyesha hali ni mbaya zaidi vijijini ambapo mwanafunzi wa shule ya msingi anatembea wastani wa dakika 31.5 kufika shuleni ikilinganishwa na dakika 29.4 walizotumia mwaka 2014/2015.

Wanafunzi wa ngazi hiyo wanaoishi mijini wanatumia wastani wa dakika 25.5 kufika shuleni ikilinganishwa na mwaka 2014/2015 ambapo walitumia dakika 22.5, takwimu hizi zinaonyesha kuwa muda umeongezeka kidogo.

Utafiti huo uliofanywa na NBS kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) ilihusisha kaya 3,352 nchini.

Mtafiti na mdau wa elimu, Nicodemus Shauri anasema wanasiasa ni chanzo cha tatizo hilo kwa sababu wao wana ushawishi wa kupanga sehemu ambazo shule zinatakiwa zijengwe.

“Tangu shule zimeanza kujengwa nchini kiuhalisia ongezeko lake ni dogo na mikakati ilikuwa shule zijengwe karibu na makazi ya watu ili kuwe na urahisi kwa wanafunzi kufika. Lakini kwa sasa wanasiasa na watu wenye ushawishi wanazipeleka maeneo wanayoamua wao,” anasema.

Shauri anasema umbali mrefu na wanafunzi kutembea kwa miguu inawaathiri katika utulivu katika masomo yao.

“Hii lazima itaongeza muda kwa wanafunzi kufika shuleni na inaweza kuathiri utulivu na ‘concentration’ (uzingativu)kwenye masomo yao,” anasema.

“Kuhusu wanafunzi kuchelewa lazima utafiti zaidi ufanyike, takwimu zichambuliwe katika ngazi ya jinsi ili tupate picha kubwa,”anaongeza.

Shauri alipendekeza uwepo wa magari ya shule ambayo yataakuwa yanawachukua wanafunzi hao nyumbani kwao hadi shule na kuwarudisha.

“Kuondoa wanafunzi kutembea kwa miguu ni kutumia mabasi ya shule ambayo kwa shule za Serikali ni ngumu kwa sasa, kwa sababu sio kipaumbele chao na watasema hawana fedha,” anasema.


Athari kutembea umbali mrefu

Tatizo la umbali mrefu kwa wanafunzi kufika shuleni, limewahi kufanyiwa utafiti mwingi nchini ambapo athari kubwa imeonekana kwenye kushusha ufaulu wa wanafunzi.

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Kitaaluma cha Gitoya (G-CARD) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) mwaka 2021, ulioitwa ‘Mtazamo wa wadau wa elimu kuhusu athari za umbali wa shule kutoka nyumbani katika ufaulu wa wanafunzi miongoni mwa shule za sekondari za Serikali katika Wilaya ya Rorya, ulionyesha umbali mrefu unamsababisha mwanafunzi achelewe kufika shule na kukosa baadhi ya masomo, hivyo kuwa katika hatari ya kutofaya vizuri kwenye masomo.

“Umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni unawafanya wanafunzi wengi kuchelewa kufika shuleni na kukuta masomo yameanza, jambo linalosababisha wanafunzi kukosa sehemu ya utangulizi au kipindi chote kinachoanza mapema,” inasema ripoti ya utafiti huo.

Inaongeza: “Baadhi ya wanafunzi wanafika wakiwa wamechoka na kutokwa na jasho kutokana na safari ndefu. Uchovu kwa wanafunzi, husababisha umakini duni na kupelekea kuwapo kwa ufaulu duni kwa wanafunzi hao.’’


Wasemavyo wadau

Mtaalamu wa saikolojia, Naima Omary anasema kutembea kwa miguu kwenda shule, kunaweza kuyumbisha akili ya mtoto na kumfanya ashindwe kuwaza masomo kwa kiasi kikubwa na badala yake awaze aliyokutana nayo njiani.

“Akili ya binadamu inahitaji utulivu ili kufanya kitu kwa ufanisi, kama mtoto atatembea kwa miguu tena kwa umbali mrefu, njiani anakutana na vitu vingi pengine vitamfanya aviwaze zaidi kuliko masomo ya siku hiyo,”anasema.

Naima aliongeza: ‘‘Uchovu pia ni madhara ambayo mtoto atayapata endapo atatembea kwa umbali mrefu, atafika amechoka sana na umakini kwenye masomo yake utakuwa mdogo, inaweza kumsababishia asifanye vizuri,”anasema.

Athumani Ngitola, mjasiriamali katika eneo la Mabibo mwisho jijini hapa alisema wanafunzi wengi wa mjini wakiwa wanaenda shule kwa miguu wanapata shida ya kuvuka barabara na hiyo inawachelewesha sana kufika shule.

“Hawa watoto wanahangaika sana kuvuka barabara hadi utawaonea huruma. Mimi binafsi nawasaidia kuwavusha kama nisipokuwa bize maana kuna hatari wasipoongozwa na mtu mzima,”anasema.

Ngitola anasema kwa siku moja anaweza kuwavusha wanafunzi kuanzia 50 hadi 70 kutegemeana na siku husika.